Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alipo Moallin Azam ipo

Moallin Azam DC Alipo Moallin Azam ipo

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Pale KMC benchi la ufundi lipo chini ya kocha Mmarekani mwenye asili ya Somalia. Anaitwa Abdi Hamid Moallin. Kocha huyo alitua nchini kwa mara ya kwanza Januari 2022 akiwa kama kocha wa timu za vijana za Azam FC, lakini baadaye alipewa timu kubwa kabla ya kuondolewa. Alikaa Azam kwa miaka miwili na na miezi mitano akitenda majukumu tofauti ya kiufundi.

Kabla ya kutua Azam aliwahi kuzifundisha Horseed SC ya Somalia, timu ya taifa ya Somalia na pia alifanya kazi na Columbus Crew SC ya Marekani kama kocha, skauti na mtathimini michezo ‘video analyst’ katika nyakati tofauti.

Huo ni wasifu wake kwa ufupi. Kwa sasa yupo KMC. Ndiye kocha mkuu na amefanikiwa kuifanya timu hiyo kucheza soka safi na la ushindani ikiwa ‘Top Four’ kwenye msimamo. Ipo nafasi ya nne na alama 21 baada ya mechi 14.

Moallin kwa kiasi kikubwa ameibadili KMC. Kuanzia kwa wachezaji na namna wanavyocheza ndani ya uwanja.

Tangu amefika kikosini hapo amesajili wachezaji wasiopungua 10, lakini wengi wao ni wale aliofanya nao kazi akiwa Azam FC. Na hiyo haijaishia kwa wachezaji pekee, lakini hata kwa baadhi ya watendaji wa benchi la ufundi. Ni kama amehama na washikaji zake waliopiga mzigo pale kwa matajiri Azam FC.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea majina tisa ya ‘watu kazi’ ambao Moallin alifanya nao kazi Azam na sasa amewavuta KMC wanaendelea kupiga mzigo. Hii ndio ile Roma na Moni Centrozone waliimba ‘Usimsahau Mchizi’. Shuka nayo!

JOHN MATAMBALA ‘KANTE’

Huyu ni kocha msaidizi wa sasa pale KMC. John ni zao la Azam na historia yake ya maisha ya soka inafurahisha kwani kwa mara ya kwanza alienda pale kama fundi msaidizi wakati wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Uwanja wa Azam Complex mwaka 2010 na baada ya hapo wadosi wa Azam wakamfungulia maisha na sasa ni kocha. Stori yake tutakupa siku nyingine.

Wakati Moallin anatua Azam alimkuta John akiwa kocha tayari. Wakaanza kufanya kazi kwa pamoja kuanzia timu za vijana hata ile kubwa. Huenda kuna kitu Moallin alikiona kwa John kwani alivyorejea Dar es Salaam kuinoa KMC aliwaambia viongozi wa timu hiyo ya Kinondoni wamletee John awe msaidizi wake na hilo likatimia. Hadi sasa wanafanya kazi kwa pamoja na mambo yanaenda.

WILBOL MASEKE

Huyu ndiye kipa namba moja wa KMC kwa sasa. Maseke ni zao la akademi ya Azam na miongoni mwa wachezaji walioaminiwa mapema na kupandishwa timu kubwa wakiaminiwa kuwa watafanya makubwa muda wao ukifika. Baada ya kuvaa uzi wa timu kubwa mambo yakaanza kumgeukia Maseke ndani ya muda mfupi na kwenda ndivyo sivyo huku nidhamu ikitajwa kuwa tatizo.

Moallin alifanya naye kazi pale Azam na sasa amempa kazi KMC na kumwamini akimfanya kuwa kipa namba moja akililinda lango la Kino Boys.

AWESU AWESU

Ukikiangalia kikosi cha KMC kwa sasa utamuona jamaa mmoja kiungo mwenye rasta kichwani na mkono wa kushoto kuna kitambaa cha unahodha.

Anaitwa Awesu. Ndiye nahodha wa sasa wa KMC lakini kabla ya hapo alipita Azam na kufanya kazi na Moallin kwa nyakati tofauti. Moallin anamkubali sana Awesu na sasa amempa cheo cha unahodha na wanapiga mzigo pamoja KMC.

TEPSIE EVANCE

Baada ya kusota benchi kwa muda mrefu ndani ya kikosi cha Azam tangu alipopandishwa kutoka kademi, Moallin alipopewa timu akaanza kumtumia Tepsi kama winga kwenye mechi.

Tepsi gari liliwaka kipindi cha Moallin pale Azam. Baadaye Mmarekani huyo akaondoka na Tepsi mambo yakambadilikia akarudi benchi.

Wakati Moallin anatua KMC akagundua Tepsi hatumiki mara kwa mara Azam. Akamuomba kwa mkopo, Azam wakamuachia na sasa ni miongoni mwa silaha muhimu sana katika kikosi cha KMC.

TWALIB NURU

Huyu ni beki wa kati anayefanya shuguli zake za sasa pale KMC.

Nuru ni bwana mdogo ambaye ni zao la akademi ya Azam na alianza kupata nafasi kujumuika katika kikosi cha wakubwa pale Azam enzi za Moallin.

Moallin alivyorudi Bongo alikuta Nuru anasota benchi Azam na akipata nafasi ni dakika chache na kuamua kumuomba kwa mkopo na sasa ni miongoni mwa mabeki tengemeo katika timu ya KMC.

ISAH NDALA

Huyu ni kiungo Mnigeria aliyesajiliwa na Azam msimu uliopita akitokea Plateau United ya nchini kwao.

Ndala alicheza Azam lakini muda mwingi kikosini aliupata nyakati ambazo kocha mkuu alikuwa Moallin.

Ni kama walielewana vyema kwani Moallin alivyorejea msimu huu akitua KMC, alimuomba Ndala kwa mkopo na sasa wanafanya kazi pamoja huku akipata muda wa kutosha kucheza katika kikosi hicho cha wana Kinondoni.

EMMANUEL KABEREGE

Staa mwingine wa timu za vijana za Azam ni Emmanuel ‘Emma’. Ukienda viwanja vya vijana wanamkubali sana huyu kijana.

Hata Moallin alimkubali alipomuona na kuona inafaa kufanya naye kazi tangu wote wapo Azam.

Kocha huyo aliporejea KMC alimsajili pia Emma na sasa wapo wote Kino Boys wakipeperusha bendera ya Watoza ushuru.

NYASHA CHALANDULA

Hili jina utakuwa hulijui. Huyu ni Mzimbabwe ambaye taaluma yake ni kocha wa viungo na utimamu wa mwili kwa wachezaji ‘Fitness Coach’.’

Chalandula alitua mwaka 2020 kama kocha wa viungo wa Azam wakati huo akitokea kwenye timu ya taifa ya Zimbabwe na kufanikiwa kufanya kazi na makocha wengi waliopia Azam akiwemo Moallin.

Baadaye Azam ilimpa ‘Thank You’, lakini Moallin ameona isiwe tabu amemrudisha tena Bongo na sasa ni kocha wa viungo KMC.

SHAABAN CHILUNDA

Mshambuliaji huyu wakati msimu unaanza alikuwa Simba lakini sasa utamuona KMC baada ya kutua kikosini kwenye dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu.

Moallin alifanya kazi na Chilunda wakiwa Azam kabla ya wote kuondoka na sasa wamejumuika pamoja KMC. Maelewano mazuri katika kazi baina yao ndiyo yamewaunganisha. Tusubiri tuone Chilunda atafanya nini ndani ya KMC.

Chanzo: Mwanaspoti