Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amerudi! Nabi apumua, sasa Krosi zitamiminika

Djuma Shabani Beki wa Kulia wa Yanga Djuma Shaban

Fri, 11 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiwango cha Yanga dhidi ya Mbeya City kimemkera Kocha Nasreddine Nabi, lakini akasisitiza kwamba baada ya mechi yao na Biashara wana jambo lao.

Kocha huyo ambaye tangu juzi amewarejeshea mastaa wake programu nzito ya mara mbili kwa siku, ametamba kwamba wanarudi na staili yao ya krosi za kasi na mabao na wataanza kuonyesha makali hayo kwenye mechi na Mtibwa kumalizia mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu huku Manungu, Turiani.

Alisema ujio beki wake Mkongomani Djuma Shaban anayecheza beki ya kulia kwenye mechi na Mtibwa utakuja sambamba na staili mpya ambazo wamezifanyia kazi mazoezini kwenye siku hizi chache kuhakikisha Yanga inarejesha makali yake. Djuma alikosa mechi tatu zilizopita akiwa amesimamishwa kwa kumpiga kiwiko beki wa kulia wa Polisi Tanzania, Yahaya Mbegu katika mchezo wa ligi wiki chache zilizopita.

Tangu kusimamishwa kwa Djuma, Yanga imekuwa ikiwatumia mabeki Paul Godfrey ‘Boxer’ katika mechi moja ya Shirikisho huku ile ya ligi akicheza Dickson Job ambao wote Nabi hakuonyesha kuridhishwa na ufanisi wao kwenye staili yake ya uchezaji.

Nabi amegundua kwamba katika mchezo wa Mbeya City, Job ambaye halisi anacheza beki wa kati lakini alishindwa kupiga hata krosi kutokea pembeni.

Mbali na Djuma pia beki wa kushoto, Yassin Mustapha, Nabi alisema kwamba anaweza kuwa tayari kucheza kufikia wiki ijayo wakiwafuata Mtibwa Sugar kule Manungu ambako amesisitiza watapambana kwa namna yoyote.

“Djuma na Yassin wana ubora mkubwa wa kupita pembeni na kutengeneza krosi za kutosha, hii ni nguvu ambayo katika mechi kadhaa zilizopita tumeikosa na sasa watarudi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tulikuwa na ubora mdogo katika kuzalisha mashambulizi katika maeneo hayo hili lilitukwamisha sana ingawa nawapongeza waliocheza kwa kuwa tulizuia vizuri na hatujaruhusu bao wala kupoteza hili ni kubwa nalo.”

Nabi alisema alipanga kufanyia kazi aina ya timu ambazo hucheza na wachezaji wengi nyuma ya mpira na kwamba kurejea kwa wachezaji hao kutatengeneza nguvu mpya ya kuwa na mbinu mbadala katika kuzalisha mashambulizi.

“Timu nyingi kama Mbeya City wanajua nguvu yetu kubwa ni kuwa bora kutoka eneo la katikati ya uwanja sasa tukiwakosa watu bora wa kutengeneza mashambulizi tukitokea pembeni tutakuwa na akili mbadala ya kutafuta ushindi,” alisema Nabi akisisitiza bado wako kwenye kasi nzuri na mzunguko wa pili wataingia na nguvu kubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live