Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika wapo, Ufaransa wapo

Ufaransa Waafrika Afrika wapo, Ufaransa wapo

Sat, 17 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya Morocco kuwa ni Taifa la Afrika lakini kwenye mechi ya nusu fainali dhidi ya Ufaransa baadhi ya mashabiki wa soka kutoka barani Afrika walikuwa wakishangilia Ufaransa wakiamini ina mastaa wengi wenye asili ya Afrika.

Ni kweli Ufaransa ni miongoni mwa mataifa ambayo yanawakilishwa na wachezaji wengi wenye asili ya Bara la Afrika aidha kwa kuzaliwa ama chimbuko la familia zao.

Hawa hapa ni mastaa wa Ufaransa walioanza kwenye kikosi cha kwanza dhidi ya Morocco na waliokaa benchi ambao wana uraia ama asili ya Afrika.

Jules Kounde

Mbali ya kuzaliwa Ufaransa beki huyu kisiki ambaye alianza kwenye mechi, ana uraia pacha kwa sababu baba yake anatokea Benin, Hivyo ana uraia wa Benin na Ufaransa.

Hata hivyo, hakucheza kwenye timu yoyote ya vijana ya Taifa ya Benin, maisha yake ya soka yote yamekuwa nchini Ufaransa pekee.

Aurelien TchouamÈni

Amecheza mechi zote sita za Ufaransa na kufunga bao moja, mbali ya kuzaliwa na kuishi Ufaransa tangu amezaliwa, jamaa pia ana uraia wa Cameroon taifa ambalo baba yake alitokea kabla ya kuingia Ufaransa kwa ajili ya kutafuta maisha. Huyu pia hajacheza timu yoyote ya taifa ya vijana ya Cameroon.

Fofana

Jamaa ni tofauti kidogo yeye ana asili ya nchi tatu za Afrika, kwanza amezaliwa Ufaransa ambapo ndiko alikochagua kuichezea timu ya taifa ya huko, lakini asili hasa ya wazazi wake wote ni Ivory Coast na inadaiwa kwamba walitua Ufaransa kwa ajili ya kusaka maisha bora.

Mbali na Ivory Coast jamaa anadaiwa ana asili ya Mali ambapo baadhi ya ndugu zake wanatokea huko.

Ibrahima Konate

Amezaliwa katika Jiji la Paris, Ufaransa lakini wazazi wake wote wanatokea Mali, kwenye michuano hii amecheza mechi nne tu ikiwemo na ile ya juzi Jumatano.

Ana uraia wa nchi zote hizo mbili lakini hakuwahi kucheza kwenye timu yoyote ya vijana ya Mali ingawa inadaiwa huwa anaenda nchini humo mara kwa mara na kutoa misaada. Jamaa ni miongoni mwa mabeki tegemeo wa Ufaransa kwa sasa.

Ousmane Dembele

Jamaa huyu ana asili ya huko Maurtania, ingawa hadi sasa hajachukua uraia pacha na kuwa raia wa nchi hiyo lakini ukweli ni kwamba wazazi wake wote wawili waliingia Ufaransa wakitokea nchi hiyo na walikuwa kwenye harakati za kutafuta maisha bora.

Katika kuonyesha Uafrika wake Dembele ameoa nchini Morocco, mrembo Rima Edbouche mwaka jana, hivyo hata wakati wanacheza na Morocco alikuwa anacheza dhidi ya mashemeji zake.

Kama ilivyo kwa baadhi ya mastaa wengine hapo juu Dembele pia hajawahi kucheza timu yoyote ya vijana ya Maurtania.

Kylian Mbappe

Hapa ndipo Waafrika wanaumia sana kwa sababu baba wa jamaa aliwahi kuwasiliana na shirikisho la soka la Cameroon na kuwaambia mtoto wake anacheza mpira yupo Ufaransa lakini walikataa na inadaiwa walidai pesa ili wamuite kwenye timu ya taifa, wakati huo Mbappe alikuwa ndio kwanza kijana anachipukia.

Baba wa mshkaji huyu anatokea Cameroon na inadaiwa kuwa ana asili pia ya Nigeria, alizamia Ufaransa kwa ajili ya kutafuta maisha na huko akakutana na mama yake Mbappe ambaye ni raia wa Algeria.

Hivyo kwa haraka haraka asili ya Mbappe ni Cameroon na Algeria lakini hadi sasa bado hajachukua uraia wa nchi zozote kati ya hizo ameendelea kuwa na uraia wa Ufaransa pekee.

Randal Kolo Muani

Aliingia akitokea benchi kwenye mechi dhidi ya Morocco, na kuzamisha kabisa matumaini ya Morocco kwa kufunga bao la pili. Ana uraia pacha (Ufaransa na Congo), wazazi wake wote wamezaliwa Ufaransa lakini asili yao zaidi ilikuwa ni Congo ambako kuna baadhi ya ndugu zao wanaishi hadi leo.

Staa huyu anaripotiwa kutokea familia inayojiweza kidogo kiuchumi na kwenye Kombe la Dunia mwaka huu amecheza mechi mbili na kufunga bao moja.

WENGINE Axel Disasi (Congo), Matteo Guendouzi (Morocco), Youssouf Fofana (Mali), Steve Mandanda (DR Congo), William Saliba (Cameroon), Dayot Upamecano- (Guinea Bissau) na Eduardo Camavinga (Angola)/.

Chanzo: Mwanaspoti