Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Air Manula wala asiwe na wasiwasi nafasi yake ipo salama

Aishi Manula Wasi Wasi Aishi Manula

Wed, 9 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unapokuwa Aishi Manula nyakati hizi unakuwa na wasiwasi mwingi. Wakati upo kwako Kitunda unaambiwa kwamba Simba imepeleka golikipa kutoka Brazil katika kambi yao ya Uturuki. Moyo wako unapatwa na wasiwasi.

Hakuna mwanadamu ambaye hana hofu na kazi yake. kazi ni maisha. Kazi ni kila kitu. Lazima Aishi alipatwa na hofu. Kipa mrefu kutoka taifa kubwa kama Brazil anapokwenda katika kambi ya timu Uturuki wakati wewe upo nyumbani, lazima upatwe na wasiwasi.

Sijui kimetokea nini haswa kwa kipa huyu. Ghafla Simba walitangaza kuachana naye ingawa walikuwa wamemtangaza siku chache. Tunaambiwa ni majeraha. Wengine wana hisia tofauti kwamba huenda hakuwa mzuri sana na ndio maana Simba waliachana naye.

Lakini sasa Simba wameamua kwenda kwa golikipa mwingine, Hussein Abel kutoka KMC. Vyovyote ilivyo, Aishi kuwa na wasiwasi. Naiona nafasi yake ya kwanza katika lango la Simba. Huwa haipotei kiurahisi katika miaka ya karibuni.

Kuna nafasi mbili ambazo ni ngumu kwa timu kupata wabadala wake. wafungaji na hii nafasi ya kulinda lango. Huku langoni angalia namna ambavyo kwa muda mrefu sasa Tanzania hatuzalishi makipa wa maana. Makipa wengi ni wa kawaida tu.

Zamani tulikuwa na makipa wengi hodari, warefu na mashujaa langoni. Sasa hivi kwa soka la ndani tuna makipa wengi wafupi, sio mashujaa na wanashindwa kutumia misingi ya ukipa kulinda lango. Kwanini Aishi Manula awe na wasiwasi.

Msimu uliopita nimetazama mechi nyingi za Ligi Kuu na makipa wamefungwa mabao mengi ya kipuuzi mpaka unajiuliza kama kuna kipa mzawa anayeweza kumng’oa Aishi katika lango la Simba achilia mbali timu ya Taifa ya Tanzania.

Lakini hata nje ya nchi makipa hawapo wengi na ndio maana timu ikipata kipa mzuri wanakaaa naye kwa muda mrefu. Huyu Aishi mwenyewe alipoondoka Azam lango lao halikuwahi kutulia tena mpaka majuzi walipompata kipa kutoka Ghana ambaye anaonekana kuwa mzuri na mwenye kimo sahihi.

Ni hawa hawa Azam wenyewe walirudi tena kwa Aishi wakitaka arudi katika lango katika dirisha kubwa lililopita la uhamisho. Hawajawahi kumsamehe mtu ambaye aliruhusu Aishi aende Simba kijinga. Kuanzia hapo wameingia hasara kubwa karibu kila msimu kusaka kipa mpya. majuzi tu walituletea hadi kipa ambaye wanadai alikuwa anadaka katika Ligi Kuu ya Ufaransa. Kumbe hakuna kitu.

Jiulize, Yanga kabla ya kumnasa Djigui Diarra waliwahi kuwa na kipa gani makini? Wamepita makipa wengi ambao wote walikuwa wa kawaida tu. kipa aliyeshtua kidogo alikuwa Beno Kakolanya ambaye si ajabu ndio maana alikuwa anawaringia.

Vinginevyo tangu enzi za kina Yaw Berko Yanga hajaiwahi kupata kipa makini kiasi cha kumuamini kwenda naye vitani kiurahisi. Hii nafasi ni adimu. Hawa hawa Simba katika dirisha hili walijua kwamba wanahitaji kuwa na kipa mahiri baada ya Aishi kuonekana angekuwa nje kwa muda mrefu.

