Kocha wa Morocco, Walid Regragui alifungiwa mechi mbili katika Fainali za Mataifa ya Afrika na kufutiwa adhabu hiyo Ijumaa Januari 26 na atasimama kwenye nafasi yake ya kocha kwenye mechi ya hatua ya 16 bora dhidi ya Afrika Kusini.
Hivi karibuni, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche alidai Morocco ina nguvu kubwa Caf hadi inajipangia waamuzi wa kuchezesha mechi zao ili wawapendelee.
Regragui, ambaye aliipeleka Morocco katika nusu-fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022, alisimamishwa kutokana na kuzozana na nahodha wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Chancel Mbemba wakati wa mchezo wa makundi uliopigwa Januari 21 katika Uwanja wa De San Pédro.
"Kufutiwa huku kunahusu pia faini iliyotolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa kocha Regragui," ilisema taarifa ya Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF).
"Maamuzi ya Kamati ya rufaa yanakuja baada ya hoja za utetezi zilizowasilishwa na FRMF."
Regragui alifungiwa mechi nne lakini mbili zilikuwa kifungo huru.
Kocha huyo alitumikia mechi moja dhidi ya Zambia Januari 24 na nafasi yake ikachukuliwa na kocha msaidizi Rachid Benmahmoud.
Morocco itakutana na Afrika Kusini katika hatua ya 16 bora Jumanne ijayo mjini San Pedro.