Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Akili ya Benchikha na mtego wa Gamondi

Benchikha X Gamondi Akili ya Benchikha na mtego wa Gamondi

Sat, 13 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Aprili 20 ni kivumbi na jasho kwenye Uwanja wa Mkapa. Simba inakwenda kukutana na Yanga, ikiwa na kumbukumbu mbaya ya mchezo wa mwisho Novemba 5 mwaka jana. Simba ilifungwa mabao 5-1.

Hayakuwa matokeo mazuri kwa upande wao, ilifedheheka, ilinyanyasika na kuingia unyonge ambao uliifanya ishindwe kutamba katika vijiwe vya mazungumzo ya soka, huku watani zao wa jadi Yanga, ikitembea kifua mbele.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi aliweka mtego katika nyakati ambazo Simba ilipoupoteza mpira, alifahamu inachelewa sana kufunga mianya yao na kama inakutana na timu yenye wakimbiaji wazuri basi inakaribisha shida kwenye lango lao katika kila muda ambao itakuwa inashambuliwa.

Ukiyatazama mabao matano ambayo Yanga iliyafunga katika mchezo wa dabi uliopita, asilimia kubwa yalipatikana baada ya Simba kupoteza mpira. Katika soka ni kawaida kwa timu yoyote duniani kubomoa umbo la ulinzi inaposhambulia na inavyotakiwa ni wao wawe haraka kuliunda tena umbo hilo la ulinzi ili kuziba njia za pasi za wapinzani na kupunguza madhara baada ya kuupoteza mpira.

Ukizitazama timu zote mbili katika kipindi hiki ambacho wanaendelea kucheza mechi zao nyingine bado Simba inaonekana kuwa na tatizo ile ile ambalo mara kadhaa limekuwa kikiifanya iruhusu mabao. Angalau katika mechi ambazo Simba imekuwa ikitumia viungo watatu wakabaji wamekuwa wagumu kupitika ila si katika daraja wanalotakiwa wawepo kama timu kubwa.

Ukimwona Sadio Kanoute, Babacar Sarr na Fabrice Ngoma wameanza pamoja, hapa maana yake Simba inapopoteza mpira inakaba kwa kutumia muundo wa 4-3-3 (mabeki wanne, viungo wa kati wawili na washambuliaji watatu).

Wanapitika lakini si kama wanavyotumia muundo wa 4-2-3-1 (mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na mshambuliaji mmoja) ambao katikati kunakuwa na Ngoma na Babacar.

Shida kwao wanapotumia viungo watatu wakabaji, wanapata shida kwenda mbele kwa sababu ya kuzikosa pasi sahihi kutoka kwenye eneo la kiungo, tutaiona akili ya Benchikha juu ya nini atafanya ili kutibu matatizo yake ya msingi ili kushinda mechi hii ya watani wa jadi ambayo mashabiki wengi wa Simba wanaonekana kuihofia.

Kwa Gamondi unaweza kusema kwa asilimia kubwa vitu vingi vipo sawa, ingawa bado hii ni dabi lolote linaweza kutokea. Kwa upande wake kuanzia muundo wa uchezaji, uwajibikaji wa wachezaji wake na ufanisi wa matendo, anapata mabao mengi kutoka kwenye eneo la kiungo licha ya washambuliaji wake kupoteza sana nafasi za kufunga mabao, timu yake inakuwa na kasi kubwa ya kuziba mianya baada ya kupoteza mpira.

Wanakaba vizuri na kwa asilimia kubwa kwani Gamondi amekuwa muumini wa kutumia muundo wa 4-2-3-1 na mara chache hutumia muundo unaohusisha walinzi watatu nyuma (3-5-2, 3-4-3), wanaposhambulia wanatumia namba 10 karibu wawili au watatu (Aziz Ki, Maxi na Pacome) kwa kupishana na kubadilishana nafasi na msingi wao mkubwa wa kufunga mabao uko hapo.

Si kwa bahati mbaya kwa Yanga kwa sababu wao ndio timu yenye mwendelezo bora wa kiwango katika soka la Tanzania kwa sasa.

Bahati mbaya kwenye mchezo wa dabi hujui nini kitatokea na nani atapotea, bila shaka Gamondi analifahamu hili, mechi za dabi ni mjumuisho wa mambo mengi kuanzia maandalizi ya kimwili na kiakili, ni mechi ambazo zina mazingira tofauti na mechi nyingine za kawaida. Je, ni nini kitatokea kwenye dabi ya wikiendi ijayo Kwa Mkapa? Tusubiri kuliona hili.

Chanzo: Mwanaspoti