Matokeo yake ilikuwa rahisi kwao kuwanasa wachezaji wa nafasi za ndani mapema kuliko kipa. Waliwanasa kina Willy Onana Osamba mapema tu lakini mpaka dakika za majeruhi walikuwa wanahaha kusaka kipa. Kisa? Makipa mahiri wapo wachache na waliopo tayari wana mikataba na klabu zao.

Dennis Onyango ana miaka 38 sasa hivi lakini bado Mamelodi hawamuachii. Kwanini? Sio rahisi sana kupata kipa wa aina yake. kuna makipa wengi vijana Afrika Kusini lakini je wamefikia sifa zake? Mamelodi wakitaka kumuachia Onyango labda wampate Aishi Manula. Inapofikia hapo kila mtu anaamua kubakia na kipa wake.

Tatizo la makipa linawatesa hata wazungu. Ni kama ilivyo kwa tatizo la wafungaji wa aina ya Fiston Mayele. Mpaka sasa Yanga watakuwa wanajiuliza kama mshambuliaji wao mpya Hazif Konkoni ataweza kuziba pengo la Mayele. Haiwi rahisi sana.

Wale wale Yanga iliwachukua muda mrefu kuziba pengo la Herritier Makambo baada ya staa huyu wa Congo kuondoka kwenda Horoya. Walijaribu kusaka washambuliaji lukuki hapo katikati lakini haikuwezekana.

Walileta washambuliaji wa ajabu kina Yikpe mpaka mashabiki wakakata tamaa. Baadaye wakaamua kumrudisha Makambo mwenyewe huku bahati ya mtende pia ikiwaangukia kwa kumpata Mayele katika dirisha hilo hilo la uhamisho.

Mara ngapi Azam walimtamani tena John Bocco arudi kikosini kwao? Kupata wafungaji na makipa sio kazi rahisi sana kama watu wengi wanavyofikiri. Aishi anapaswa kurudi na ubora wake pia atakapokuwa timamu wa mwili lakini siamini kama Simba wataweza kuliziba pengo lake kwa urahisi.

Amepitia mengi pale Simba. alipofungwa bao la mbali na Mapinduzi Balama katika pambano la watani wa jadi kuna watu wa Simba walijaribu kumgeuka. Mechi iliyofuata akapangwa Kakolanya. Akaanza kufanya makosa. Wakamgeukia Aishi tena kimya kimya.

Namkumbuka rafiki yangu kiongozi wa Simba aliwahi kunipigia simu akimshutumu kwamba bao ambalo Aishi alifungwa na Aziz Ki aliupanga vibaya ukuta wake kwa makusudi ili afungwe. Nikamuuliza kwanini wasiachane naye kama mnaamini anawafungisha makusudi? Akanijibu kwa upole tu “ni ngumu kupata kipa mwingine kama Aishi kwa sasa”. Huu ndio uhusiano wa shaka alionao Aishi na watu wa Simba.

Nadhani mwenyewe anafahamu. Kinachofurahisha zaidi ni kwamba pindi atakaporudi katika lango la Simba atapata heshima kubwa zaidi kwa sababu viongozi watakuwa wameona ugumu wa kupata makipa bora katika bara la Afrika kwa sasa. Haiwi rahisi sana kama ambavyo viongozi wanavyojiaminisha. Aishi asiwe na wasiwasi.

Naamini Simba wangeweza kufika nusu fainali ya CAF kama wangekuwa na Aishi langoni. Wydad hawakuwa na ubora wao walipocheza na Simba katika mechi zote mbili. Mechi ya kwanza Simba walikosa mabao mengi pale Taifa.

Mechi ya pili Simba walifungwa bao jepesi la kichwa pale Casablanca na naamini Aishi angekuwa langoni angecheza. Lilipokuja suala la penalti, licha ya kwamba Clatous Chama na Shomari Kapombe walikosa lakini bado naamini kipa wao, Ally Salim hakuwa na ubora wa kucheza penalti. Aishi asingeruhusu penalti zote nne katika nyavu zake. Ametuthibitishia hilo mara nyingi tu tangu alipokuwa anacheza michuano ya Cocacola hadi alipoenda Azam.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: