Straika wa Mashujaa FC, Abiyudi Mtambuku amesema msimu huu umekuwa bora na wa heshima kwake baada ya kupandisha timu kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake ya soka, huku akisema yuko tayari kucheza popote.
Kinda huyo alikuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Maafande hao tangu kuanza msimu akifunga jumla ya mabao 11 yakiwamo mawili yaliyopandisha timu hiyo ligi kuu kupitia play off.
Nyota huyo aliyewahi kucheza Kurugenzi FC ya wilayani Maswa mkoani Simiyu alikuwa tishio kwenye championship na kufanikiwa kuipa heshima Mashujaa kupanda daraja na kukata kiu ya mashabiki wa soka mkoani Kigoma waliokosa uhondo huo kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Abiyudi alisema hadi sasa tayari simu zimeanza kuita kutokana na kiwango alichoonesha haswa kwenye mechi mbili za mwisho za play off dhidi ya Mbeya City.
Alisema kazi yake ni soka, hivyo yupo tayari kucheza popote kimsingi maslahi yawe ni yenye kushawishi lakini uhakika wa namba ili kuendeleza kipaji chake huku akichekelea rekodi ya kupandisha timu.
“Naweza kusema ulikuwa msimu wangu bora na wa thamani kubwa, sikuwahi kupandisha timu japokuwa ni kitu kilikuwa kwenye ndoto zangu, nashukuru kuna timu nimeanza kupokea simu zao wakinihitaji na nipo tayari kwenda popote,” alisema Mtambuku.
Aliongeza kuwa siri ya mafanikio ni kujituma na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi lakini nidhamu ya kazi ndio ilimng’arisha hadi kumalizika kwa msimu.
“Mashujaa bado sijazungumza nao japokuwa nilisikia wananitaka nibaki kwa ajili ya msimu ujao, hivyo nasubiri kusikia kauli yao na namna walivyojipanga binafsi sina tatizo kama tukikubaliana,” alisema nyota huyo.