Unazikumbuka zile 5-0 ilizopewa Simba kutoka kwa AS Vita katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019?
Katika mchezo huo uliopigwa Kinshasa kuna kiungo mkabaji aliyewapoteza kabisa kina Jonas Mkude na James Kotei waliokuwa wakiichezea Simba kipindi hicho, jina lake Nelson Omba Munganga. Sasa jamaa huyo ameibukia Tabora United iliyomsajili kutoka DC Motema Pembe ya DR Congo aliyokuwa akiichezea baada ya kuondoka Vita na juzi alitambulishwa rasmi tayari kuitumikia timu hiyo.
Munganga anayefahamika zaidi kwa jina la ‘The Beast’ aliyecheza na nyota waliowahi kuja kutamba nchini kupitia Yanga kama Mukoko Tonombe, Yannick Bangala, Fiston Mayele, Jesus Moloko na Djuma Shaban ni kati ya ingizo jipya la Tabora inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja.
Uongozi wa klabu hiyo ulitoa taarifa mapema kwamba wamefikia makubaliano na klabu ya DC Motema Pembe ya kumsajili kiungo huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Munganga kabla ya kwenda DC Motema Pembe aliitumikia AS Vita Club akiwa nahodha wa kikosi hicho na kufanikiwa kushinda tuzo ya kiungo bora wa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa 2018/2019, lakini pia alishawahi kuitumikia Magreb Fes iliyopo Ligi Kuu ya Morocco na timu ya taifa ya DR Congo kwa vipindi tofauti.
Huo unaweza kuwa usajili mkubwa zaidi kwa Tabora, kwani licha ya kufanya maingizo mapya, lakini aina ya uchezaji wake unaweza kuinufaisha katika mambo mengi kutokana na uzoefu alionao wa kucheza mechi za kimataifa na ni pendekezo la kocha Goran Kapunovic aliyeamua kusalia kikosini ili kupiga kazi. Awali ilielezwa alikuwa mbioni kuondoka, lakini Goran alisema ameamua kusalia katika timu hiyo kutokana na malengo mazito waliyonayo, kwani kwa sasa Tabora ipo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 15 kutokana na mechi 13.