Imeelezwa tayari Azam FC, imekamilisha usajili wa kipa Mohamed Mustafa (27), kutoka Al-Merrikh ya Sudan na huenda akaanza kuonekana kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi, huko Zanzibar.
Yanga iliiondoa Al Merrikh ya Sudan raundi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0, huku Clement Mzize aliandika rekodi ya kumfunga nje ndani kipa Mustafa na kuivusha timu hiyo hatua ya makundi.
Mwanaspoti limepata taarifa za usajili wa kipa huyo, kutoka kwa mmoja wa kiongozi wa Azam, aliyesema walifikia uamuzi huo baada ya makipa wao kusumbuliwa na majeraha yatakayowaweka nje kwa muda mrefu.
Wakati makipa Ali Ahamada na Abdullah Iddrisu wakiendelea na matibabu, Azam wanaamini kipa huyo atakuwa msaada kwenye mechi za Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), na mashindano ya Mapinduzi.
"Makipa wetu wamepata changamoto, hivyo hatukuwa na namna nyingine zaidi ya kusajili kipa mpya," kilisema chanzo.
Imeelezwa kipa huyo anaweza kuonekana langoni kesho wakati Azam inafungua dimba dhidi ya Mlandege FC, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Amaan.