Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliyefariki ajali ya Kalaba azikwa, familia yamkana mume

Klaba Ajali Aliyefariki ajali ya Kalaba azikwa, familia yamkana mume

Tue, 23 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wanafamilia na marafiki wa Charlene Mumba Kabaso, aliyefariki katika ajali iliyotokea Aprili 13, 2024 eneo la Kafue nchini Zambia wamejumuika kutoa heshima za mwisho na kumpumzisha kwenye makazi yake ya milele, huku ikibainishwa kwamba hakuwa mke wa Boyd Mkandawire kama ilivyoelezwa awali.

Charlene alifariki dunia Aprili 13, mwaka huu katika ajali ya gari aina ya Mercedes Benz ambapo alikuwa dereva lilipogongana na roli la mafuta.

Katika ajali hiyo alikuwa na kiungo wa zamani wa TP Mazembe na Timu ya Taifa ya Zambia, Rainford Kalaba ambaye aliwahishwa hospitali kutibiwa na sasa anaendelea vizuri.

Ibada ya kuaga mwili wa marehemu ilifanyika Alhamisi, Aprili 18, mwaka huu katika Kanisa la Victory Bible lililopo Lusaka kisha kuzikwa katika makaburi ya Leopards Hill Park mjini humo.

FAMILIA YAMKANA MUME Baada ya ajali kutokea mitandao mingi ya kijamii iliripoti kwamba Charlene ni mke wa mwanasoka wa zamani wa Zambia, Boyd Mkandawire ambaye ni rafiki wa Kalaba.

Hata hivyo, katika risala ya marehemu ilibainika kwamba wawili hao hawakuwa wanandoa zaidi ya kuzaa watoto wawili pekee kwani hakuna sehemu iliyobainisha ameacha mume zaidi ya kuelezwa alikuwa na watoto wawili wa kiume.

Dada yake Charlene aitwaye Jennifer Kabaso amefichua hilo kwa kusema: “Mdogo wangu Charlene hakuolewa na Boyd. Hakuna mahari iliyolipwa kwa familia, lakini wamezaa watoto wawili wa kiume. Ndiyo maana katika historia ya maisha yake hamkusikia ameolewa kwa sababu ukweli ni kwamba mdogo wangu Charlene hakuolewa na Boyd Mkandawire.

“Kwa hiyo mbali na uvumi na taarifa za uongo mitandaoni, ndugu yangu hakuolewa wala hakupewa talaka na Boyd. Ni kweli waliwahi kupendana na kupata watoto, lakini hawakuwahi kuoana hata ndoa ya kimila.”

MKANDAWIRE AVUNJA UKIMYA Kwa upande wake, Mkandawire amejibu ishu hiyo akisema: "Tulioana mw

aka 2014 wakati yeye (Charlene) akiwa bado anasoma Shule ya Araka. Nimelipa mahari kwa mama yake kisha tukaanza kuishi pamoja.

"Hatukuwahi kuachana na mke wangu. Sababu za kwenda kuishi Chilenje ni kutokana na kuwa karibu na hoteli anayofanyia kazi."

Mkandawire amesema wakati Charlene akiwa kwa mama yake walikuwa wakiwasiliana vizuri na wala hawakuwa na matatizo.

"Msiba ulipotokea nilikwenda nyumbani kwao na kukaa siku mbili, lakini sikupewa heshima ninayostahili. Familia iliniambia nikae pembeni," alisema nyota huyo wa zamani wa Kabwe Warriors.

Ameongeza kuwa alilipa mahari ya Kwacha 12,000 (takriban Sh1.2 milioni) wakati anamuoa Charlene 2014, ikabaki deni la Kwacha 8,000 (Sh799,374) ambayo aliilipa baada ya mazishi kwani jumla alitakiwa kulipa Kwacha 20,000 (Sh1,998,434).

KALABA AAMKA Wakati Charlene akizikwa, taarifa kutoka University Teaching Hospital alikolazwa Kalaba zinabainisha nyota huyo afya yake inazidi kuimarika.

Hivi karibuni picha zilisambaa zikimuonyesha akiwa ameamka kutoka kitandani jambo linaloashiria afya yake ipo vizuri tofauti hapo awali.

Kabla ya hapo, taarifa ilitoka kwamba Kalaba ameanza kuzungumza na kupata chakula kama kawaida.

ZAMBIA, DR CONGO WAMTAKIA HERI Katika kuonyesha wapo pamoja na Kalaba katika kipindi hiki, TP Mazembe kwenye mchezo wa wikiendi iliyopita wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly waliocheza nyumbani DR Congo walimtakia apone haraka.

Kabla ya kuanza kwa mchezo huo straika wa zamani wa Zambia, Given Singuluma aliingia uwanjani sehemu ya kuchezea akiwa ameshika jezi ya TP Mazembe yenye jina la Kalaba na namba 18 aliyokuwa akiivaa nyota huyo alipokuwa klabuni hapo.

Pia kabla ya kuanza kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Zambia uliochezwa wikiendi kati ya Kabwe Warriors na Green Eagles, wachezaji wa timu hizo walionyesha ujumbe wa kumtakia heri.

Kalaba aliitumikia kwa muda mrefu TP Mazembe na kufanikiwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 sambamba na Kombe la Shirikisho Afrika 2016.

Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Zambia kilichoshinda Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2012 chini ya Kocha Mfaransa Herve Renard.

Chanzo: Mwanaspoti