Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika inatisha na kuteswa

Kindumbwe Afrika inatisha na kuteswa

Fri, 18 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hatimaye kindumbwendumbwe cha fainali za Kombe Dunia 2022 kinachojumuisha timu 32 zilizogawanywa katika makundi manane kinaanza Jumapili hii nchini Qatar kwa wenyeji kukutana na Equador.

Afrika inawakilishwa na Cameroon, Ghana, Morocco, Tunisia na Sengal na nchi zote hizi ziliwahi kushiriki fainali hizo miaka iliyopita. Cameroon ndio iliyoshiriki mara nyingi (nane) kuanzia 1982 na mara nne mfululizo kati ya 1990 na 2002 na kuwemo katika fainali za 2010, 2014 na za hivi sasa.

Ghana inashiriki kwa mara ya nne ambapo ilianza 2006, 2010, 2014 na 2022. Morocco inaiwakilisha Afrika mara ya sita kuanzia 1970, 1986, 1994, 1998, 2018 na 2022 na Tunisia imeingia fainali hizo kwa mara ya tano kuanzia 1978 na 1998, 2002, 2006 na 2018. Hata hivyo, Senegal inacheza kwa mara ya tatu kuanzia 2002, 2018 na hizi za 2022. Mashindano ya Kombe la Dunia yalifanyika kwa mara ya kwanza Uruguay 1930 na kushirikisha nchi 13 sita za Amerika Kusini, nne Ulaya na tatu Amerika Kaskazini.

Wenyeji Uruguay waliungana na Paraguay, Bolivia, Brazil, Peru, Mexico, Marekani, Chile na Argentina. Washiriki wengine walikuwa ni Yugoslavia, Ubelgiji, Romania na Ufaransa. Uruguay ilibeba kombe baada ya kuifunga Argentina 4-2.

Katika mashi-ndano ya pili yaliyofanyika Italia 1935 nchi 32 zilishiriki na 16 zilitinga hatua hiyo. Misri ilikuwa nchi pekee ya Afrika na ilitolewa baada ya kufungwa 4-2 na Hungary.

Wakati huo kulikuwa hakuna kundi la Afrika na Misri ilikata tiketi baada ya kupangwa kundi moja na Uturuki na Palestina, lakini Uturuki ilijitoa na Misri ilipata njia nyeupe baada ya kuifunga Palestina 7-1 katika mchezo wa kwanza jijini Cairo na 4-1 zilipokutana Jerusalemu, Palestina.

Hakuna nchi ya Afrika iliyoshiriki mashindano yalipoanza tena 1950 baada ya kusimama kutokana na Vita Kuu vya Pili vya Dunia vilivyoanza 1938 na kumalizika 1945. Misri ilikuwa mshiriki pekee kutoka Afrika mashindano ya 1954, lakini haikufuzu kuingia fainali baada ya kugombea tiketi na Italia na kufungwa 1-2 Cairo na 5-1 katika mchezo wa pili jijini Milan. Misri, Ethiopia na Sudan zilitaka kushiriki mashindano ya 1958, lakini Ethiopia ilikataliwa na Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (Fifa). Na Misri na Sudan zilizokuwa katika kundi la Afrika na Asia zilijitoa zilipopangwa kucheza na Israel.

Nafasi ya Afrika na Asia ilipewa Wales na uamuzi huo haukushangaza kwa sababu wakati ule Rais wa Fifa alikuwa Mwingereza, Stanley Rouse. Hakuna nchi ya Afrika iliyoshiriki fainali hizo hadi Morocco ilipocheza zile zilizofanyika Mexico 1970 baada ya kuitoa Tunisia kwa ushindi wa sarafu. Timu hizo zilitoka sare kwa pointi na mabao katika michezo mitatu iliyochezwa Morocco, Algeria na Italia.

Morocco ilifungwa 1-2 na Ujerumani, 3-0 na Peru na kutoka sare ya 1-1 na Bulgaria na Brazil ilibeba kombe kwa kuichapa Italia 4-1 katika fainali. Wakati nchi ya Afrika inayooongoza kushiriki mara nyingi fainali hizo ni Cameroon inayofuata ni Nigeria kwa kuingia mara sita, Algeria (4), Ivory Coast na Misri (3). Nchi zilizoingia mara moja ni Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Angola.

