Safari yoyote ya mafanikio huanzia chini na ndivyo ilivyo kwa nyota wengi wa kimataifa wanaopambana kwenye ligi kubwa duniani. Maisha ya msoto hayana tofauti kwa Dickson Ambundo ambaye ameweka ndoto kubwa katika mchezo huo.
Tangu aanze soka lake amepita klabu za Mbao FC ya Mwanza, Lipuli ya Iringa, Gor Mahia ya Kenya, Dodoma Jiji ya Dodoma, Yanga na sasa Singida Fountain Gate ya Singida, anasema safari yake ndio kwanza imeanza na anataka kucheza timu kubwa zaidi ya alizopita ikiwamo Yanga.
Winga huyu anayefanya vizuri katika timu ya Singida aliyoanza kuitumikia rasmi msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake na Yanga, alifanya mazungumzo na gazeti hili na kueleza mengi ikiwamo safari yake nzima ya soka mpaka kucheza Kenya na baadaye kurudi Tanzania, na ilikuwaje hadi kutua Yanga na namna alivyotamaniwa na timu za Ligi Kuu. Pia anafafanua sababu za yeye kuonekana alipungua makali alipokuwa Yanga na ishu yake na Gor Mahia ilivyomalizika.
Mwanaspoti: Ulikuwa nyota mkubwa Dodoma Jiji, ilikuwaje ukaenda Yanga? Ambundo: Yanga ni moja kati ya timu nilizozipenda. Niliona itanifaa na kilichonivuta zaidi ni malengo yao kwani ilikuwa imewaka sana wakati huo hivyo sikuwa na sababu ya kuchomoa ofa yao ilipoletwa mezani na nilisaini kutumika miaka miwili pale.
Mwanaspoti: Vipi kuhusu kucheza timu kubwa zaidi? Ambundo: Nina umri mzuri na ninaamini nafasi ya kucheza timu kubwa zaidi ya Yanga ipo.
Mwanaspoti: Ukiwa Yanga kiwango kilishuka, unazungumziaje hilo? Ambundo: Sio kweli. Makali yangu hayakupungua. Yanga ni timu kubwa sana na kuna wachezaji wa kila namna. Sio rahisi kupata nafasi kama watu wanavyofikiria. Kocha ana machaguo yake na tunatofautiana viwango. Hivyo shabiki anaweza kuona mimi ni bora zaidi lakini kocha asione hivyo. Nilijitahidi kuonyesha kila jitihada zangu nilipopewa nafasi ya kuitumikia timu yangu.
Mwanaspoti: Yanga ilikuwa na mafanikio kwenye misimu miwili kabla hujaondoka na kutua Singida, kwenye mafanikio hayo, kipi unajivunia zaidi? Ambundo: Nina vitu vingi ila naweza kusema vikubwa viwili.
Medali ya CAF ni heshima kubwa ambayo ninayo na kila ninapokwenda kama mchezaji inaniongezea thamani na kunitofautisha na wengine. Kingine ni kucheza na wachezaji wakubwa wenye uwezo kunizidi, hii ilinifundisha vingi hadi sasa naitumia hapa nilipo kwani niliondoka na ujuzi mkubwa.
Mwanaspoti: Tunafahamu ulichezea Gor Mahia ya Kenya ukitokea Alliance. lakini kule Gor hamkuachana vyema. Kwanza ulipataje dili la Gor Mahia na kilitokea nini ukaondoka vile?
Ambundo: Nilianza kuchezea timu nyingi ikiwamo Mbao FC, Alliance na nilikuwa na rekodi nzuri ya ufungaji mabao hadi kufikia hatua ya kuwa mchezaji bora wa mwezi wa Ligi Kuu. Wakati huo nilitamani kupata kiatu kabisa hivyo Alliance ilinitambulisha kwenye dunia ya soka hadi Gor wakaleta ofa ya kuhitaji huduma yangu.
Mwanaspoti: Ilikuwa ni mara ya kwanza kucheza soka nje ya nchi, maisha ya Gor Mahia yalikuwaje? Ambundo: Maisha yalikuwa mazuri kwani nilitoka Alliance kwa heshima hivyo kule nilipokewa kwa heshima na kuichezea kwa mafanikio makubwa na kuendelea kutangaza jina langu hadi sasa niko hapa.
Mwanaspoti: Kipi kilikuondoa Gor na vipi kuhusu sakata lako na timu hiyo baada ya kuvunja mkataba, ilikuwaje?
Ambundo: Nilitoka kule kwa sababu ya Janga la Corona na lilisitisha shughuli zote ikiwemo michezo. Hivyo, tulikubaliana na Gor niondoke na walitakiwa kunilipa lakini walisitasita hivyo nikaenda Fifa ili nipate haki yangu. Nashukuru Fifa walilimaliza vizuri na kupata haki yangu nikiwa nimeshaondoka huko na hivyo nimeshamalizana nao.
Mwanaspoti: (Alitua Dodoma Jiji baada ya kuondoka Kenya na alicheza kwa msimu mmoja kabla ya mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga kuona kiwango chake na kumpa mkataba wa miaka miwili kuitumikia wana Jangwani. Hata hivyo kwenye soka hasa la nchi tofauti kuna utofauti). Unauzungumziaje utofauti wa soka la nje na hapa nchini?
