Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aliou Cissé afunga mjadala wa Sadio Mane

Aliou Cisse Aliou Cissé afunga mjadala wa Sadio Mane

Mon, 21 Nov 2022 Chanzo: Dar24

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Senegal Aliou Cissé amesema kukosekana kwa Mshambuliaji na Nahodha wa Kikosi chake Sadio Mane kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2022, sio pigo kwake bali ni kwa Dunia nzima.

Mane alipata majeraha ya mguu majuma mawili yaliyopita akiwa katika jukumu la kuitumikia klabu yake FC Bayern Munich ya Ujerumani, siku chache kabla ya kuitwa kwa kikosi cha Senegal kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia.

Cissé amezungumza na Waandishi wa Habari nchini QATAR na kusema, ni kweli Mshambuliaji huyo alikua na umuhimu mkubwa sana kwenye Fainali za Mwaka huu, lakini hana budi kujipanga kwa wachezaji waliopo ili kufanikisha lengo wanalolikusudia.

Amesema Watu wa Senegal wameumizwa na kukosekana kwa Mane, lakini pia ana uhakika Mashabiki wengi Duniani, wameumizwa pia na taarifa za kukosekana kwa Mshambuliaji huyo ambaye alitoa mchango mkubwa wakati wakisaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu 2022.

“Kuumia kwa Sadio Mane haiathiri watu wa Senegal pekee bali ulimwengu wa michezo wote, pengine bara zima, au kila mtu katika soka. Hatupaswi kusahau kwamba tunazungumza juu ya mchezaji bora wa pili duniani”

“Mane anawakilisha bara la Afrika pamoja na Senegal, Nimepokea simu nyingi kutoka kote ulimwenguni”

“Makocha wote wanajenga timu karibu na mchezaji wao bora, hivyo ndivyo ilivyo kwetu pia. Lakini Tuna timu imara pia, yenye wachezaji wenye uzoefu na vijana walio tayari kukabiliana na changamoto.” alisema kocha huyo.

Nahodha wa Uholanzi Virgil van Dijk nae amehuzunishwa na kukosekana kwa nyota huyo ambaye waliwahi kucheza pamoja Liverpool.

“Tukiwa Kama marafiki, Nina huzuni kwa ajili yake. Ninajua jinsi anavyofanya kazi kwa bidii ili kusaidia Taifa lake, najua anataka kuwa muhimu kwa Senegal,”

“Amekuwa muhimu kwao. Ni wazi atakuwa ni pengo kubwa kwao. Matumaini yetu ni kuwa tunaweza kufaidika kidogo na hilo.” amesema Cissé

Senegal inaanza kulisaka Taji la Dunia leo kwa kupapatuana na Uholanzi majira ya saa moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki, mchezo ambao utaunguruma katika Uwanja wa Al Thumama, mjini Doha.

Mchezo huo wa Kundi A utachezeshwa na Mwamuzi kutoka nchini Brazil Wilton Sampaio.

Chanzo: Dar24