Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ally, kocha kijana anayetembelea nyota ya Marsh

Ahmad Ally Prisons Ally, kocha kijana anayetembelea nyota ya Marsh

Thu, 14 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Huenda akawa ndiye kocha mkuu mwenye umri mdogo kwenye Ligi Kuu Bara, lakini Ahmad Ally wa Tanzania Prisons ameendelea kuonyesha uwezo mkubwa kazini.

Ally alitambulishwa Prisons mapema Desemba, mwaka jana akiziba nafasi ya Fred Felix ‘Minziro’ aliyesitishiwa mkataba kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Tangu akabidhiwe mikoba hiyo kocha huyo ameiongoza katika michezo 10 ukiwamo mmoja wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo ameshinda sita, sare mbili na kupoteza miwili.

Katika mechi alizopoteza ni dhidi ya TRA ya First League kwenye kombe la ASFC walipoondoshwa mapema hatua za awali kwa penlati 5-4 baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu ya bila kufungana.

Pia timu hiyo ilipoteza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga kwa mabao 2-1, huku sare zikiwa ni dhidi ya Ihefu na Azam na ikishinda mbele ya Mashujaa, Dodoma Jiji, Singida Fountain Gate, Tabora United na Simba.

ALIANZIA WAPI?

Kocha huyu alianza kazi ya ukocha katika kituo cha michezo ambacho mmiliki wake ni kocha wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Sylivester Marsh cha jijini Mwanza.

Kwa takribani miaka mitano aliishi kituoni hapo akiwa karibu na hayati Marsh ambaye alisifika kwa upole, weledi na misimamo kazini akiamini katika taaluma.

Kituo hicho kilichopo Mtaa ya Soko la Mirongo jijini Mwanza kiliwahi kutoa timu ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Marsh Queens na ile ya wavulana inayoshiriki Ligi ya Mkoa wa Mwanza.

Kocha Ally aliachiwa kituo hicho ambacho kilitoa vijana wengi wakiwamo Ally Msengi ambaye alicheza soka la kulipwa Afrika Kusini kabla ya dirisha dogo msimu huu kutua Prisons.

Pia yupo beki wa zamani wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na Mbao FC, Boniface Maganga anayekipiga KMC kwa sasa ambao wamepikwa na Ally katika kituo hicho ambacho kinaitwa Marsh Athletes.

Baadaye Ally alitua Mbao akipoitwa na aliyekuwa kocha mkuu kipindi hicho, Ettiene Ndayiragije, raia wa Burundi alipokabidhiwa timu hiyo baada ya kupanda Ligi Kuu msimu wa 2016/17.

Ally alikuwa msaidizi wa Ettiene hadi kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ikiwa ni msimu wao wa kwanza katia Ligi Kuu, licha ya kupoteza mechi kwa mabao 2-1 dhidi ya Simba.

Baada ya kudumu Mbao, kocha huyo mzaliwa wa Tabora alitimka na Ettiene kujiunga na KMC walipong’ara kumaliza nafasi ya nne na kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, baadaye Ettiene alipata ulaji Azam na kumuacha Ally pale KMC akiwa na mwenzake Faraji Muya ambaye kwa sasa wapo wote Prisons akihudumu nafasi ya kocha wa viungo.

Ally aliendeleza kazi yake KMC kabla ya kuletewa kocha raia wa Rwanda, Hitimana Thiery aliyekuwa amezifundisha timu za Biashara United na kuipandisha Ligi Kuu timu ya Namungo.

Hata hivyo, baada ya KMC kutofanya vizuri, msimu uliopita uongozi ulipitisha fagio kwenye benchi la ufundi na kuwasomba Ally pamoja na mwenzake Muya na kuibukia Prisons.

HISTORIA YAKE

Ally alizaliwa mkoani Tabora na katika harakati zake aliibukia mikononi mwa kocha hayati Marsh aliyempokea katika medani za mpira akiwa mdogo jijini Mwanza.

Kocha huyo hajacheza sana mpira katika levo za ushindani badala yake aliishia ngazi ya mkoa, alikokuwa akicheza nafasi ya kipa katika timu ya Marsh kwenye Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Nyamagana hadi Mkoa wa Mwanza.

Maisha yake ya mpira alikuwa sambamba na Marsh ambaye mbinu zote hadi timu ya Taifa muda mwingine alikuwa akimkokota kubeba vifaa ikiwa ni njia ya kumuandaa kwa maisha ya baadaye ya ukocha.

Hata baada ya kifo cha kocha Marsh, Machi 14, 2015, Ally hakuondoka haraka kituoni hapo akiendelea kufundisha vijana wengine waliokuwa wamebaki wakiwamo wanawake hadi kucheza Ligi Kuu kabla ya kushuka daraja na kupotea.

HESHIMA PRISONS

Kutua kwa kocha huyo kuziba nafasi ya Minziro, wengi walishika vichwa wakiamini majukumu hayo ni makubwa na huenda asifanye chochote kutokana na matokeo iliyokuwa nayo timu.

Ally aliikuta Prisons nafasi ya 13 kwa pointi saba lakini kwa sasa wapo nafasi ya tano kwa alama 27 huku akikusanya alama nne kwa vigogo Simba na Azam FC.

Katika michezo 10 aliyoongoza kocha huyo amepoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga walipolala 2-1 huku mechi moja tu na Ihefu ndio iliisha kwa suluhu ya bila kufungana, huku nyingine timu ikipata bao.

Rekodi na heshima aliyoweka ni kumtibulia Kocha Mkuu wa Simba, Abdelakh Benchikha ambaye tangu atue nchini kuchukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alikuwa hajapoteza mechi yoyote Ligi Kuu.

Simba iliyokuwa imetoka kushinda mabao 6-0 dhidi ya Jwanneng Galaxy katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi ligi ya mabingwa Afrika, haikuamini kilichowakuta kwa Maafande hao waliowanyamazisha.

ANALESENI KUBWA

Akizungumza kwa nyakati tofauti, kocha huyo mwenye leseni ya Diploma A ya CAF anasema siri ya mafanikio ni ushirikiano alionao ndani na nje ya uwanja na kila mmoja kutimiza wajibu wake.

Anasema baada ya kuikuta timu katika mazingira magumu, aliamua kukaa na wachezaji kuwakumbusha wajibu wao na kulinda taswila ya timu na wao wenyewe.

“Uongozi unayo sapoti kubwa kwangu, wachezaji wamenikubali tunaongea lugha moja, kabla, wakati na baada ya mechi lazima tujadiliane namna ya kutoka kuhakikisha tunapata ushindi,” anasema Ally.

Kuhusu mechi dhidi ya Simba, kocha huyo anasema aliwasoma kabla kwa takribani siku tatu tangu walipomaliza mchezo wao dhidi ya Azam na kubaini wapi pakuwakamata.

“Niliwaangalia muda mrefu tangu tulipomaliza mchezo na Azam nikagundua eneo la beki yao si imara sana nikaingia na mbinu za kushambulia kwa kushtukiza na kufanikiwa kushinda.

“Malengo yetu ni kushinda kila mechi, nikisema kumaliza nafasi nne yote ni mipango ya Mungu, kimsingi ni kuendelea kuwaandaa wachezaji kuendeleza ushindi,” anasema kocha huyo.

Chanzo: Mwanaspoti