Ni mechi ngumu sana kwa Simba, Al Ahly walikuja na mpango wao Dar es Salaam wakafanikiwa kupata ushindi wa goli 1-0 wakawa na faida ya dakika 90 za mchezo wa kwanza baada ya kupata ushindi ugenini.
Leo Al Ahly wakiwa nyumbani wanahitaji kuulinda ushindi wao, wakipata ushindi au sare yoyote wanakwenda Nusu Fainali. Haitakuwa mara ya kwanza kwa Ahly kuvuka hatua hii kwenda Nusu Fainali.
Ikumbukwe ndio timu ambayo inapambana kufika Fainali kwa mara ya tano [5] mfululizo! Wanajua kucheza hizi mechi kwa namna ya kupata matokeo.
Simba wanaingia kwenye mchezo wa pili wakiwa tayari wamepoteza mchezo wa nyumbani, mara zote silaha ya Simba imekuwa ni uwanja wa nyumbani lakini wakati huu wamepoteza mbele ya timu kubwa na yenye historia ya aina yake kweye mshindano haya.
Mimi naamini Al Ahly wanakwenda kumalizia kile ambacho wameanzanacho Dar es Salaam, Simba wana mlima mrefu sana wa kupanda na ni vigumu kwao kutoboa.
Kwa hiyo nawapa Al Ahly 90% ya kufuzu Nusu Fainali, 10% zilizobaki naziacha kwa Mnyama kwa sababu mchezo wa mpira wa miguu una matokeo ya kushangaza! Simba wanaweza kufanya lolote kwa hizo asilimia 10.