Hakuna nchi ya Afrika Mashariki iliyowahi kucheza fainali. Nchi ya kwanza Afrika kushinda hatua ya kwanza ya fainali hizo ni Tunisia 1978 walipokuwa katika kundi moja na Ujerumani Magharibi, Poland na Mexico. Katika mchezo wao na Mexico walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa wamefungwa bao 1-0, lakini walicharuka kipindi cha pili na kuibuka washindi kwa 3-1.

Katika mchezo wa pili na Poland walilala 1-0 na kwenda sare ya bila ya kufungana na Ujerumani, lakini hawakufanikiwa kusonga mbele kutokana na wastani mdogo wa mabao. Katika fainali za 1982 Algeria walishinda michezo miwili katika kundi lao ikiwa ni pamoja na kuwafunga mabingwa watetezi Ujerumani Magharibi mabao 2-1 na kuichapa Chile 3-2, lakini walifungwa 0-2 na Austria. Matokeo ya kupangwa ya mchezo wa mwisho yaliipa ushindi wa bao 1-0 Ujerumani ilipocheza na Austria na kuifanyaa Algeria na Chile kutupwa nje.

Mashabiki wa kandanda waliofika uwanjani siku ile walipiga kelele kulaaani na walitoka uwanjani mara kilipoanza kipindi cha pili kwa kuikataa aibu ile. Morocco ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuvuka hatua ya awali ya fainali za 1986 baada ya kutoka sare bila kufungana na Poland na kuzifunga England na Ureno. Katika mzunguko wa pili walitolewa na Ujerumani kwa bao pekee lililokuwa na utata na kuelezwa na vyombo vya habari kama zawadi aliyoporwa bwana mdogo na kupewa bwana mkubwa.

Cameroon walifanya maajabu 1990 na hasa walipowafunga mabingwa watetezi Argentina walioongozwa na Diego Maradona kwa bao 1-0. Katika mchezo huu Cameroon walibaki na wachezaji tisa katika dakika 20 za mwisho baada ya wawili kupewa kadi nyekundu ambazo hazikustahiki.

Roger Milla akiwa na umri wa miaka 38 alionyesha ujuzi hauzeeki kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wao wa mabao 3-1 walipokutana na Romania 2-1. Cameroon waliingia robo fainali na zikibaki dakika saba kukata tiketi ya nusu fanali, lakini England ilibebwa kwa kupewa penalti ya ajabu ili kuyafanya matokeo yawe 2-2. Mchezo ulipokwenda dakika za nyogenza huku England ikibebwa Cameroon ilijikuta ikifurushwa katika mashindano kwa kufungwa mabao 3-2.

Mwaka 1998 Nigeria ilikuwa nchi pekee ya Afrika kuingia mzunguko wa pili. Nchi nyingine zilizoiwakilisha Afrika zilikuwa ni Cameroon, Morocco, Tunisia na wenyeji wa mashindano - Afrika Kusini. Mashindano ya 2002 hayatasahaulika kwa Senegal kuonyesha kandanda safi na kufika robo fainali.

Katika fainali za 2004 zilizofanyika Brazil nchi za Algeria na Nigeria zilifuzu kwenda hatua ya pili ya mashindano, wakati Ghana na Cameroon hazikuwa na matokeo mazuri Ivory Coast walicheza vizuri, lakini penalti ya dakika ya mwisho ilipocheza na Ugiriki iliwafikifikisha mwisho wa safari. Awali Ivory Coast iliifunga Japan mabao 2-1.

Kwa ujumla nchi za Afrika hukumbwa na matatizo mengi katika fainali za Kombe la Dunia hii ni pamoja na yale ya kisiasa kama mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na uhaba wa fedha na hata kuwanyima wachezaji posho. Hata hivyo, nchi za Afrika zimeonyesha uwezo mkubwa ukitilia maanani huzifunga timu ngumu kama za Ujerumani, Argentina, Brazil na Ufaransa.

Kiwango ambacho wawakilishi wa Afrika walichoonyesha katika michezo ya karibuni kinatia moyo na kutoa matumaini ya kufanya vizuri katika fainali za Qatar. Matumaini ni mazuri, lakini wakati ukifika ndio tutapata jibu sahihi. Tusubiri.

Chanzo: Mwanaspoti