Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyeitibulia Simba katua

Okejepha Simba.jpeg Augustine Okajepha

Mon, 8 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba inaendelea kutambulisha mastaa ambapo jana ilikuwa ni zamu ya kiungo Mnigeria Augustine Okajepha akiwa mchezaji wa saba mpya, saa chache baada ya kuliweka hadharani benchi jipya la ufundi lenye sura mpya tano akiwamo kocha wa makipa aliyewahi kuwatibulia Wekundu katika michuano ya CAF.

Kocha huyo anayeshtua ni Wayne Sandilands aliyetua nchini kuwanoa kipa Ayoub Lakred, Aishi Manula na Ally Salim akiwa ana miaka miwili tu tangu alipostaafu kucheza soka la ushindani akiichezea Orlando Pirates ya Afrika Kusini, nchi iliyoleta sura tano mpya za benchi hilo jipya.

Benchi hilo jipya litakuwa chini ya kocha Fadlu Davids atakayesaidiwa na Darian Wilken  wakati  Sandilands atasimamia makipa, ilihali kocha wa viungo ni Riedoh Berdien na mtathimini wa video ni Mueez Kajee.

Katika benchi hilo ni kwamba kuna sura tatu ambazo zimewahi kuitibulia Simba Aprili 24, 2022 ikishindwa kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kazi hiyo ilifanywa na Davids mwenyewe akisaidiana na Wilken pamoja na Sandilands wote wakati huo wakiwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Iko hivi. Seti hiyo anakosekana kocha mmoja tu, Mandla Ncikazi ambaye hachelewi kukinukisha kutokana na kusema hovyo, lakini wawili waliosimamia shoo hiyo ya kibabe wametua Msimbazi.

Tuanze na Sandilands ambaye kazi yake kubwa ndio iliwahi kuitibulia Simba baada ya kufanya kitu kikubwa kwa kuwasoma wapiga penalti wa Wekundu hao na kumpa ujuzi kipa wa Orlano wakati huo, Mghana Richard Ofori.

Orlando baada ya kutoshana na Simba sare mbili katika mechi zao mbili, kila mmoja akishinda nyumbani kwa bao 1-0, matuta ndio yaliamua nani anakwenda nusu fainali.

Kocha Ncikazi amesema kuwa wakati wanajiandaa kwenda kupigiana penalti ambako hawakutaka kufika huko na Simba, walimgeukia Sandilands ambaye wakati huo alikuwa na mwaka mmoja tu tangu atoke kuhitimu mafunzo ya ukocha wa makipa kwa ngazi ya juu.

Ncikazi alisema wakati wakijiuliza watatoboaje hatua hiyo wakijua Simba ni hatari kwa matuta, Sandilands aliwahakikishia kuwa Ofori anajua kitu cha kufanya na anawajua mastaa wote waliokuwa uwanjani kipindi cha pili watakaopiga matuta kwa Wekundu hao.

“Tulilazimika kumsikiliza yeye unajua kwanza na yeye (Sandilands) alikuwa anajua sana kucheza penalti wakati anacheza. Alipotuambia Ofori yuko sawa tuliamuamini na kweli tukavuka kwa kazi nzuri ya kipa wetu,” alisema Ncikazi.

“Huyo ni kocha mzuri wa makipa wa kisasa anapenda kutumia mbinu za mazoezi ya kisasa kufundisha makipa. Nadhani hilo benchi zima kuanzia Fadlu litafanya makubwa hapo. Simba imepata watu wa maana sana ni wao tu sasa kuwapa muda waifanye kazi kwa ufanisi.”

Katika hatua hiyo ya penalti, Ofori alicheza penalti ya kwanza ya aliyekuwa kiungo wa Simba, Jonas Mkude aliyepo Yanga kwa sasa, huku ile ya Henock Inonga ikigonga mwamba kisha kipa huyo kupiga penalti ya mwisho ya ushindi kwa Orlando iliyofanikiwa kuing’oa Simba kwa mikwaju 4-3.

Kocha huyo aliyezaliwa Agosti 23, 1983 katika mji wa eneo la Benoni uliopo Gauteng ni kipa wa zamani wa SuperSport United, Silver Stars, Platinum Stars, Mamemodi Sundowns na Orlando Pirates klabu ailiyokuwa ya mwisho kwake kuidakika kabla ya kustaafu na kuhamia kwenye ukocha na kwa sasa ana miaka 40, ikiwa ni mitatu pungufu na aliyonayo Fadlu.

Kazi kubwa aliyonayo ni kusaidia kuondoa tatizo la msimu uliopita ambapo Simba iliandika rekodi mbaya ikiruhusu mabao 25 katika Ligi Kuu yakiwamo 7-2 ya Dabi ya Kariakoo, Manula akifungwa matano katika kipigo cha 5-1 na Ayoub kupigwa mawili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live