Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alonso ana jambo lake Bundesliga

Xabi Alonso .jpeg Kocha wa Bayern Liverkusen, Xabi Alonso

Sat, 17 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Vinara wa Bundesliga, Bayer Leverkusen iko ugenini Heidenheim leo Jumamosi ikisaka kudumisha tofauti ya pointi 5 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Ujerumani.

Chama hilo la kocha Xabi Alonso liliandikisha moja ya matokeo maarufu zaidi katika historia ya Bundesliga lilipowachakaza mabingwa watetezi Bayern Munich wikiendi iliyopita, na kuwashawishi wengi kwamba wanaweza kubeba ndoo ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani msimu huu.

Baada ya kutawala soka la Ujerumani kwa miaka 12, matumaini ya Bayern ya kuendeleza ubabe yalipata pigo kubwa baada ya kichapo cha wikiendi iliyopita kutoka kwa Leverkusen, ambao walitembeza boli jingi na kupata ushindi waliostahili wa 3-0.

Licha ya safu ya ushambuliaji ya Leverkusen kuundwa na wakali kibao, walikuwa ni mabeki wao watatu waliofunga mabao yaliyoizamisha Bayern, huku Josip Stanisic akiitungua klabu-mama yake, na pacha ya ma-wing-back wa hatari, Alex Grimaldo na Jeremie Frimpong, ikaongeza mabao mengine katika kipindi cha pili.

Die Werkself bado wanaendelea kuwa timu pekee katika ligi tano kubwa za Ulaya ambao hawajapoteza mchezo katika michuano yoyote msimu huu, na wakiboresha mwendo huo kufikia 32 leo, wataifikia rekodi ya muda wote ya Ujerumani inayoshikiliwa na Bayern ya kutopoteza mchezo kuanzia mwanzo wa msimu.

Wakiwa wameshinda mechi tano kati ya sita tangu mwaka 2024 uanze, Leverkusen hawaonyeshi dalili za kutoifuata rekodi hiyo, kama ilivyokuwa katika ushindi wa Jumamosi iliyopita ambao uliwafanya waweke pengo kubwa la tofauti ya mabao, pamoja na pointi.

Baada ya pia Bayern kupoteza mchezo wa Lazio katika Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki, Leverkusen watakuwa ‘wanali-zoom’ tu anguko la miamba hiyo, jambo ambalo litachangia kuwaongeza mzuka kwenye mechi ya leo. Alonso anajua kwamba hawezi kuwachukulia poa Heidenheim, akijua kwamba timu yake ya Leverkusen ndio pekee ambayo haijapoteza mchezo kwenye Bundesliga.

Ikishinda mechi nne na kutoka sare nne katika mechi nane zilizopita, timu iliyopanda daraja ya Heidenheim imejiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja ikitinga ndani ya Top 10 ya msimamo. Mwanzoni mwa Desemba, Heidenheim ilikuwa chini katika nafasi ya 14, lakini pointi 15 hizo ilizozoa kati ya 24 ilizowania, zimeiinua kwa pointi 11 juu ya mstari wa kushuka daraja.

Ushindi wa 2-1 dhidi ya Werder Bremen wikiendi iliyopita ilikuwa ya kwanza ndani ya mwaka 2024 baada ya mfululizo was are na kudumisha matumaini madogo yaliyopo ya kufuzu kucheza michuano ya Ulaya.

Licha ya kupasuka 4-1 kwenye Uwanja wa BayArena mwanzoni mwa msimu huu, Heidenheim ilipata ushindi maarufu dhidi ya Leverkusen katika mechi ya Kombe la DFB Pokal mwaka 2019, waliwalaza 2-1 kwenye Uwanja wa Voith Arena, wanaokutana tena leo.

Heidenheim ya kocha Frank Schmidt huenda ikamkaribisha kikosini Denis Thomalla ambaye ametokea kuwa mgonjwa baada ya kukosa mechi waliyoshinda ugenini dhidi ya Bremen wiki iliyopita. Elidon Qenaj na Marnon Busch wote bado hawako fiti tayari kurudi, wakati Thomas Keller hatacheza tena msimu huu kutokana na majeraja ya goti.

Leverkusen itawakosa wachezaji muhimu ambao wamechangia mafanikio ya timu hiyo msimu huu, kwani Exequiel Palacios na Victor Boniface wote wako nje ya uwanja kwa majeraha.

Odilon Kossounou anaweza kurejea baada ya kutua akitokea kutwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 akiwa na timu yake ya taifa ya Ivory Coast wiki iliyopita, lakini kwa kuwa safu ya ulinzi iko katika ubora wa juu, anaweza asirejeshe namba yake kikosini haraka.

Kikosi kinachotarajiwa kuanza cha Heidenheim:

Muller; Traore, Mainka, Gimber, Fohrenbach; Maloney, Schoppner, Pieringer; Dinkci, Kleindienst, Beste

Kikosi kinachotarajiwa kuanza cha Bayer Leverkusen:

Hradecky; Tapsoba, Tah, Hincapie; Frimpong, Andrich, Xhaka, Grimaldo; Hofmann, Borja Iglesias, Wirtz

Chanzo: Mwanaspoti