Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amrouche anavyojibebesha msalaba Taifa Stars

Adel Amrouche Stars Amrouche anavyojibebesha msalaba Taifa Stars

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Juzi usiku kocha mkuu wa timu ya Taifa ‘TaifaStars’, Adel Amrouche alitangaza kikosi cha wachezaji 35 watakaoingia kambini kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Niger na Morocco.

Stars ipo kundi E na itaanza kutupa karata yake ya kwanza Novemba 18 dhidi ya Niger kwenye Uwanja wa Stade de Marrakech, Morocco.

Miongoni mwa wachezaji aliowaita kocha huyo amemrejesha kiungo Feisal Salum ‘Feitoto’ ambaye alikosekana takriban mara mbili licha ya kelele kutoka kwa wadau wa soka kuwa alistahili kutokana na kiwango chake. Feitoto hadi sasa amefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara.

Katika kikosi chake Fei sio mshambuliaji wa kati, bali kiungo mshambuliaji na sasa kurejea kwake ni wazi alistahili.

Majina mengine ambayo Amrouche ameyatangaza yameacha midomo wazi wadau wa soka kama ilivyo hapa chini.

KIPA

Katika eneo hili Amrouche amewaita makipa watano ambao ni Beno Kakolanya, Aishi Manula, Abuutwalib Mshery, Kwesi Kawawa na Metacha Mnata. Miongoni mwa sehemu ambazo zimeonyesha kuwa na sintofahamu kwenye uteuzi ni makipa hawa.

Hakuna utata kwa Kakolanya ambaye alikuwa mbadala wa Manula kwa muda mrefu na hata alipokuwa ameumia (Manula), yeye alisimama langoni na Stars ikafuzu Afcon 2023.

Kurejea kwa Manula pia langoni sio ishu kubwa kwa sababu tayari ameshapona na juzi kati alionekana kwenye mechi ya watani wa jadi dhidi ya Yanga.

Ishu ipo kwa makipa watatu Metacha, Mshery na Kawawa ambao wameitwa huku kukiwa na makipa wengine walioonyesha viwango bora na hakuna ambaye hajui hilo. Kukosekana kwa Ally Salim wa Simba ambaye amekuwa mbadala wa Manula pale Simba ni wazi kunaacha maswali.

Ally alisimama langoni Simba kwenye mechi kali na nyingi wakati Manula akiwa majeruhi, lakini hajaitwa huku akiitwa Mshery ambaye mara yake ya mwisho kukaa langoni ni msimu uliopita. Kama ni katika kumtengeneza Mshery kwa miaka ya baadaye, basi ukweli ni kwamba hawa wote (na Ally Salim) umri wao unakimbizana.

Kwa upande wa Mnata, kwa sasa hana nafasi mbele ya Djigui Diarra pale Yanga, lakini yupo kikosini Stars, hivyo ni wazi wangeitwa makipa wengine ambao wanafanya vizuri kwa sasa kwa sababu timu ya Taifa sio ya wachezaji walewale.

Yupo Wilbol Maseke anayeidakia KMC na Aaron Kalambo (Dodoma Jiji) ambao wamezifanya timu zao ziwe kwenye nafasi tano za juu Ligi Kuu ambao wangeitwa ili kuchota uzoefu.

Kalambo aliwahi kujumuishwa kwenye timu ya Taifa Tanzania ambayo ilicheza fainali za Mataifa Afrika (Afcon 2019) Stars ikiwa chini ya Emmanuel Amunike.

MABEKI

Kitendo cha kuwaita Omary Mvungi (FC Nantes) na Edwin Balua (Tanzania Prisons) kama mabeki kinaacha maswali pia.

Mvungi ni mshambuliaji wa kati akiwa nchini katika kituo cha Cambiaso na hata kwenye klabu yake ya sasa - FC Nantes nchini Ufaransa anatambulika kuwa mshambuliaji wa kati.

Kuitwa kwa wachezaji hao kama mabeki maana yake kunawanyima nafasi wachezaji wengine wanaocheza nafasi hizo kupata muda wa kuichezea timu ya Taifa.

Kikosi cha Stars kilitarajiwa kuingia kambini juzi kuwa na siku takriban saba za mazoezi ambayo kocha anatakiwa kumtengeneza Mvungi kutoka kwenye ushambuliaji kuja kwenye kukaba jambo ambalo kama angewaita wenye asili ya ukabaji ingekuwa rahisi kucheza.

Kwa Balua huwa anacheza kutoka kushoto au kulia, hivyo kama anakwenda kutumika beki katika pande hizo wapo wachezaji Aboubakar Ngalema (kushoto), Kelvin Kijiri (kulia) na Anderson Shekimweri (kulia) wanamudu vyema na tumeona wameziweka wapi timu zao katika Ligi Kuu Bara.

Ni wazi Amrouche kwenye mechi hii anataka kwenda kukaba, lakini kutuita washambuliaji kwenye eneo la ukabaji huku wakiwa hawajawahi kucheza na muda mfupi uliopo wa kuwaweka kwenye mfumo inafikirisha.

USHAMBULIAJI

Suala ni mazoea? Basi lipungue kwa Stars kwani ipo wazi nafasi ya John Bocco ni ndogo na hilo lipo hata katika klabu yake, Simba ambako anaanzia benchi na wakati mwingine haingii kabisa uwanjani. Lakini Amrouche ameendelea kumuita. Kweli ni mkongwe na inawezekana akawa anatoa ushauri kwa vijana, lakini yupo Mbwana Samatta na Simon Msuva ambao wanaweza kufanya kazi hiyo. Kuitwa kwa Bocco kunaendelea kuwanyima nafasi washambuliaji wengine wanaocheza ligi za ndani na wamefanya vizuri hadi sasa.

WASIKIE WAKONGWE

Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Stars, Zamoyoni Mogella anasema kitendo cha kurejeshwa Manula na kutoitwa Salim kunaweza kumvuruga kisaikolojia mchezaji huyo.

“Sijajua benchi lilikaa vipi. Nimeona wamemrejesha Manula, sasa ufiti huo kaupata wapi? Tuache kwenda kwa mazoea yule Ally alikuwa anahitaji mwendelezo timu ya Taifa na kama hajajengwa vizuri kisaikolojia tunaweza kumpoteza,” anasema.

Upande wa washambuliaji kuitwa kama mabeki, Mogella anasema inaweza isiwe tatizo kwa sababu soka la sasa limebadilika. “Zamani mshambuliaji unaambiwa tu haya Mogella nenda kafunge, lakini kwa siku za karibuni sayansi imebadilika mno, mchezaji unaweza cheza popote pale.”

Naye mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko anasema: “Wachezaji wengi wanaoitwa ni kutengenezewa hali ya kujiamini. Upande wa washambuliaji kucheza kama mabeki kwa sasa ni jambo la kawaida kwa kocha atakavyocheza.”

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Stars, Hery Morris anasema kocha anatakiwa ajue timu ya Taifa inabadilika muda wowote kulingana na viwango vilivyopo vya wachezaji wakati husika.

Morris anasema: “Upande wa Manula sishangai sana hata kama hana utimamu wa mwili, lakini ameshadaka mechi nyingi zenye presha hivyo ikitokea hatacheza kuna kitu anaongeza kwenye benchi pale.”

Chanzo: Mwanaspoti