Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amrouche arudia kosa la Amunike

Adel Amrouche Stars Amrouche arudia kosa la Amunike

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwaka 2019 Tanzania ilifuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ikiwa ni mara ya kwanza baada ya takribani miaka 39 na mara ya pili katika historia. Kocha wa Tanzania alikuwa nyota wa zamani wa Barcelona na shujaa wa Nigeria kwenye AFCON za mwaka 1994, Emmanuel Amunike.

Nasema shujaa wa Nigeria kwani yeye ndiye aliyefunga mabao mawili muhimu yaliyoipa Nigeria ushindi wa 2-1 dhidi ya Zambia na kuwa mabingwa katika mchezo wa fainali.

Baada ya kuisaidia Tanzania kufuzu, Amunike akaita kikosi chake cha kushiriki fainali zile zilizofanyika Misri.

Amunike alianza kwa kumuacha Jonas Mkude ambaye wakati ule alikuwa na kiungo bora wa ulinzi aliyeisaidia Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini kosa kubwa zaidi lilikuwa katika uchaguzi wa mabeki wa kati, yaani namba nne na namba tano.

Katika eneo hilo Amunike aliwaita wakongwe Aggrey Morris kutoka Azam FC na Kelvin Yondan kutoka Yanga. Pamoja na Ali Mtoni ‘Sonso, (marehemu), Vincent Philipo kutoka Mbao FC ya Mwanza na Abdi Banda kutoka Baroka FC ya Afrika Kusini.

Baadaye ukafanyika mchujo wa mwisho na kumpunguza Abdi Banda na kubaki na hao wengine.

Amunike ambaye alichezea Barcelona iliyokuwa na wachezaji wakubwa kama Ronaldo de Lima, ni kama alikuwa hajui alichokuwa anakifanya.

Timu ikaenda Misri na kucheza mechi mbili za kirafiki; dhidi ya Zimbabwe na Misri.

Katika mechi dhidi ya Misri, Aggrey Morris akaumia vibaya kiasi cha kuyakosa kabisa mashindano.

Amunike akalazimika kuita beki mwingine kujaza nafasi, akamuita David Mwantika kutoka Azam FC ambaye hakuwepo hata kwenye kile kikosi cha awali.

Katika hali ya kawaida ilitarajiwa kikosi kilichoitwa awali ndicho chenye wachezaji wa kutegemewa, kuliko wale watakaoitwa baadaye. Na wale waliokwama kwenye mchujo ndiyo walipaswa kuitwa wakati wowote ikitokea shida kwa waliopenya mchujo. Lakini hiyo haikuwa kwa Amunike. Akamuacha Banda na kumuita Mwantika kujazia nafasi.

Kuondoka kwa Aggrey Morris kungetoa nafasi ya beki mmoja wa kati ya Vincent Philipo na Ali Mtoni Sonso kucheza pamoja na Kelvin Yondan ambaye ndiye aliyekuwa pacha ya Aggrey.

Halafu Banda angeitwa kuziba nafasi ya yule mmoja aliyeingia kikosini kuziba nafasi ya Aggrey.

Lakini haikuwa hivyo, Mwantika aliyeitwa kwa dharura akaenda kuingia kwenye timu na kuwaacha akina Ali Mtoni na Vincent Philipo kwenye benchi.

Hapo ndipo Amunike alipojichanganya. Kama Mwantika alikuwa bora zaidi ya Ali Mtoni na Vicent Philipo, kwanini alimuacha katika kikosi alichokiita mwanzo?

Haya ndiyo makosa anayoyarudia Amrouche. Katika kikosi chake, kamuita Abdulmajid Zakaria kutoka Namungo ambaye msimu huu wote hajacheza mechi zinazofika tano.

Yaani mchezaji wa Namungo ambaye hapati nafasi kule, anaitwa timu ya taifa kwenda AFCON na kuachwa wanaocheza kila siku kama Edward Charles Manyama wa Azam FC au Albdulmajid Mangalo wa Singida Fountain Gate?

Hatuombei walioitwa wapate majeraha kama Aggrey Morris mwaka 2019, lakini ikitokea hivyo kwa bahati mbaya, ina maana Abdulajid Zakaria ndiye atakayecheza?

Kama hawezi kucheza pale Namungo, atawezaje kucheza kwenye timu ya taifa, tena kwenye fainali za AFCON? Makocha ni watalaamu na wanatakiwa kuachwa wafanye kazi zao kitaalamu. Lakini mambo kama haya huwafanya watu wasiwaamini na kushindwa kuwaacha wafanye kazi zao kwa uhuru kwa sababu wanaweza kuharibu.

Amrouche alianza kuonesha dalili za kuharibu kwenye uitaji wa kikosi chake, pale alipomuacha Lusajo Mwaikenda wa Azam FC ambaye alikuwa akicheza kila mechi klabuni kwake na kumuita Israel Patrick Mwenda wa Simba ambaye alikuwa akıkaa benchi tu klabuni kwake. Baadaye aibu ikamsuta na kumpa nafasi Mwaikenda na kumuacha Israh, lakini bado akaharibu kwa Zakaria. Hapa sisemi kwamba angeitwa Manyama au Mangalo ndiyo lazima Tanzania ingefanya vizuri, la hasha. Ninachosema ni kwamba timu ya taifa itumike kama zawadi kwa wachezaji wanaofanya vizuri.

Kuita timu ya taifa bila kuzingatia kiwango cha mchezaji husika katika wakati husika, ni kuunajisi mpira. Kuchezea timu ya taifa kunatakiwa kuwe matunda ya uwekezaji katika weledi na kujituma kwa kila mchezaji.

Hii itawafanya wachezaji wajitume zaidi wakiamini kocha wa timu ya taifa anawafuatilia na chochote kinaweza kutokea. Lakini wanapoitwa wachezaji kama Zakaria wa Namungo ambaye hata hachezi, kunawavunja moyo wale wanaojituma na kujitoa kwelikweli.

Chanzo: Mwanaspoti