Kingo kutoka nchini Nigeria na Klabu ya Simba SC Victor Patrick Akpan ambaye kwa sasa anaitumikia Ihefu FC kwa mkopo wa nusu msimu amesema, kitendo cha kuaminiwa na Kocha John Simkoko kinazidi kumuimarisha na anaamini atarejea tena kwenye timu yake kupambania namba.
Akpan alisajiliwa na Simba SC msimu huu akitokea Coastal Union ya Tanga kwa mkataba wa miaka miwili ambapo amedumu ndani ya kikosi cha Msimbazi kwa nusu msimu na kutolewa kwa mkopo baada ya kushindwa kupigania namba.
Akpan amesema kuwa majeraha ya mara kwa mara yalikuwa kikwazo kwake na kushindwa kuonesha ubora wake lakini tangu ametua Ihefu ameanza kurejea kwenye ubora wake ambao utamfanya arudi kutetea namba kwa waajiri wake Simba.
“Natambua uwezo wangu sio wa kushindwa kucheza Simba SC bali majeraha ndio yalikuwa yananirudisha nyuma ila kwa sasa nipo vizuri sana hata ikitokea narudi Msimbazi leo, kila mmoja ataona ubora wangu,”
“Unajua unapocheza ndani ya timu kubwa kama Simba SC lazima kwanza uwe na hofu muda wote ni timu ambayo ina mashabiki wengi na wanataka kukuona ukifanya vizuri wakati wote,” amesema Akpan.
Aidha, mchezaji huyo amekanusha taarifa ya kwanza anaomba kurudi kwenye timu yake ya zamani ya Coastal Union.
“Kwa kweli mimi bado mchezaji wa Simba SC na mkataba wangu mpaka mwisho wa msimu utakuwa imebaki mwaka mmoja, nina furaha kucheza hapa Ihefu FC kwa kuwa nimekuja kujiweka imara.”
“Taarifa za kurudi Coastal Union hazina ukweli wowote lakini mwisho wa msimu ndio itafahamika zaidi wapi nitaelekea huenda nikarudi Simba au nikaondoka nje ya Tanzania,” amesema Akpan.