Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alichokisema Conte kwa Spurs ndiyo ugonjwa unaitafuna Azam FC

Azam Official Team Kikosi cha Azam

Thu, 30 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Tottenham Hotspur ya England, Antonio Conte, amekuwa gumzo wiki iliyopita baada ya kuwachana wachezaji na viongozi wa timu yake mbele ya waandishi wa habari na tayari amefukuzwa juzi kuifundisha timu hiyo

Conte alifanya hivyo mara tu baada ya mchezo wa sare ya 3-3 ugenini dhidi ya Southampton, Machi 18, 2023. “Hadi kufikia hapa nimejitajidi sana kuficha hali halisi lakini sasa, siwezi tena.

“Sisi siyo timu ya ushindi kabisa. Tuna kundi la wachezaji 11 ambao wanaingia uwanjani. Nawaona wachezaji wabinafsi, wachezaji ambao hawataki kusaidiana na wasiojituma,” alisema Conte.

Conte alikerwa na kitendo cha timu yake kuruhusu mabao mawili ya dakika za mwisho na kupoteza uongozi wa 3-1.

“Wameyazoea maisha haya hapa Tottenham. Hawachezi kwa ajili ya kushinda kitu cha maana.

“Hawataki kucheza kwenye presha...hawana presha. Kwao ni rahisi tu. Hadithi ya Tottenham ndiyo hii hii kwa miaka takribani 20 sasa, kuna mwekezaji lakini hawajawahi kushinda kitu. Kwanini unadhani?”

Mara ya mwisho Tottenham kushinda taji lolote ilikuwa mwaka 2008 waliposhinda Kombe la Carabao. Ukitaka ligi, basi mara ya mwisho ni kabla ya uhuru wa Tanganyika.

Conte anasema tatizo ni kwamba Tottenham hakuna ari ya ushindani.

Watu wameshajikatia tamaa, hakuna anayeamini kwamba klabu yao inaweza kushinda kitu. Hiyo ndiyo hali inayowatafuna Azam FC hapa nyumbani.

Ukiiona Azam FC inacheza huwezi kuona kama wachezaji wanacheza ili kushinda kitu...wanacheza ili mpira uishe, basi.

Hawana ushindani, hawaufurahii mchezo wenyewe...hawana ari. Kwa kifupi hawachezi kwa presha yoyote...kwao kila kitu ni rahisi tu. Hadi Desemba, Azam FC ilikuwa inachuana na Yanga kileleni, wanashushana tu...leo Azam FC yuko juu, kesho Yanga yuko juu.

Lakini kwa kuwa hawawezi kucheza kwenye presha, rigwaride likawashinda, sasa wako nafasi ya nne, alama 18 nyuma ya Yanga, na zinaweza kuongezeka.

Antonio Conte alikuwa anawasema Tottenham Hotspur lakini ujumbe wake umefika hadi Chamazi. Azam FC ikiwa inaongoza hata 3-0, usishangilie hadi mpira uishe...zinaweza zikarudi zote. Azam FC ikifungwa bao dakika ya kwanza, inaweza isirudishe...mechi imeisha hiyo.

Wachezaji wake ni wanyonge sana kichwani, yaani siyo washindani kabisa. Wanafanya makosa ya kizembe yanayowagharimu kufungwa au kukosa mabao. Asilimia kubwa ya mabao ambayo Azam FC inafungwa, au mechi inazopoteza, siyo kwa kuzidiwa mbinu bali makosa binafsi ya wachezaji.

Wachezaji wanapofanya makosa mengi uwanjani maana yake akili zao ziko sehemu nyingine kabisa...haziko uwanjani, haziko kwenye mechi yao.

Ni sawa tu na dereva anayeendesha gari halafu akili zake haziko barabarani, atasababisha ajali tu. Hicho ndicho anachokilalamikia Antonio Conte kutoka kwa wachezaji wake. Anasema wachezaji wanafanya makosa uwanjani halafu lawama zinaenda kwa makocha na wanafukuzwa.

“Kosa la mchezaji uwanjani linahusika kuwa kosa la klabu na kocha anayekuwepo, na ndiyo ilivyo kwa makocha wote waliokuwa hapa. Nimeona makocha ambao Tottenham imeshakuwa nao kwenye benchi. Unaharibu taswira ya kocha kuficha upungufu kila wakati.”

Na hiki ndicho kinachoendelea Azam FC. Tangu timu hiyo ipande daraja kucheza Ligi Kuu mwaka 2008, ni msimu mmoja tu wa 2011/12, ndipo kocha (Stewart Hall) alianza msimu na kuumaliza. Lakini hakuna kocha mwingine yeyote katika wakati wowote ambaye alianza msimu wake na akaumaliza akiwa kwenye benchi la ufundi la Azam FC.

Haiwezekani kuwa mara zote hizo tatizo ni kocha, hapana...ni wachezaji. Hawajitambui, hawajui kucheza kwenye presha. Na hii ni kitu ambacho wachezaji wanarithishana. Anaweza akaja mchezaji mpya na ari yake ya kushinda lakini akiwakuta waliopo wala hawafikirii kushinda, naye anapoa. Ndiyo unasikia Dube anamaliza msimu ana bao moja.

Yule Dube aliyekuja mwaka 2020 ndiyo wa kumaliza msimu mzima na bao moja kweli? Huwezi amini, msimu wa 2021/22 Dube alifunga bao moja tu katika mechi zaidi ya 18. Viongozi wa Azam FC wanatakiwa kuwa wabunifu kweli kweli kwenye hilo ili kubadilisha akili za mitazamo ya wachezaji wao. Bila hivyo watakuwa kama Tottenham Hotspur, kukaa miaka zaidi ya 15 bila hata kikombe cha kahawa!

Chanzo: Mwanaspoti