Afisa habari wa klabu ya wekundu wa msimbazi Simba Sc, Ahmed Ally amewajibu baadhi ya mashabiki na wapenzi wa soka wanaosema timu hiyo ni mbovu.
Ameeleza hayo katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika mapema ya jana Machi 13, 2023 jijini Dar es Salaam.
Ahmed amesema wao sio wabovu ndio maana wanashiriki Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwa sababu timu zote mbovu zilishatolewa kushiriki mashindano hayo.
“Hakuna timu mbovu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu zilishatolewa katika mashindano hayo,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa ligi ya mabingwa wakati inaanza ilikua na zaidi ya timu 200 ambapo yalifanyika mashindano na zilizokuwa mbovu zote zikatolewa na kubaki timu 16 ambazo zote ni timu nzuri zenye kuujua mpira vizuri.
“Championship wakati inaanza ilikua na timu zaidi ya 200, mbovu zote zikatolewa zikabaki timu 16, ambao ndio sisi tunaoshiriki na wote 16 tunacheza vizuri na timu zetu ni nzuri,” amesema Ahmed.
Aidha Ahmed amekiri kuwa ni kweli watu wanavyosema kuwa Simba inashinda lakini haina furaha kutokana na kushinda kwa bahati tena ushindi mwembamba ambao unawafanya wawe na presha kabla ya mchezo kuisha.
“Ni kweli huwa tunashikilia roho kwa sababu unaposhinda goli moja ni lazima uwe na wasiwasi kuwa lile goli litarudishwa haijalishi unacheza mpira mkubwa kiasi gani lazima ukae kwa mashaka” amesema Ahmed.
Ahmed amesema haya baada ya mechi yao ya kimataifa dhidi ya Vipers kushinda 1-0 na kupelekea watu kuzungumza mengi ikiwemo kuwaita wabovu kutokana na kushinda ushindi mwembamba wa 1-0 kila mechi iliyowapa ushindi.
Mechi inayofuata ni Simba dhidi ya Horoya ambayo itapigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Machi 18, mwaka huu.