Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amunike kuifumua Taifa Stars

49698 Amunike+pi

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miaka 39 ya kuhangaika si mchezo. Mwaka huu walau Tanzania imekata tiketi ya kucheza fainali za Afrika zitakazofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Kocha Msaidizi wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, Emmanuel Amunike ndiye aliyefanhya kazi ya kuivusha Tanzania kwenye fainali hizo ambazo mwaka huu zimebadilishwa mfumo lakini pia timu kuongezeka kutoka 16 hadi 24.

Tanzania ilikata tiketi baada ya kuibandua The Cranes ya Uganda mabao 3-0 mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Uganda kupoteza kwenye michuano hiyo kwa mabao ya Saimon Msuva, Erasto Nyoni na Aggrey Morris.

Amuneke na vijana wake wamemaliza nafasi ya pili katika Kundi L wakiwa na pointi nane wakati Uganda imemaliza na pointi 13. Timu nyingine katika kundi hilo ni Lesotho iliyomaliza na pointi sita wakati Cape Verde pointi tano.

Uganda na Tanzania kutoka Afrika Mashariki zinaungana na wenyeji Misri, Nigeria, Senegal, Morocco, Mali, Algeria, Ghana, Zimbabwe, Ivory Coast na Angola kucheza fainali hizo.

Nyingine zilizofuzu ni Tunisia, Cameroon, Guinea-Bissau, Madagascar, Burundi, Benin, Afrika Kusini, Kenya, DR Congo, Guinea, Mauritania na Namibia.

Droo ya fainali hizo imepangwa kufanyika Aprili 12 Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Cairo, Misri.

Timu 24 kutoka katika makundi 12, zitapangwa katika vyungu vinne kulingana na ubora wa viwango na timu zitapangwa kwenye makundi manne yenye timu sita tayari kwa fainali hizo.

AMUNIKE ALIVYOPAGAWA

Vyombo mbalimbali vya habari hasa Nigeria vimempongeza Amunike kwa kazi nzuri kiasi cha kuipa sifa Tanzania lakini pia kujitengenezea CV ya kuivusha Tanzania katika fainali za Afrika kwa mara ya pili na katika kipindi kirefu.

Mtandao wa Concise News wa Nigeria ulimkariri Amunike akisema: “Inawezekana ni Mungu, inawezekana ni wachezaji, au inawezekana ni hamasa ya Watanzania iliingia hadi kwa wachezaji…

“Lakini wakati nilipokuja hapa, mkutano wangu wa kwanza na waandishi wa habari, ilikuwa Agosti mwaka jana, nilisema kitu kimoja, ni jitihada na kujituma kwa wachezaji ndio njia pekee itakayotuvusha, ninaamini ni jitihada.”

Kocha huyo aliyekipiga klabu ya Barcelona ya Hispania miaka ya nyuma, anakuwa kocha wa pili Mnigeria kupeleka timu kwenye fainali za Afrika akitanguliwa na marehemu, Stephen Keshi aliyeibeba Togo pia kwenda Fainali za Misri mwaka 2016.

Amunike, pia aliwahi kuzinoa Julius Berger, Ocean Boys, pamoja na timu ya Taifa ya Nigeria ya U-17 kabla ya kutua Al Khartoum SC. Pia Amunike aliiongoza Nigeria kutwaa Kombe la Dunia kwa vijana wa U-17 mwaka 2015 nchini Chile.

ANAVYOITAZAMA TANZANIA

Amunike, ambaye pamoja na kusema ni jitihada za wachezaji, lakini anasema pia kuwa ni Mungu amewabeba wachezaji wa Tanzania hata wakafuzu kwa miaka 39.

Akizungumza na Shirika la Habari la Nigeria, (NAN) kwa simu kutoka Dar es Salaam, Tanzania, Amunike anasema: “Tunamshukuru Mungu kwa kuwezesha Tanzania kufuzu fainali hizi.

“Kufuzu kwetu ni nguvu ya Mungu. Pia, sapoti ya Watanzania ambao wenyewe walishasema wanataka kwenda Afcon.”

Anasema kwamba kilikuwa kitu cha kufurahisha kwa Watanzania milioni 55 kushangilia kufuzu Fainali za Afrika.

Kocha huyo anasema kuwa kuna kazi kubwa ya kuiweka Taifa Stars katika muundo unaotakiwa wa kucheza fainali zitakazofanyika Misri na kwamba kinachotakiwa ni maandalizi ya maana na timu iwe na mlengo mmoja wa ushindi.

“Tumefuzu lakini kuna kila sababu ya kubadilisha mawazo yetu kwamba tumefuzu sasa inatakiwa maandalizi kwa ajili ya mashindano makubwa mbele yetu.

“Watu hawaangalii kufuzu kwetu, kitakachoangaliwa ni matokeo kwenye fainali za Misri,” anasema.

