Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Al Ahly wamemwambia ukweli wake MO Dewji?

Mo X Infantino X Motsepe Al Ahly wamemwambia ukweli wake MO Dewji?

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna dunia mbili tofauti ambazo tunaishi. Kuna dunia yetu hii ya Ligi Kuu Bara na hawa kina Tatu Malogo. Halafu kuna dunia ya pili hii ya kina Al Ahly na Patrice Motsepe.

Ni dunia mbili tofauti. Kwenye Ligi Kuu Bara huwa tunasema soka letu kivyetu vyetu. Tunafahamu namna tunacheza mechi zetu. Timu zinafahamu namna gani zinapata ushindi. Ndio dunia yetu.

Haishangazi kuona waamuzi wanakosea kila siku kwa kuibeba timu moja tu.

Yaani kila mwamuzi akikosea anakuwa amezipendelea Simba au Yanga. Akikosea zaidi basi ameinyima Azam FC penalti ya wazi ama goli halali. Mwisho wa siku tunasema ni makosa ya kibinadamu.

Yaani inawezekanaje waamuzi wakosee pale Mbeya kwa kutoa uamuzi wa kuibeba Simba kisha wengine wakafanye makosa kama hayo Singida. Kwanini waamuzi hawakosei na kuzibeba Mtibwa Sugar, Geita Gold, KMC ama nyingine wakati wakicheza na vigogo? Hakuna.

Hii ndiyo dunia yetu. Dunia ambayo Clatous Chama ni staa mkubwa mno. Dunia ambayo Pacome Zouzoua na Yao Kouassi ni mastaa wakubwa mno. Ndiyo dunia yetu. Tunazungumza na kuelewana.

Ni dunia ambayo Ihefu ikiifunga Yanga basi imepania mechi. Hakuna watu wanaoheshimu soka. Hakuna watu wanaheshimu uwekezaji wa Ihefu. Basi tu kwa kuwa ni timu kutoka kijijini, inaonekana ina haki ya kufungwa tu. Inashangaza sana.

Tunaamini zaidi ushirikina kuliko uwezo wa makocha. Yaani ni bora watu wakeshe wakilinda uwanja kuliko kumpa kocha nafasi kubwa ya kusimamia mambo ya kiufundi. Tunaamini katika fitina kuliko soka lenyewe. Ni ajabu na kweli. Ni simanzi kubwa.

Sasa ukitoka katika dunia yetu hii ya kuamini mambo ya nje ya uwanja kuliko ndani ya uwanja, kuna dunia nyingine huko nje. Ni hii dunia ya Al Ahly ya Misri. Hawa wanaishi katika dunia yao.

Malengo ya Al Ahly siku zote ni kutwaa ubingwa wa Afrika. Kila wakianza msimu lengo mama linakuwa kushinda ubingwa wa Afrika ili kwenda kushiriki Klabu Bingwa ya Dunia.

Hivyo uwekezaji wa Al Ahly siku zote unalenga kuiteka Afrika. Wamewekeza zaidi ndani ya uwanja. Thamani ya kikosi cha Al Ahly kwa sasa inakadiriwa kufikia Sh80 bilioni. Ni fedha nyingi sana hata kwa kuzitamka tu.

Ni bajeti ya baadhi ya wizara katika nchi masikini. Ni fedha ambazo unaweza kutengeneza barabara ya lami ya takriban kilomita 80 au zaidi. Ni uwekezaji mkubwa mno.

Yule Hussein EL Shahat peke yake amenunuliwa kwa Dola 5 milioni (Zaidi ya Sh12 bilioni). Ni zaidi ya nusu ya bajeti ya Simba kwa msimu huu. Ni fedha ambayo Al Ahly imetumia kumnunua mchezaji mmoja tu. Tena huyu alianzia benchi dhidi ya Simba hapo juzi.

Hao kina Aliou Dieng, Mahmoud Kahraba, Reda Slim, Percy Tau na wengineo ni uwekezaji mkubwa sana. Fedha imemwagika kukamilisha sajili zao. Fedha nyingi zaidi inatumika kulipa mishahara yao. Ndio uwekezaji wa kushindana kwa ngazi ya Afrika.

Huu ndio ukweli ambao Al Ahly walipaswa kumwambia Mohamed Dewji juzi. Wangemwambia ukweli kuhusu ndoto ya kutwaa ubingwa wa Afrika na uwekezaji unaohitajika. Siyo jambo jepesi hata kidogo. Lazima uwekeze kweli katika timu uwanjani.

Huwezi kutwaa ubingwa wa Afrika kwa kuwategemea hawa kina Willy Onana, Shaban Chilunda, John Bocco na wengineo. Kuna uwekezaji mkubwa zaidi unahitajika pale Simba. Lazima timu isajili wachezaji wa maana zaidi kama huyu Fabrice Ngoma au Che Fondoh Marlone. Ni wachezaji wa daraja la juu.

Hata wakati ule TP Mazembe inatawala soka la Afrika ilifanya uwekezaji mkubwa ndani ya uwanja. Ilikuwa na mastaa kwelikweli.

Kina Kazembe Mihayo, Tresor Mputu, Rainford Kalaba, Given Sunguluma, Ngadu Kasongo na wengineo. Iliwekeza kweli. Baadaye ikawachukua kina Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na wengineo.

Mazembe ikatawala soka la Afrika. Kufika nusu fainali kwao ikawa jambo la kawaida. Siku zote ndoto za Mazembe zilikuwa kutwaa ubingwa wa Afrika. Walifanikiwa sana. Ndani ya miaka 10 wakatwaa Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu na Kombe la Shirikisho Afrka mara mbili.

Nini siri kubwa ya mafanikio yao? Ilikuwa uwekezaji wao. Walichukua wachezaji bora kutoka nchini mwao. Wakasajili wachezaji bora kutoka nchi nyingine. Wakawa na kikosi imara. Wakashindana na Waarabu katika mbio za uwanjani.

Siku zote tunaweza kuona kama Waarabu wanatuonea, lakini ukweli ni kwamba wamewekeza sana ndani ya uwanja. Ni kama wanavyofanya Mamelodi Sundowns kwa sasa. Ndiyo timu ya ukanda wa Kusini mwa Afrika ambayo imewekeza kwelikweli ndani ya uwanja. Inaweza kushindana na Waarabu.

Chanzo: Mwanaspoti