Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Akili Bandia ilivyoweka bayana mkeka wa makocha Ulaya

Artif Intel Akili Bandia ilivyoweka bayana mkeka wa makocha Ulaya

Sat, 25 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu kubwa za Ulaya zitaingia sokoni kwenye dirisha la majira ya kiangazi likapofunguliwa ili kusaka makocha wapya kwa ajili ya msimu wa 2024-25.

Miamba ya soka kama Chelsea, Bayern Munich na Juventus ni miongoni mwa vigogo wa Ulaya vitakavyokuwa bize kusaka makocha wapya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Mauricio Pochettino ameshtua wengi baada ya kuachana na Chelsea baada ya msimu wa Ligi Kuu England ulipofika tamati wiki iliyopita.

Bayern yenyewe bado ipo sokoni kutafuta kocha wa kuja kuchukua mikoba ya Thomas Tuchel, wakati Juventus yenyewe inataka kocha mpya baada ya kumfuta kazi Massimiliano Allegri. Wakati klabu nyingi kubwa kutaka makocha wapya, zile zitakazofanya haraka na kuwa na pesa za kutosha ndizo zitakazofanikiwa kunasa makocha wenye vipaji.

Lakini, wakali wa masuala ya uhamisho wa wachezaji na makocha, walitumia Akili ya Bandia (AI) kutambua ni makocha gani watakaofukuziwa na klabu hizo zinazosaka mabosi wapya wa mabenchi yao ya ufundi.

Chelsea - Julian Nagelsmann

Chaguo la kwanza la Akili Bandia kwa Chelsea ni kocha wa zamani wa Bayern Munich, Julian Nagelsmann.

Kwa sasa Nagelsmann ni kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani na anatazamwa kama mmoja wa makocha vijana wenye ubunifu mkubwa kwenye soka. Nagelsmann ana rekodi nzuri ya kukuza viwango vya wachezaji vijana wanaotamba Ulaya kwa sasa. Akiwa na umri wa miaka 34, anaweza kwenda kuwa msaada mkubwa wa kubadili hali ya mambo huko Stamford Bridge endapo itafanikiwa kunasa saini yake.

Makocha wengine waliopendekezwa na AI kwenye mpango huo wa kuinoa Chelsea ni Erik ten Hag, Allegri, Brendan Rogers na Tuchel.

Manchester United - Zinedine Zidane

Zinedine Zidane anatajwa kuwa namba moja kwenye makocha wanaoweza kutua kuinoa Manchester United kwa mujibu wa AI. Kocha huyo Mfaransa alipata mafanikio makubwa kwa awali zake mbili alizokuwa Real Madrid na aliweka rekodi ya kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo.

Kocha Erik Ten Hag bado yupo Man United, lakini kinachoonekana ni huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea endapo timu itashindwa kubeba Kombe la FA. Zidane atarejesha akili ya ushindi kwenye kikosi hicho cha Old Trafford na kupata nguvu ya kunasa mastaa wenye majina makubwa.

AI imetaja makocha wengine pia wanaoweza kutua Man United ni Pochettino, Nagelsmann, Antonio Conte na Luis Enrique.

Bayern Munich - Roberto De Zerbi

Bayern Munich pengine ipo kwenye hatua za mwisho kabisa za kumpa kazi Vincent Kompany kwenda kuchukua mikoba ya Tuchel, lakini jina la Roberto De Zerbi ndilo lililochaguliwa na AI litatua kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Bundesliga. Kocha huyo Mtaliano aliachana na Brighton baada ya msimu wa Ligi Kuu England kumalizika, kitu ambacho kilishtua wengi. AI inafichua staili ya soka la kushambulia la De Zerbi litakwenda sawa na mtindo wa Bayern hasa kutokana na wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho kwa sasa. Makocha wengine waliotajwa AI kwenye kibarua cha kwenda kuinoa Bayern ni Pochettino na Enrique, huku wengine ni Gian Piero Gasperini na Allegri.

Barcelona - Marcelo Gallardo

AI imemchagua Marcelo Gallardo kuwa chaguo la kwanza kwa wale watakaokwenda kurithi mikoba ya Xavi huko kwenye kikosi cha Barcelona. Muargentina huyo kwa sasa yupo huru baada ya kuachana na Al-Ittihad - lakini huko nyuma aliwahi kuhusishwa na Barcelona.

Gallardo anaweza kwenda kuifanya Barcelona kurudi kwenye ubora wake kutokana na ujuzi wake wa kutumia soka la ujuzi mwingi na mbinu za mchezo.

Makocha wengine waliotajwa na AI kwenye uwezekano wa kwenda kuinoa miamba hiyo ya La Liga ni pamoja na Ten Hag, De Zerbi, Nagelsmann na Mikel Arteta.

Juventus - Zinedine Zidane

Kama ilivyo kwa Man United, Zidane ametajwa tena na AI ni chaguo la kwanza huko Juventus.

Mfaransa huyo aliwahi kuichezea Juventus huko kwenye Serie A, hivyo anaweza kurudi kufanya kazi kwenye klabu yake zamani na kuirudisha makali yake ya kutamba kwenye soka la Ulaya.

Zidane aliichezea Juventus kati ya mwaka 1996 na 2001 na ana ufahamu mzuri wa utamaduni na historia ya klabu hiyo. Lakini, Kocha wa Bologna, Thiago Motta kwa sasa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa timu hiyo ya Turin.

Makocha wengine waliitajwa na AI ni Conte, Pochettino, Gasperini na Allegri.

AC Milan - Mauricio Pochettino

AI imefichua kocha anayepewa nafasi kubwa ya kwenda kuinoa AC Milan ni Pochettino itakapoachana na Stefano Pioli. Muargentina atapeleka uzoefu mkubwa wa kuzinoa klabu za Chelsea, Tottenham, Paris Saint-Germain na Southampton huko AC Milan. Pochettino ni mzuri na kucheza soka zuri lenye kuvutia na pasi za kutosha. Timu zake zimekuwa zikicheza soka la kushambulia sana kitu ambacho kinaendana kabisa na falsafa za Milan.

Makocha wengine waliotajwa na AI kwenye uwezekano wa kwenda kuinoa AC Milan ni pamoja na Ralph Hasenhuttl, Allegri, Gasperini na Ten Hag. Milan ilikuwa ikihusishwa na Julen Lopetegui, lakini kocha huyo kwa sasa amechapata kazi huko West Ham United, alikoenda kurithi mikoba ya David Moyes.

Brighton - Ralph Hasenhuttl

AI inaamini kocha wa zamani wa Southampton, Hasenhuttl anafaa kwenda kufanya kazi Seagulls.

Bosi huyo wa Austria amekuwa hana kazi tangu alipofutwa kazi Southampton hadi hapo alipojiunga na Wolfsburg. Kocha huyo aliisaidia timu hiyo kuondoka kwenye kundi la kushuka daraja na haonekani kuwa na mpango wa kuachana na timu hiyo. Brighton inaweza kuwa na imani ya kumng’oa Hasenhuttl na kwenda kumpa kazi ya kuwanoa vijana wao wenye vipaji vikubwa kwenye kikosi chao.

AI imewataja makocha wengine pia wenye uwezo wa kwenda kuinoa Brighton ni Gasperini, Marco Rose na Lucien Favre. Kwenye uhalisia, makocha wanaopigiwa hesabu na Brighton kwa sasa ni McKenna na Francesco Farioli.

Chanzo: Mwanaspoti