Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amini usiamini, Kimataifa Singida wamo

Amisi Tambwe Amissi Tambwe

Fri, 31 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Ammis Tambwe amesema wanajipanga msimu ujao kushiriki mashindano ya kimataifa na ahadi yao kwa mashabiki ni kufanya vizuri michezo iliyobaki.

SBS inashika nafasi ya tatu (3) kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 48 huku Yanga ikiongoza na pointi 65 na Simba inashika nafasi ya pili na pointi 57.

Timu hiyo imebakiza michezo mitano, mitatu nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania, Yanga na Ruvu Shooting huku mechi za ugenini zikiwa dhidi ya KMC na Namungo.

Aprili 2 mwaka huu SBS itacheza robo fainali michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Tambwe ambaye amewahi kuwika na timu za Simba na Yanga alisema licha ya ugumu wa mashindano mbalimbali wanayoshiriki lakini wanaamini watashiriki mashindano ya kimatifa msimu ujao.

“Ni faraja na furaha kwetu msimu wetu wa kwanza kwenye ligi lakini tumefanya vizuri na kupata matokeo katika michezo mingi tuliyocheza, tutacheza michuano ya kimataifa na tutafanya vizuri,” alisema nyota huyo ambaye aliipandisha daraja timu hiyo wakati huo ikiitwa DTB.

Kuhusu kutopata nafasi ya kikosi cha kwanza, Tambwe alisema kocha ndiye mwenye jukumu la nani aanze lakini akadai aliumia na sasa amepona na kama atapewa nafasi ataisaidia timu yake.

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, John Kadutu alisema ujenzi wa uwanja wa timu hiyo uliopo eneo la Mtipa mkoani Singida unaendelea.

Alipoulizwa umefikia hatua gani, Kadutu alisema; “Subiri subiri mambo mazuri zaidi yanakuja."

Hata hivyo, inaelezwa uwanja huo unatarajiwa kuwekwa kapeti hivi karibuni na msimu ujao timu hiyo itautumia katika Ligi Kuu Bara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live