Pazia la Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) msimu wa mwaka 2023/2024 linafunguliwa kesho katika viwanja vitano tofauti nchini, huku Uwanja wa Nyamagana jijini hapa vita ikiwa ni kati ya wenyeji Alliance Girls dhidi ya majirani zao, Geita Gold Queens.
Alliance Girls ambayo inashiriki ligi hiyo kwa msimu wa sita mfululizo itamenyana na Geita Gold ambayo ni msimu wake wa kwanza baada ya kupanda daraja msimu huu, mchezo huo utapigwa kuanzia saa 10 jioni.
Mbali na vikosi, vita nyingine kwenye mchezo huo itakuwa kwenye mabenchi ya ufundi na Kocha wa Alliance, Ezekiel Chobanka atakuwa anashindana mbinu na Kocha wa Geita Gold, Sultan Juma aliyekuwa msaidizi wake kwa misimu zaidi ya mitatu Alliance Girls.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Alliance, Chobanka amesema kwa maandalizi aliyoyafanya, uzoefu alionao kwenye ligi hiyo na namna alivyowaandaa wachezaji wake pamoja na faida ya kucheza uwanja wa nyumbani, anaamini atapata ushindi.
“Kiuhalisia maandalizi sijaanza leo, nilianza miezi sita iliyopita nikijiandaa na msimu mzima wa ligi, kwa hiyo nafahamu mechi itakuwa ngumu, nawaheshimu Geita na benchi lao la ufundi, mwalimu wao alikuwa msaidizi wangu msimu uliopita, kimsingi itakuwa mechi ya mvutano mkubwa.”
“Kitakachokuja kuamua ni mbinu na vijana waweze kuzitekeleza kwa usahihi, basi yeyote anaweza akashinda, lakini nina imani tutashinda kwa sababu tuko nyumbani na vijana wangu namna nilivyowaandaa,” amesema Chobanka.
Kocha wa Geita Gold Queens, Sultan Juma amesema licha ya ugeni na kukosa uzoefu kwenye mashindano hayo anaamini wataanza vizuri msimu wa Ligi ya Wanawake kwani usajili wao umechanganya wachezaji wachache wenye uzoefu na vijana wapya, huku akiamini utakuwa na mvuto kiufundi kutokana na makocha wote wawili kufahamiana kimbinu.
Hata hivyo, akizungumzia ushiriki wao kwenye mashindano ya African School Championship, Ukanda wa Afrika Mashariki yaliyomalizika hivi karibuni Kenya, huku kikosi chake kikishika nafasi ya tatu, Chobanka amesema wamepata uzoefu mkubwa na vijana wake wameiva kucheza mechi kubwa jambo litakalowasaidia kwenye Ligi Kuu.
“Tulienda kushindana tulicheza mechi nne tukashinda mbili, sare moja na kupoteza moja na kuwa washindi wa tatu huku Uganda wakiwa mabingwa, tumejifunza timu zinavyocheza kimkakati kwa hiyo imewajengea uwezo wa kupambana hata wakikutana na timu ngumu wanaweza kucheza, naona kuna kuimarika kwa vijana wangu,” amesema Chobanka.