Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Anayechelewesha Baleke kutangazwa Yanga ni huyu

Baleke Yanga.jpeg Anayechelewesha Baleke kutangazwa Yanga ni huyu

Fri, 19 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kumekuwa na maswali mengi juu ya kushindwa kutambulishwa kwa Jean Baleke licha ya straika huyo wa zamani wa Simba kuonekana mazoezini na kuwa kwenye msafara wa Yanga unaoenda Afrika Kusini na Mwanaspoti likajaribu kuchimba kujua ukweli.

Wachezaji wengi waliopo katika vilabu mbalimbali nchini DR Congo wanamilikiwa na watu binafsi, Agency na Academy, hivyo ukiuziwa mchezaji au ukipewa kwa mkopo lazima pia umalizane na watu wanaommiliki mchezaji huyo.

Inaelezwa pamoja na Baleke kupewa mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, pia bado ni mchezaji wa TP Mazembe ambao walimsajili mwaka 2021 akiwa na miaka 19 kwa mkataba wa miaka mitano, hivyo klabu zinazomhitaji lazima zizungumze na wahusika, hata hivyo Yanga imemalizana na klabu hiyo ya DR Congo, lakini ugumu upo kwa Al Ittihad ya Libya aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo.

Tunafahamu kwamba Baleke, alibakiza mkataba wa miezi sita na Al Ittihad, kwani alisaini mwaka mmoja na ametumikia nusu, hivyo inawia ngumu Yanga kutangaza kwa sababu itaonekana imesajili mchezaji wa klabu nyingine na itaingia kwenye mgogoro na Walibya. Kwa upande wa wakala wake, Jeunnesse Sportive de Kinshasha (JSK) yeye hana shida kwa sababu anataka mteja wake apate timu nzuri na acheze.

Chanzo cha taarifa hiyo kinasema, “Yanga tumemalizana na TP Mazembe, ishu inakuja timu aliyotokea ndio tunashughulikia hilo, ili tuwe huru na mchezaji wetu. Ndio maana amerudishwa Kennedy Musonda ambaye tulikuwa na lengo la kuachana naye, lakini nisisitize tunaendelea kulishulikia.”

Mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kupita Simba na kufunga jumla ya mabao 16 kwa msimu mmoja na nusu, amekuwa akionekana katika uwanja wa mazoezi na klabu ya Yanga.

Lakini pia ni sehemu ya wachezaji waliosafiri kwenda Afrika Kusini kwenye mechi za Kirafiki dhidi ya FC Augsburg ya Ujerumani.

Yanga wako hatua za mwisho kumalizana nao na huenda Baleke atatangazwa Yanga kabla dirisha la usajili la (CAF) halijafungwa hapo kesho Julai 20, 2024.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live