Beki wa Coastal Union ya Tanga, Lameck Lawi kabla ya kupata tuzo ya mchezaji chipukizi, amemtaja straika wa Yanga, Clement Mzize ndiye alikuwa anamnyima usingizi kwa namna alivyokuwa na msimu mzuri.
Alisema baada ya kuona jina lake limeingizwa kwenye kipengele cha chipukizi bora alipata faraja ya kazi yake kuonekana, ila baada ya kuona yupo na Mzize ni kama alimpa changamoto ya ushindani ya kinyang'anyiro hicho.
Lawi ambaye anaitumikia Coastal Union amekuwa na msimu bora akiwa ni mmoja kati ya wachezaji walioisaidia timu hiyo kubaki kwenye ligi.
"Kiukweli Mzize amefanya kazi kubwa sana ndani ya kikosi cha Yanga kwani siyo rahisi mchezaji anayepanda kutoka kikosi B akapafomu moja kwa moja, lakini nashukuru kila mtu amepata kwa sehemu yake.
"Ni tuzo inayomanisha vitu vingi kwenye maisha yangu, inanipa ari ya kujituma zaidi na kuona inawezekana kiwango changu kuonekana kwa ukubwa zaidi na kuzifikia ndoto zangu za kuwa mchezaji mkubwa na hilo ni deni kuhakikisha msimu ujao nafanya makubwa zaidi.
Alisema ulikuwa msimu wa mafanikio kwake, lakini pia anawashukuru makocha na wachezaji wenzake ambao walifanya kazi kwa pamoja kuisaidia timu ya Coatal Union "Ushirikiano na wachezaji wenzangu umefanya nionekane bora."
Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Joseph Lazaro alisema anajivunia mafanikio aliyoyapata mchezaji wake, akimtaka uwe mwanzo wa kufanya makubwa zaidi kwenye karia yake.