Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aggrey amnyooshea mikono Mayele

Aggrey Morris Aggrey amnyooshea mikono Mayele

Sat, 9 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Beki tegemeo wa Azam FC, Aggrey Morris amekiri kwa mdomo wake kuwa, Fiston Mayele wa Yanga analijua lango. Mayele alifunga bao la ushindi wa 2-1 dhidi ya Azam juzi usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Aggrey na mwenzie Abdallah Kheri ‘Sebo’ walikuwa na bato la hatari dhidi ya Mayele kuhakikisha hafungi au kuleta madhara langoni mwa Azam na kazi hiyo waliifanikisha kwa dakika 77 tu. Baada ya hapo straika huyo akawazidi akili na kutetema baada ya kutupia dakika ya 78 akiunganisha krosi ya Djuma Shaban na kumuacha kipa Ahmed Salula akiokota mpira nyavuni.

Staa huyo alikiri Mayele anafanya kazi yake kama straika na hakuona shida kumpongeza kwa bidii aliyoionyesha kuitetea timu yake, ipate pointi tatu.

“Soka ndivyo lilivyo, Mayele kapambana kafunga, upande wangu nilipambana kuilinda timu yangu ila Yanga wakatumia mapungufu yetu kutuadhibu, hatuwezi kuishia hapo tunajipanga kwa mechi zijazo,” alisema Aggrey na kuongeza;

“Mayele anajua kufunga na hakati tamaa, yote katika yote mpira sio uhasama nimpongeze kisha maisha mengine yaendelee.”

Mfungaji wa bao la Azam, Rodgers Kola aliyemtungua kipa wa Yanga, Djigui Diarra dakika ya 10 akipokea asisti ya Bruce Kangwa, alisema japo wamezikosa pointi tatu, ila waliupiga mpira mwingi.

Kola aliyefikisha bao la tano, alisema matokeo ya soka hayaangalii nani kacheza vizuri, ila nani anamaliza kwa ushindi ili kuzipata pointi tatu muhimu.

“Sijaona kama Yanga imecheza sana kuliko sisi, tumejituma sana, ila kwenye mpira kosa moja linakuadhibu ndicho ilichokifanya Yanga,” alisema.

Bao la juzi limemfanya Mayele kuwa kinara akifikisha mabao 11 akimuacha Reliants Lusajo wa Namungio wenye 10.

SURE BOY DAH!

Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amedhihirisha Yanga haijakosea kumsajili baada ya kutawala vilivyo eneo la kiungo katika mechi ya juzi dhidi ya Azam.

Katika mchezo huo Sure Boy alikuwa anacheza sambamba na Zawadi Mauya aliyekuwa akicheza kwenye eneo la ukabaji zaidi na kumuacha mwenzake aweze kusambaza mipira yake pembe zote na hata katikati.

Upande wa Azam alicheza Kenneth Muguna na Mudathir Yahya ambao kipindi cha kwanza walicheza kwa maelewano mazuri huku wepesi wao wa kupiga pasi za pembeni (kwa mawinga) hasa upande wa kushoto kulionekana kuwa na faida zaidi.

Sure Boy pia alikuwa mwepesi wa kupiga mashuti na dakika 62 baada ya Yanga kupata kona na mpira kutoka nje ya boksi kiungo huyu alifyatuka shuti kali na kupita pembeni kidogo ya goli na kuwafanya mashabiki washike vichwa.

“Nilijiandaa kwa mchezo huu na kujua ni mechi ngumu, nilifanya hivyo nje ya mazoezi ya mwalimu na lengo niwe kwenye ubora na nashukuru Mungu kwa kiasi kikubwa nimefanya kitu kizuri nilipokuwa nipo uwanjani,” alisema Sure Boy.

Aidha Sure Boy alifichua alipokea simu ya baba yake mzazi (Abubakar Salum), aliyemuelekeza; “Nilimuahidi baba sitamuangusha kwa kufuata misingi aliyonielekeza haikuwa ngumu kwangu kulitimiza hilo kutokana nilikuwa nimejiandaa vya kutoka kiakili na mwili na nashukuru nimekwenda kutimiza ahadi,kwa aina ya viungo hawa ninao kutana nao najiona kuendelea kufanya vizuri.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz