Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alonso huu ni mwaka wa kufosi Bundes

Xabi Alonso .jpeg Kocha wa Bayern Liverkusen, Xabi Alonso

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wataweza? Zimebaki mechi 10 Ligi Kuu ya Bundesliga kumalizika huku Bayer Leverkusen ya kocha Xabi Alonso ikijiimarisha kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya mabingwa watetezi Bayern Munich. Ishu ni je, wataweza kushikilia bomba?

Hili ndilo swali linaloulizwa na kila mmoja mashabiki wa soka na hata wachambuzi wa mchezo huo unaopendwa zaidi duniani.

Leverkusen imekuwa katika ubora unaomshangaza kila moja msimu huu, ikifanya mambo makubwa tangu Alonso akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo ambayo ilikuwa katika hatari ya kushuka daraja.

Lakini tangu kiungo huyo wa zamani wa Liverpool na Real Madrid apewe timu, Leverkusen imekuwa inatisha iking’ang’ania kileleni mwa msimamo kwa muda mrefu na sasa inaonekana ina jambo lake. Lakini jambo hilo litategemea uwezo uwezo wa timu hiyo kushikilia bomba hadio mwisho wa msimu. Watakata upepo au huu ndio mwaka wao?

Kama Alonso na jeshi lake wataweza kushikilia bomba na kutwaa ubingwa msimu huu, itakuwa ni mara ya kwanza kubeba katika miaka 120 ya historia ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1904.

Leverkusen haimo katika orodha ya washindi wa ligi hiyo kwa sababu hawajawahi kutwaa taji la Bundesliga. Wamemaliza katika nafasi ya pili mara tano, idadi ambayo ni kubwa zaidi ya klabu yoyote ambayo haijawahi kutwaa ubingwa. Mara yao ya mwisho kumaliza katika nafasi ya pili ilikuwa msimu wa 2010/11. Huu ndio mwaka wa kufosi? Au gundu litaendelea?

Leverkusen juzi iliweka tofauti ya pointi 10 kileleni baada ya kuifunga FC Cologne iliyobakiwa na watu 10 uwanjani.

Hiyo ni baada ya mabingwa mara 11 mfululuzo, Bayern Munich kushikiliwa katika sare ya 2-2 dhidi ya Freiburg Ijumaa iliyopita na kumpa Xabi Alonso nafasi ya kuongeza pengo kubwa la pointi kati ya timu hizo mbili za juu.

Mambo yao yalirahishishwa baada ya Jan Thielmann wa Cologne kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumfanyia madhambi kiungo Granit Xhaka.

Jeremie Frimpong akafunga bao la kuongoza kabla ya Alex Grimaldo kuweka chuma cha pili kwa shuti la chini katika kipindi cha pili.

Leverkusen, ambayo sasa imecheza mechi 34 bila ya kipigo katika michuano yote msimu huu, ina pointi 64 ikifuatiwa na Bayern yenye pointi 54 baada ya kila timu kucheza mechi 24.

Kama alivyoimba msanii wa Bongofleva, Dayoo katika ngoma yake inayotrendi ya ‘Huu Mwaka (Ndio mwaka wa kufosi, mtake msitake, mtaniita bosi)’, inawezekana Alonso akaitwa bosi wa Bundesliga na pia gwiji wa Leverkusen iliyoshindwa kulitwaa taji hilo kwa miaka yao yote 120 tangu klabu ya Leverkusen ilipoanzishwa.

Wakati vita ya kileleni ikiwa hivyo, pale kwenye Top 4 katika kuwania nafasi za kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya bado mchuano ni mkali. VfB Stuttgart iliyo na pointi 50 katika nafasi ya tatu ilishinda 3-2 dhidi ya Wolfsburg na imewaacha mbali kidogo wapinzani wake Borussia Dortmund wenye pointi 44, ambao wanakabwa koo na RB Leipzig wenye pointi 43 katika nafasi ya tano. Pointi hizo ni baada ya Dortmund kuifunga Union Berlin 2-0, huku Leipzig ikiichakaza VfL Bochum 4-1 wikiendi iliyopita.

Kipigo kizito cha wikiendi iliyopita kilikuwa ni cha Augsburg iliyoipondaponda SV Darmstadt kwa mabao 6-0 na kuishindilia mkiani mwa ligi ikibakiwa na pointi 13.

Mbali na Darmstadt, mapambano ya kujaribu kuepuka kushuka daraja yanaihusisha pia Mainz yenye pointi 16 ikiwa katika nafasi ya 17 na FC Cologne iliyo na pointi 17 katika nafasi ya 16.

Chanzo: Mwanaspoti