Ambundo: Inategemea na nchi ila kwa Kenya kuko tofauti kwa upande wa mashabiki, huku watu wanapenda soka zaidi ila karibia vingi tunaendana.
Mwanaspoti: Na ni nini kilikupeleka Dodoma Jiji na sio kwingine kama timu kubwa za Yanga na Simba wakati ulitoka timu kubwa Kenya? Ambundo: Niliporudi nilikuwa mchezaji huru. Ofa ya Dodoma Jiji ilikuwa nzuri na sikuwa na sababu ya kuikataa.
Mwanaspoti: Vipi maisha ya Dodoma uliyaonaje? Ambundo: Nashukuru nilicheza kwa mafanikio makubwa na hadi kuzitamanisha timu kubwa kunisajili na Yanga kufanikiwa kwenye hilo kwani uwezo ndio ulinibeba.
Mwana spoti: Kuna stori zilizuka umesitishiwa mkataba na Yanga, vipi kuhusu hilo na umecheza timu nyingi sasa uko Singida Fauntain Gate, kwanza niambie ilikuwaje ukaamua kwenda Singida na si kwingine?
Ambundo: Nilishaanza mazungumzo na Singida baada ya kuona mkataba wangu na Yanga unamalizika, Singida walizungumza na mimi na nikachagua kuwa nao kwani ni timu nzuri na yenye malengo makubwa na ina nafasi nzuri Ligi Kuu. Pia si kama watu wanavyofikiri, sikuvunjiwa mkataba na Yanga bali nilimaliza muda wangu na kuondoka nikiwa huru.
Mwanaspoti: Unayaonaje maisha mapya Singida? Ambundo: Huku bado ni mazingira mapya kwa hiyo bado tunaendelea kuzoea ila ni mazuri hayana shida wachezaji wengi nafahamiana nao.
Mwanaspoti: Umekuja Singida na umepata namba kikosi cha kwanza moja kwa moja. Nini siri kuhusu hilo? Ambundo: Hakuna kitu rahisi katika maisha bali ni juhudi na machaguo ya kocha, hakuna cha ziada. Ila kubwa ni kuipambania namba.
Mwanaspoti: Yanga na Singida zina tofauti gani kwako? Ambundo: Hakuna utofauti sana kwani zote zipo Ligi Kuu na ziko nafasi nzuri na zote zinacheza kimataifa.
Mwanaspoti: Maisha ya Yanga na Singida lazima yana utofauti nje ya uwanja, vipi bata la Yanga lilikuwaje? Ambundo: Ilikuwa ni timu kubwa na tuliishi kama familia kubwa yenye upendo na amani, ijapokuwa matatizo madogo madogo hayakosekani ila niliyafurahia maisha yale zaidi kuliko timu nyingine nilizopita.
Mwananspoti: Kuna wakati wewe na Saido Ntibazonkiza mlipata kashikashi mkiwa Yanga baada ya kudaiwa kutoroka kambini jijini Mwanza. Hii ishu ilikuweka kwenye wakati gani hasa kwa kocha?
Ambundo: Hali haikuwa nzuri hasa ukikosea na kocha alitoa adhabu. Kwangu hakikuwa kipindi chepesi kwani masikio ya wengi yalitaka kujua uamuzi wa mwisho utakuwaje. Niliamua kuomba msamaha mapema kwani nilijua makosa ni yangu na mambo yalimalizika salama.
Mwanaspoti: Kila mchezaji ana staili yake ya ushangiliaji, Fiston Mayele alitisha na staili yake ya kutetema. Yako ni ipi na ina maana gani? Ambundo: Nina aina nyingi za ushangiliaji ila wengi wanaifahamu ile kama bishoo na haina maana, ila nimejikuta napenda tu kufanya hivyo kila nikifunga bao.
Mwanaspoti: Wewe ni mtu wa aina gani? Ambundo: Mimi ni mkimya sana na sipendi maneno na mtu kama kuna kitu unataka kujua kunihusu niulize mwenyewe, naamini nitakujibu vizuri kuliko mtu mwingine kwani hakuna anayenifahamu vizuri zaidi yangu. Nagombana na wengi kwani wanapata taarifa za uongo wakati wana uwezo wa kuniuliza na nikawaambia ukweli.
Mwanaspoti: Ukiachana na winga nafasi gani unapendelea kucheza? Ambundo: Napendelea zaidi kucheza kama mshambuliaji namba 10 ingawa wengi wamezoea kuniona kama winga pekee.
Mwanaspoti: Isingekuwa soka ungekuwa nani au ungefanya nini? Ambundo: Kwa kweli sijui ningefanya nini maana mpaka sasa hivi sina kitu au kazi napenda kuifanya zaidi ya soka.
Mwanaspoti: Winga gani Ligi Kuu unamkubali? Ambundo: George Makang’a wa KMC
Mwanaspoti: Kwa nini Makang’a? Ambundo: Ni winga ambaye napenda kumfuatilia na ninamwona ana kitu kikubwa kuliko watu wanavyodhania au kumwona.