Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Alexander-Arnold anukia Real Madrid

Trent Alexander Arnold Real Madrid Trent Alexander-Arnold

Thu, 18 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa kulia wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold, yupo katika hatua nzuri ya kujiunga na Real Madrid katika dirisha hili la usajili linaloendelea Ulaya akiwa amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake kwa Majogoo wa Anfield.

Real Madrid imekuwa ikihusishwa na staa huyo kwa muda mrefu na mara kadhaa iliripotiwa kutuma wawakilishi kwenda Liverpool kwa ajili ya kumtazama katika mechi alizocheza.

Trent ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Liverpool na taarifa za kuondoka kwake zimezidi kupamba moto hivi karibuni baada ya kocha Jurgen Klopp kuachana na timu hiyo mwisho wa msimu uliopita.

Wababe wa Madrid wamekuwa wakitafuta beki wa kulia kwa muda na mbali ya Trent, waliwahi kuhusishwa na Reece James, lakini changamoto kubwa ilionekana kuwa ni mkataba wake na majeraha ya mara kwa mara ambayo amekuwa akiyapata mchezaji huyo wa Chelsea.

Katika msimu uliopita Trent, nyota wa kimataifa wa England alicheza mechi 37 za michuano yote barani Ulaya na kutoa asisti tisa. Hata hivyo mchezaji huyo pia amekuwa katika rada za timu nyingine Ulaya.

JUVENTUS ipo katika hatua za nzuri ili kuipata saini ya kiungo wa Atalanta na timu ya taifa ya Uholanzi, Teun Koopmeiners, 26, ambaye pia anawindwa na Liverpool inayotaka huduma yake kaitka dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi. Teun ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2027, katika msimu uliopita alicheza mechi 51 za michuano yote.

ASTON Villa inahitaji Pauni 60 milioni kutoka Al-Ittihad ili kumuuza mshambuliaji raia wa Ufaransa, Moussa Diaby, 25, katika dirisha hili. Kocha wa Villa, Unai Emery anatamani kusalia na staa huyo, hivyo mabosi wa timu hiyo wanapambana kumbakisha, lakini ikishindikana wanataka kumuuza kwa bei ghali ili pesa itakazopata isajili mbadala wake.

MARSEILLE imefikia makubaliano na Manchester United kumnunua mshambuliaji wa timu hiyo raia wa England, Mason Greenwood kwa ada ya uhamisho ya Pauni 26.7 milioni katika dirisha hili. Greenwood, 22, amevutia timu nyingi Ulaya baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita akiwa na Getafe. Mkataba wa Greenwood unamalizika 2025.

LIVERPOOL imefikia patamu katika mazungumzo na wawakilishi wa beki wa Crystal Palace, Marc Guehi ili kuipata saini yake katika dirisha hili baada ya kuvutiwa na kiwango alichoonyesha tangu kwa msimu uliopita. Hata hivyo, Palace imeonyesha kutokuwa na nia ya kumuuza Guehi kwa sababu imeshamtoa Michael Olise na inaamini akiondoka timu itaharibika zaidi.

STRAIKA wa Chelsea, Romelu Lukaku, 31, amewaambia mabosi wa Napoli yupo tayari kujiunga na timu hiyo, lakini kwa sharti la Victor Osimhen kuuzwa kwani akibaki anaamini anaweza akakosa nafasi ya kucheza. Lukaku ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo AS Roma, mkataba wake na Chelsea unatarajiwa kumalizika 2026.

CHELSEA imefikia makubaliano ya kumsajili beki wa Boca Juniors na timu ya taifa ya Argentina, Aaron Anselmino, 19, katika dirisha hili la usajili wa majira ya joto kwa ada ya Pauni 17 milioni baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu. Anselmino ambaye msimu uliopita alicheza mechi tano za michuano yote, mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.

AL-NASSR imeripotiwa kuachana na mchakato wa kumsajili kipa wa Manchester City, Ederson, 30, baada ya kukataliwa ofa ya Euro 30 milioni. Ederson anayemaliza mkataba 2026 aliwekewa mezani ofa ya mshahara wa Pauni 900,000 kwa wiki. Baada ya kuachana na Ederson, Al Nassr imehamia kwa kipa wa Athletico Paranaense, Bento, 25.

Chanzo: Mwanaspoti