Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema kuwa hakuna ugumu wowote wa kucheza mchezo bila kuwa na kocha wao mkuu, Abdelhak Benchikha.
Ahmed amesema hayo mara baada ya kutua Tanga kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Coastal Union utakaopigwa kesho Jumamosi katika Dimba la Mkwakwani huku Mnyama akiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons kwa kipigo cha bao 2-1.
Benchika ameondoka jana Simba kuelekea nchini kwao Algeria kwa ajili ya kuhudhuria kozi fupi ya siku tano huku akiiacha timu chini ya kocha msaidizi Farid Zemiti.
"Baada ya mchezo, Kocha Benchikha alikaa na wachezaji na kuanisha makosa yote yaliyofanyika na kusababisha tukapoteza mchezo ule. Kisha alikaa na benchi lake la ufundi akawambia wapi kulikuwa na shida kwenye mchezo ule.
"Baada ya hapo akaandaa mpango kwa ajili ya kwenda kukabiliana na Coastal Union kabla ya yeye kuondoka kwenda nyumbani kwao Algeria kwenye kozi.
"Kwa hiyo hakutakuwa na athari yoyote kwenye michezo yetu ijayo sababu aliyowaacha kikosini tuna watu wenye uwezo mkubwa sana kwenye soka na yule Kocha Farid ndiyo akili ya Benchikha.
"Niwatoe mashaka wanasimba, hakutakuwa na pengo la Benchikha, hata wachezaji wanajua falsafa ya mwalimu na anataka tucheze mpira wa namna gani. Hawawezi kusahau maelekezo yake ndani ya siku mbili. Hakuna ugumu wowote wa kucheza bila kuwa na Kocha Benchikha," amesema Ahmed.