Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika ilivyofanya kweli Qatar 2022

Vincent Aboubakar 2 Vicent Abubakar

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar imefika tamati juzi Ijumaa na ilichokifanya timu za Afrika kwenye mikikimikiki hiyo, bravo!

Afrika iliyokuwa na wawakilishi watano kwenye fainali hizo, Senegal, Tunisia, Morocco, Cameroon na Ghana ambazo zilipangwa kwenye makundi A, D, F, G na H mtawalia. Miamba hiyo ya Afrika haijamaliza kinyonge fainali hizo za huko Qatar.

Hakika kilichotokea kwenye hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia 2022 kimeacha kumbukumbu ya kibabe kabisa.

Afrika imeshinda

Kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, timu zote tano za Afrika ziliweka unyonge pembeni na kila moja ikipata ushindi katika kundi lake. Wakati Senegal na Morocco zikitinga hatua ya 16 bora, miamba mingine mitatu ilimaliza kibabe hatua hiyo ya makundi, ikionyesha ushindi walau mechi moja kwenye mechi zao za makundi.

Utamu zaidi kwa Waafrika, katika hatua hiyo, timu za Senegal na Morocco zilishinda mechi mbili kwenye makundi yao, huku Tunisia, Cameroon na Ghana zikigawa vichapo kwenye mechi moja kati ya tatu walizocheza katika makundi hayo.

Katika fainali hizo za Qatar, timu ya Afrika iliyopata pointi chache ni Ghana, pointi tatu - lakini wababe wengine wote walivuna pointi nnne kwenye juu, huku Senegal ikivuna pointi sita na Morocco pointi saba na kuongoza Kundi F lililokuwa na nchi za Croatia, Ubelgiji na Canada.

Vigogo watulizwa kibabe

Wakati fainali za huko Qatar, mataifa makubwa kwenye soka kama Ufaransa, Brazil, Ubelgiji, Denmark hayakufua dafu mbele ya timu za Kiafrika kwenye mechi zao za hatua ya makundi, ambapo vigogo hao walikumbana na joto ya jiwe kwa kupangwa kundi moja na timu za Afrika.

Ufaransa ilichapa timu za mabara mengine, lakini ilipokipiga na Tunisia kwenye mechi yao ya mwisho ya hatua makundi, ilikutana na kichapo cha bao 1-0, kama ilivyoikuta Brazil katika mchezo wake mbele ya Cameroon, nayo ilipigwa 1-0. Ubelgiji na ubabe wake, ilishindwa kutamba mbele ya Morocco kwenye Kundi F, ikichapwa mabao 2-0 matokeo ambayo yalichagia kuitupa nje mapema Wabelgiji.

Cameroon yaacha rekodi Qatar

Katika mechi ya mwisho ya Kundi G, staa wa Simba Wasioshindika, Vincent Aboubakar aliifanya nchi yake ya kuandika rekodi ya kibabe kabisa katika fainali hizo za Qatar kwa kuwa taifa la kwanza la Afrika kupata ushindi dhidi ya Brazil kwenye mechi ya fainali za Kombe la Dunia.

Si jambo la kificho, ni timu chache sana zimewahi kupata ushindi mbele ya Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia na sasa miongoni mwa timu hizo ni Cameroon, ambapo bao la kichwa la mkwali wake, Aboubakar kwenye kipindi cha pili baada ya krosi matata ya Jerome Ngom Mbekeli ilitosha kutikisa nyavu za Brazil na kushinda 1-0 na kuondoka Qatar kibabe.

Hatua 16 wajipange

Kwa viwango bora kabisa vilivyoonyeshwa na timu za Kiafrika kwenye hatua ya makundi, ujumbe umetumwa sasa kwa wapinzani wao kwenye hatua ya mtoano ya 16 bora kwamba, hakutakuwa na mzaha kabisa unapokabiliana na miamba hiyo ya Afrika.

Afrika itarusha kete yake ya kwanza kwenye hatua hiyo ya mtoano, wakati Senegal itakapowakabili England leo Jumapili, kabla ya keshokutwa Jumanne kuwashuhudia Morocco wakifanya yao mbele ya Hispania. Bila shaka, England na Hispania zitaingia kwa tahadhali kwenye mechi zao dhidi ya timu za Afrika kutokana na makali ya timu hizo walizoonyesha kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Qatar.

Ni Kombe la Dunia la kweli

Fainali za Kombe la Dunia 2022 zimeleta ukweli na dhana halisi ya kuwa unaosakwa ni ubingwa wa dunia baada ya kushuhudia kwenye hatua ya 16 bora, mabara yote ya mpira yameingiza timu zao. Kwenye hatua hiyo ya 16 bora kuna timu za Amerika Kusini, Amerika Kaskazini, Asia, Afrika, Ulaya na Australia.

Lakini, kuonyesha kukua kwa mchezo wa soka katika pande mbalimbali za dunia, kumeshuhudia mataifa makubwa kama Ujerumani, Ubelgiji, Uruguay, Serbia, Denmark, Mexico yakitolewa mapema tu kwenye hatua ya makundi na kubakiwa kuwa washangiliaji.

Wakubwa wameumbuka

Achana na Ujerumani na Ubelgiji, mataifa makubwa kabisa kwenye soka walivyoumbuka na kutupwa nje ya fainali za Kombe la Dunia 2022 mapema tu kwenye hatua ya makundi, kuna vigogo wengine kama Hispania, Ufaransa, Argentina, Ureno na Brazil walikutana na aibu ya kuchapwa na mataifa madogo kabisa ambayo awali hayakudhaniwa.

Ilianza kwa Argentina kuduwazwa na Saudi Arabia kwa kichapo cha mabao 2-1, kabla ya Ufaransa kuchapwa na Tunisia 1-0, huku Ureno nayo ilikumbana na kipigo kutoka kwa Korea Kusini 2-1 na Brazil ilikumbana na kipigo kutoka kwa Cameroon 1-0. Ubelgiji nayo ilikumbana na kichapo kutoka kwa Morocco, mabao 2-0.

Afrika yafunga mabao 19 Qatar

Kwenye hatua ya makundi pekee, Afrika imeshuhudia mastaa wake wakifunga mabao 19 kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar. Masupastaa Mohammed Kudus wa Ghana na Vincent Aboubakar wa Cameroon, hao kila mmoja alifunga mara mbili, wakati wakali wengine waliofunga bao moja moja ni Abdelhamid Sabiri, Zakaria Aboukhlal, Hakim Ziyech na Youssef En-Nesyri waliopo kwenye kikosi cha Morocco, Jean-Charles Castelletto, Eric Maxim Choupo-Moting waliokuwa kwenye kikosi cha Cameroon, Wahbi Khazri wa Tunisia, Andre Ayew, Osman Bukari, Mohammed Salisu kwenye kikosi cha Ghana na Boulaye Dia, Famara Diedhiou, Bamba Dieng, Ismaila Sarr, Koulidou Koulibaly waliopo kwenye kikosi cha Senegal.

Chanzo: Mwanaspoti