Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alvarez avunja ukimya, kufanya maamuzi mazito

Julian Alvarez 25 At 12.jpeg Mshambuliaji wa Manchester City Julian Alvarez

Wed, 31 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mshambuliaji wa Manchester City na timu ya taifa ya Argentina, Julian Alvarez ambaye amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali katika siku za hivi karibuni amesema anataka kufikiria juu ya hatima yake kuelekea msimu ujao baada ya kutoka katika michuano ya Olimpiki huko Ufaransa.

Alvarez ambaye hivi karibuni alikataa kusaini mkataba mpya wa miaka minne aliowekewa mezani na mabosi wa Man City anahusishwa na Atletico Madrid ya Hispania.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 24, msimu uliopita alicheza mechi 54 za michuano yote akafunga mabao 19 na kutoa asisti 13.

Mojawapo kati ya changamoto kubwa ambazo staa huyo amethibitisha kwamba inaweza kumfanya akaondoka Man City ni kutopata nafasi ya kucheza katika mechi kubwa ambapo mara nyingi kocha Pep Guardiola amekuwa akimtumia Erling Haaland.

Alvarez mara nyingi amekuwa akicheza mechi ambazo hazionekani kuwa na umuhimu mkubwa Man City na pia amekuwa akipata nafasi katika mechi ambazo Haaland hayupo katika kikosi kutokana na majeraha.

"Sijaacha kufikiria hatima yangu. Msimu uliopita nilikuwa mmoja wa wachezaji waliocheza dakika nyingi kwenye timu, lakini ni kweli kwamba sikuwa nacheza katika mechi muhimu jambo ambalo halipendezi. Nitatenga muda wa kuzingatia uamuzi wangu. Sijaacha kufikiria mambo kwa utulivu. Mara baada ya Michezo ya Olimpiki kumalizika nitakaa na kuangalia mustakabali wa hatima yangu," alisema.

Atletico Madrid inahitaji huduma ya Alvarez kwa ajili ya kuziba pengo la Alvaro Morata ambaye ametimkia AC Milan.

Kwa sasa staa huyo wa zamani wa River Plate yupo jijini Paris akiwa na kikosi cha Argentina akiitumikia timu hiyo katika michuano ya Olimpiki.

Chanzo: Mwanaspoti