Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyekuwa dada wa kazi apasua kidato cha sita

Mariam Mchiwa Mariam Mchiwa wakati akiwa shule ya Wasichana Songea

Sat, 13 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

“Ndoto yangu inaenda kutimia ila nimejifunza kwenye maisha heshimu kila mtu, kwa kwa kuwa inawezekana hatima yako imeshikiliwa na mtu usiyemfahamu kabisa”.

Haya ni maneno ya Mariam Mchiwa mhitimu wa kidato cha sita katika sekondari ya wasichana Songea akiwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa leo na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Mariam ambaye alisoma mchepuo wa sayansi akichukua masomo ya Kemia, Biologia na Jiografia amefaulu kwa kupata daraja la pili lenye alama 11.

Binti huyu mwenyeji wa mkoa wa Dodoma ambaye licha ya kufaulu vizuri mtihani wake wa kuhitimu kidato cha nne kwa kupata daraja la kwanza, familia yake haikuwa na uwezo hivyo hakuwa na uhakika wa kuendelea na masomo, ndipo alipofikia uamuzi wa kufunga safari hadi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kazi za ndani.

Mwaka 2022 ikiwa zimesalia siku chache kabla ya wanafunzi wa kidato cha tano kuanza masomo, gazeti la Mwanachi lilichapa taarifa kuhusu binti huyu na shauku yake ya kupata elimu.

Mfululizo wa habari kumhusu binti huyo ziliwagusa wadau mbalimbali ambao walijitokeza kwa lengo la kumsaidia kabla ya familia ya mbunge wa jimbo la Kongwa Job Ndugai kubeba jukumu hilo.

Hatua hiyo ilimuwezesha kupata mahitaji yote muhimu, kuripoti shuleni na kufanikiwa kuanza masomo na wenzake.

Miaka miwili baadaye binti huyu amehitimu kidato cha sita na amefanya mahojiano na Mwananchi akieleza furaha yake baada ya matokeo kutangazwa na kufanikiwa kupata alama zinazomwezesha kujiunga na chuo kikuu.

“Nina furaha ya ajabu, kwangu ilikuwa kama ndoto siamini naenda chuo kikuu, nitabeba dhamana kubwa kwa ajili ya familia yangu kwa kuwa mimi ndiye wa kwanza kwenye ukoo kufikia ngazi hiyo ya elimu,” amesema Maria.

Akili ya binti huyu kwa sasa ni kupata elimu ya chuo kikuu akiwa na shauku ya kusoma kozi ya chakula na lishe katika Chuo Kikuu cha Dodoma endapo atafanikiwa kuchaguliwa chuoni hapo.

Mariam hakusita kutoa shukrani zake kwa watu waliofanikisha safari yake ya elimu, akieleza namna ambavyo walibeba hatima yake.

Amesema: “Nimepata funzo kubwa kupitia hiki kilichotokea kwangu, hatima yangu ilibebwa na watu baki huenda nisingefika hapa leo bila wao. Nishukuru gazeti la Mwananchi kwa kufikisha kwa umma kile nilichopitia, naamini habari ziko nyingi lakini wakaipa umuhimu taarifa yangu iliyowezesha watu kuona na kuguswa kunisaidia.

“Nina kila sababu ya kuishukuru familia ya mheshimiwa Ndugai kwa upendo na msaada walionipatia, bila kuisahau familia ya mheshimiwa Antony Mtaka hawa wote wamegusa maisha yangu kwa namna tofauti”.

Mbali na wanasiasa hao, Mariam alitoa shukrani zake kwa Agnes Kosamu ambaye alikuwa bosi wake katika nyumba aliyokuja kufanya kazi za ndani jijini Dar es Salaam.

Agnes ndiye aliyeweka wazi kuhusu ufaulu wa Mariam baada ya kumhoji kuhusu ngazi ya elimu aliyosoma ndipo alipobaini alimaliza kidato cha nne na kupata ufaulu mkubwa.

Kwa Mariam haikuwa rahisi kuondoa mawazo yake kutoka kwenye kutafuta pesa hadi kurudi shuleni na kuwa kama wanafunzi wengine, lakini walimu wa shule ya sekondari ya wasichana Songea walilirekebisha hilo ndani ya muda mfupi.

“Ukumbuke nimeripoti shule nikiwa tayari nimeshafanya kazi za ndani, kuondoa mawazo yangu kutoka kwenye kutafuta pesa kuyarudisha shuleni ilikuwa vigumu kidogo lakini walimu wa malezi pale shuleni walinijenga vyema kisaikolojia.

“Walikuwa wana taarifa zangu kwa kuwa tayari zilishatoka gazetini hivyo walikuwa karibu na mimi wakinisihi niyaondoe mawazo hayo na niwekeze akili yangu kwenye masomo”.

Mwalimu wa malezi shule ya sekondari wasichana Songea Neema Benjamin amekiri akisema: “Ni kweli nilimfanya Mariam kama mtoto wangu kwa sababu nilijua tayari kichwani mwake alikuwa na mawazo mengine. Nilijitahidi mara kwa mara kuzungumza naye ili kumuweka sawa kisaikolojia kwa sababu niliona ana uwezo kitaaluma hivyo angeweza kufanya vizuri,”

Naye Mkuu wa shule hiyo, Ester Kulumla amesema furaha yao ni kuona binti huyo anaelekea kutimiza ndoto zake na kutumia fursa hiyo kumtaka kuongeza juhudi zaidi katika ngazi ya elimu ya juu.

Mama wa Mariam, Edina Chabago amesema ni furaha ya aina yake kuona binti yake anapiga hatua kwenye elimu licha ya kutoka kwenye familia duni.

Amesema: “Sina cha kusema zaidi ya kumshukuru Mungu na kuwaombea wote waliofanikisha kwa namna moja hadi nyingine binti yangu kupata elimu. Hatuna cha kuwalipa sisi ni maskini lakini naamini Mungu atawalipa”.

Chanzo: Mwananchi