Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amrouche asiigeuze Taifa Stars kuwa maabara

Kocha Taifa Stars Kusaka Wachezaji Zanzibar Amrouche asiigeuze Stars kuwa maabara

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BAADA ya timu ya taifa ya soka, Taifa Stars kukubali kipigo cha mabao 2-0 mbele ya Morocco, maoni ya baadhi ya watu yamekuwa eti ‘timu imejitahidi, tulicheza dhidi ya Morocco ambayo ni bora’.

Hakuna aliyekuwa anataka timu ijitahidi, bali ishinde mechi hiyo muhimu ya makundi ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia. Afrika imepanga makundi tisa ambayo kila moja litatoa timu moja itakayofuzu moja kwa moja kwenda fainali hizo zitakazofanyika mwaka 2026 katika nchi za Marekani, Mexico na Canada.

Timu Nne Bora zitakazoshika nafasi ya pili, zitapambana kutafuta mshindi ambaye atakwenda kupambana na washindi wengine wa aina hiyo kutoka mabara mengine kupata timu moja kwa ajili ya fainali hizo.

Kwa hiyo kila mechi katika hatua hii ya makundi ni muhimu na haitoi nafasi ya aina yoyote kujaribu kikosi kwa matarajio kuwa iwapo yatatokea makosa yatasahihishwa baadaye.

Ni dhahiri kuwa hakuna mnyonge kwenye kundi letu kwa kuwa mabadiliko yamekuwa ni makubwa sana na ndio maana matokeo ya mechi nyingine za hatua ya makundi yamekuwa ya kushangaza. Usingetegemea Nigeria ilazimishwe sare nyumbani na Lesotho, au Afrika Kusini ikubali kipigo cha mabao 2-0 mbele ya Rwanda au Ghana ipate ushindi wa mbinde.

Lakini leo hii kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche anajaribu wachezaji katika mechi ya nyumbani dhidi ya Morocco, timu iliyofika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 zilizofanyika Qatar.

Tulitegemea kuwa mechi kama hiyo ingepewa umuhimu mkubwa, hasa kutokana na hamasa iliyowekwa kuanzia kwa mashabiki, klabu hadi Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, ambaye licha ya kutoa ndege ya kuisafirisha timu kwenda nje katika mechi ya kwanza, alinunua tiketi zote za mzunguko kuhamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia Stars.

Lakini saa chache kabla ya mechi yakaanza mazingaombwe. Kikosi kilipotangazwa, kila mmoja alishikwa na butwaa. Yaani Mbwana Samatta na Simon Msuva wanaanzia benchi? Yaani Aishi Manula anaanzia benchi. Basi kwanini asianze Kakolanya? Yaani Dickson Job anaanzia nje?

Yaani Kibu Denis ndio aanze kama mshambuliaji wa kati? Kwani timu haina mshambuliaji asilia?

Maswali yalikuwa mengi, lakini ule ustaarabu wa kuheshimu taaluma ya wengine ukatawala. Na hata matokeo mengine yaliyopatikana bila ya Mohamed ‘Tshabalala’ Hussein na Shomari Kapombe ukawafanya watu wafunge midomo kwa kuwa kumekuwa na matokeo ya kushangaza bila ya wachezaji tegemeo. Sare ya bila kufungana na Algeria nyumbani, ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Niger na ushindi dhidi ya Uganda uliwafanya watu wasihoji mengi.

Majibu ya maswali hayo ndio yangeweza kutuliza watu, lakini nayo yakawa mazingaombwe. Kwamba makipa wote waliumia ndio eti Amrouche akalazimika kumtumia Kawawa, ambaye hajawahi kucheza hata mechi moja ya kimataifa.

Alikuwa na Metacha Mnata ambaye alimuacha wakati timu ikienda Morocco kucheza mechi ya kwanza kwa maelezo kuwa angemuita wakati wa maandalizi ya mechi ya marudiano, lakini hakumuita. Mechi dhidi ya Morocco ingekuwa ugenini, kocha angeweza kueleweka, lakini mechi iko nyumbani na Metacha yupo, tatizo lilitokea wapi? Kwani Manula na Kakolanya waliumia dakika chache kabla ya mchezo?

Wakati Samatta ndio silaha yetu kubwa, kocha aliona aanzie benchi, huku Clement Mzize, ambaye pia ni mshambuliaji asilia wa kati hakuwa kwenye kikosi chake. Kocha alitaka kutuonyesha maajabu.

Nikasikia anasema eti watu wamezoea kumuona Samatta na Msuva, wakati wako wachezaji wengine. Hao wengine ni Kibu kucheza nafasi ambayo hajawahi kuicheza katika ngazi ya taifa wala klabu. Leo Kibu anapangwa katika mechi ngumu dhidi ya taifa lililoendelea kisoka Afrika na inawezekana duniani. Anajaribishwa katika mechi ambayo timu inahitaji matokeo mazuri.

Ni dhahiri Samatta na Msuva wangeilazimisha Morocco iwe na woga na icheze kwa uangalifu kuliko vile ilivyokuwa huru kwenda mbele kana kwamba inacheza nyumbani.

Kama timu ilionyesha kiwango kile bila ya Samatta na Msuva, ni dhahiri kuwepo kwa wiwili hao tangu mwanzo kungeweza kutupa matokeo tofauti na kule ‘kujitahidi mbele ya timu bora’.

Baadhi wanasema Morocco ilishinda kutokana na ubora, lakini lile bao la kwanza lilitokana na ubora wao? Halikuwa na ubora wowote zaidi ya udhaifu wa kipa ‘wa majaribio’. Na kwa kudhihirisha kuwa alikuwa wa majaribio ameahidi kujisahihisha na kwamba timu itakuwa vizuri mechi zijazo. Kwanini isiwe vizuri mechi iliyopita?

Unaweza kukubaliana na bao la pili kwa sababu lilitafutwa kimbinu na pengine makosa madogo kwenye ngome ndio yalisababisha kuruhusu bao. Ni bao la kimchezo na lililotafutwa kiufundi.

Watanzania wamekuwa kimya tangu Amrouche apewe timu na amekuwa hataki kuwajibika kwa wananchi ambao kodi zao ndio zinamlipa mshahara. Na kwa kiburi hicho amefikia hatua ya kuanza kuigeuza Taifa Stars kuwa maabara ya kujaribisha vitu vyake. Kwanini asiombe mechi za kirafiki kwa ajili ya kujaribisha wachezaji anaodhani ni wazuri?

Mechi za kufuzu huwa hazitoi nafasi kwa makocha kufanya majaribio kwa kuwa wachezaji hukusanywa ndani ya siku tatu na ya nne huwa ni mechi. Kwa hiyo, kocha hulazimika kutumia wachezaji walio tayari na ambao walishajaribiwa (tested) na si kuwajaribu katika mechi ya mashindano.

Huwezi kumjaribu mchezaji ambaye umekaa naye kambini siku mbili. Ni lazima uwe na uhakika naye sana. Ndio maana hatushangai Dickson Job anapochezeshwa pembeni kwa kuwa alishajaribiwa.

Ni lazima Amrouche ajue Watanzania wamechukia kuigeuza timu yao kuwa maabara na mamlaka zimjulishe hilo. Kama kuna wakati ambao mwanga wa kufuzu unaonekana japo kwa mbali ni wakati huu ambao nafasi za kwenda fainali kwa Afrika zimeongezeka kutoka tano hadi tisa na ikiwezekana kumi. Huu ni wakati wa kutumia kila silaha iliyopo kutafuta nafasi hii na si kuweka akiba silaha kwenye vita kali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live