Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aishi atoa neno Simba

3dc82bf90f5b45920c3b5ec6e411cb82.jpeg Aishi atoa neno Simba

Thu, 1 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MLINDA mlango namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania na klabu ya Simba, Aishi Manula amesema licha ya klabu yake kuwa vinara wa Kundi A, wataingia kwa tahadhari kubwa katika mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Simba ikiwa na pointi 10 baada ya kushuka uwanjani mara nne, itakuwa mwenyeji wa AS Vita inayoshika nafasi ya tatu katika mchezo wa tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na HabariLEO jana, Manula alisema ana amini kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kwa pande zote mbili, kwani lengo lao ni kufuzu na kumaliza katika nafasi ya kwanza wakati wapinzani wao wakitaka kulipa kisasi pamoja na kusaka nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali.

“Mchezo wa soka una matokeo matatu kushinda, kushindwa na kutoka sare, mwalimu ametueleza na wachezaji wote tunajua kwamba utakuwa mchezo mgumu kwa sababu kama sisi tuliweza kushinda kwao, hata wao wanaweza kufanya hivyo kwetu kama hatutakuwa makini,” alisema.

Manula alisema mbali na mbinu walizopewa na kocha mkuu Didier Gomes ambaye amekuwa akisisitiza wachezaji kuongeza umakini ili kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu ili kuongeza wigo wa pointi na wale wanaowafuatia.

Alisema wanapaswa kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kuingia uwanjani kwa kuwaheshimu AS Vita ambao ni moja ya timu ngumu na yenye uzoefu katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha wa Simba, Gomes Da amesema atatumia muda uliobaki kusoma video ya AS Vita katika kipindi hiki kilichobaki kabla ya kukutana na wakali hao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumamosi.

Simba inahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa klabu Afrika.

Hata hivyo, zikiwa zimebaki siku chache kabla ya mchezo huo, Gomes amelalamikia kuwakosa baadhi ya nyota wake ambao walikwenda kuzichezea timu zao za taifa mechi za kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika. Afcon, ambao bado hawajarudi.

Alisema timu yake itakuwa na muda mdogo wa kuendesha darasa la kuisoma vita kupitia mikanda ya video wakati wachezaji hao watakaporudi.

“Binafsi nimeshaangalia video za mechi za timu hiyo na kuna mambo nimeyabaini lakini sasa nataka kuwaonyesha wachezaji wangu ili wajue nini cha kufanya ndani ya dakika 90 za mchezo huo dhidi ya AS Vita.”

“Baada ya kuangalia video hizo Aprili 2 (siku ya Ijumaa Kuu), tutafanya mazoezi mepesi uwanjani kufanya baadhi ya mbinu za kiufundi kupitia video kutoka AS Vita jinsi ya kuzuia na kuwashambulia,” alisema.

Gomes pia alisema wanakabiliwa na kibarua kigumu kwani AS Vita nao pia wanasaka ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga robo fainali, kitu ambacho wanaweza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz