Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Adel Amrouche ni kama ameaga Fainali za Afcon baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kumfungia mechi nane kutokana na kauli zake alizozitoa dhidi ya Morocco.
Adhabu hiyo ilitolewa jana na Kamati ya Nidhamu ya Caf, baada ya malalamiko yaliyowasilishwa na Shirikisho la Soka la Morocco (RMFF), likimlalamikia kocha huyo kwa kauli zake kuwa Morocco ina ushawishi ndani ya Caf katika kupanga mechi pamoja na maamuzi.
Kocha huyo aliyeingia Stars mwaka 2023 na kuiongoza kufuzu Fainali za Afcon zinazoendelea Ivory Coast, tayari ameiongoza Stars kwenye mechi moja ya fainali hizo dhidi ya Morocco na kufungwa mabao 3-0.
Hiyo inaweza ikawa mechi yake ya mwisho kwa Stars ambayo iko kundi F na Morocco, Congo na Zambia.
Stars imesaliwa na mechi mbili kwenye hatua ya makundi dhidi ya Zambia Januari 21 na DR Congo Januari 24. Hii ina maana mbali na michezo hiyo miwili, Amrouche atakosa michezo mingine minne kama Stars itafika fainali kutokana na idadi ya mechi alizofungiwa.