Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Agyei kumrithi Mbrazil Singida Big Stars

Enock Atta Agyei.jpeg Enock Atta Agyei

Wed, 14 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uongozi wa timu ya Singida Big Stars, uko katika mchakato wa kuinasa saini ya aliyekuwa nyota wa Azam FC, Enock Atta Agyei, kutoka nchini Ghana kuelekea usajili wa dirisha dogo linalofunguliwa Alhamisi wiki hii, imeelezwa.

Nyota huyo aliyewahi kuitumikia Azam FC mwaka 2016 na baadaye kutemwa na 'Wanalambalamba' hao, 2019 hadi 2020 alijiunga na Klabu ya Horoya AC ya Guinea na sasa ni mchezaji huru.

Agyei anayeweza kucheza winga wa kushoto na kulia, yuko katika mazungumzo ya kutua ndani ya kikosi cha Singida Big Stars kuchukuwa nafasi ya Mbrazil Peterson Silvano Da Cruz aliyevunja mkataba na klabu hiyo kwa sababu ya matatizo ya kifamilia na kurejea kwao Brazil.

Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana kutokana ndani ya uongozi wa Singida Big Stars, zimeeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamefikia mahali pazuri na muda wowote anaweza kuja nchini kujiunga na kikosi hicho.

“Ni kweli nyota huyo tunafanya naye mazungumzo na yanaenda vizuri kuja kuitumikia timu yetu kipindi cha usajili wa dirisha dogo ili kuongeza nguvu ndani ya kikosi chetu,” kilieleza chanzo chetu.

Ofisa Habari wa Singida Big Stars, Hassan Massanza, alisema kwa sasa suala la usajili limeachiwa benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu Hans Van Pluijm.

Alisema kuhusu nyota wao Da Cruz, amevunja mkataba kwa sababu ya matatizo ya kifamilia na tayari amerejea kwao Brazil.

“Usajili tutafanya kulingana na mapendekezo ya benchi letu la ufundi, nani na nani watasajiliwa hilo suala litakuja baada ya kupokea ripoti ya kocha, kwa sasa tunaendelea kujiandaa kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Massanza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live