Kocha huyo anasema kuna haja ya kufumua kikosi kwa kuongeza wachezaji wapya Taifa Stars kwa ajili ya kuongeza nguvu na zaidi ni kutokana na ugumu wa fainali zenyewe.

“Mchezaji yeyote ambaye ameonyesha uwezo, kiwango na hata nitakaowaita nitawaangalia na sitakuwa na sababu ya kuacha kuwajumuisha kwenye kikosi kitakachokwenda kwenye fainali.

“Kazi iliyopo mbele kwa sasa si ya kitoto, inahitaji maandalizi ya kweli na wachezaji wenye kiwango kikubwa,” anasema Amunike katika mahojiano na NAN.

AMUNIKE ASIFU MASHABIKI

Akizungumza na gazeti la This Day, la Nigeria, Amunike anasema kwanza alikuwa akiona usiku ni mrefu kiasi cha kuwaza nafasi ya Tanzania kufuzu Fainali za Afrika.

Anasema kuwa alikuwa akiamini kuwa Tanzania itafuzu kwa mikakati iliyowekwa na kila mmoja anataka kuona timu imevuka hatua hiyo muhimu.

“Usiku wa ushindi ulikuwa wa aina yake. Nimefurahi kupewa kazi ambayo nimeimaliza kwa jinsi tulivyopanga. Tuliweka mkakati kuwa lazima tushinde na tulishinda na zaidi ni kufuzu fainali.

“Tanzania kuna umoja na soka inawaunganisha wengi. Naona kila mmoja amefurahi hapa kila Mtanzania ana tabasamu la kupata ushindi kwenye mechi hii illiyotuvusha kwenda Cairo.

“Mtazamo wangu, kwa sasa, ni kuangalia wapi tumekosea, wapi pa kuongeza na pia kuangalia kule Cairo, Misri tutapangwa na nani,” Amuneke aliiambia This Day kwa simu.

Kuhusu kuongeza mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), straika huyo aliyekuwa kwenye kikosi cha Nigeria kilichoshinda mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa Afrika 1994 nchini Tunisia anasema mpango wake ni kuangalia nini cha kufanya kwenye fainali hizo na zaidi ni kufanya maajabu. Hata hivyo,

“Wakati huu si wa kuzungumzia suala la uhusiano wangu na FA. Cha kwanza, wachezaji wangu wameleta furaha kwa taifa la Tanzania na mimi ninafurahi kuwa sehemu ya wanaofurahi na sitaki kuona furaha inaisha katika kipindi kifupi,” Amunike alisema.

Hata hivyo, TFF juzi ilisema katika taarifa yake kwamba Amunike ataendelea kuinoa timu hiyo.

Amunike, anasema katika mchezo na Uganda alitazama mashabiki wa Tanzania waliokuwa majukwaani wakishangilia baada ya mchezo wa Lesotho na Cape Verde kumalizika naye akalazimika kushangilia kinamna akiamini sasa ameshaivusha Tanzania.

SAFARI YA STARS LAGOS 1980

Itakumbukwa Agosti 26,1979 wakati Taifa Stars ilipokuwa ikirudiana na Zambia enzi hizo ikiitwa ‘KK Eleven’ katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika Lagos, Nigeria.

Katika pambano hilo lililochezwa mjini Ndola, nje kidogo ya jiji la Lusaka, Taifa Stars ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili ifuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1968.

Timu hizo zilikuwa zinarudiana baada ya wiki mbili za mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars kuilaza Zambia bao 1-0 lililofungwa na kiungo, Mohammed Rishard Adolph.

Lakini ushindi huo haukuwa rahisi kwani mechi ilikuwa ngumu na hata kufuta matumaini ya mashabiki wengi kama timu yao ingefuzu.

Katika mchezo huo wa marudiano, ‘Kenneth Kaunda Eleven’ walipata bao la mapema katika mchezo huo ambalo lilidumu hadi dakika ya 85.

Taifa Stars wakati huo ilikuwa chini ya Kocha, Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama.

Dakika tano za mwisho, mshambuliaji wa Pan African wakati huo, Peter Tino alibadili sura ya mchezo kwa kusawazisha bao na kunyamazisha umati wa mashabiki waliofurika kwenye Uwanja wa Ndola.

Katika mchezo huo, ilipigwa kona kuelekezwa lango la Stars, lakini kipa wake, Juma Pondamali ‘Mensar’ akaupangua kwa ngumi, ukamkuta kiungo Leodegar Tenga ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Hussein Ngulungu ambaye naye alimgongea pasi ndefu Tino aliyeukwamisha kimiani.

Lakini kabla ya kufunga, akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino aliwatoka mabeki hao na alipofika nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia, alitandika kombora la mguu wa kulia, lililompita kipa wa Zambia aliyekuwa kikwazo, John Shileshi.

Katika mchezo ule Tanzania iliwakilishwa na; Juma Pondamali aliyekuwa langoni, Leopard Tasso, Mohammed Kajole/ Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.



Chanzo: mwananchi.co.tz