Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika Kaskazini noma na nusu Ligi ya Mabingwa

Kaskazini Pic Data Al Ahly

Sun, 31 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Tuendelee kuangalia hatua za maendeleo ya mchezo wa soka kwa sababu siku zote ndicho kitu pekee kinachotafutwa katika sekta yoyote ile duniani, ingawa viashiria vya maendeleo hupishana kutokana mitazamo tofauti ya watu kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya wakati husika.

Ndio maana mtu mwenye kipato cha chini au cha kati anaweza kuona kuwa ameendelea kwa sababu anamiliki gari na mwingine anajitafsiri kuwa kapiga hatua kwa kuwa anamiliki nyumba ilhali wenye vipato vya juu na matajiri wanaona hawajaendelea kwa sababu hawajafikia malengo ndio maana wanafanya jitihada za kuwekeza katika kila sekta ili kupata maendeleo wanayotarajia.

Katika mchezo wa soka maendeleo huwa na tafsiri tofauti kwani ukimuuliza shabiki wa timu kama Simba au Yanga pale inapofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa atakuambia soka la Tanzania limeendelea, ndio maana unaona timu anayoshabikia inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Linapokuja suala la timu ya taifa kutofanya vizuri mashabiki wa klabu huona kama vile hawahusiki, wakati moja kati ya viashiria vya maendeleo ya soka kwa taifa ni pale timu ya taifa inapofanya vizuri katika mashindno ya kimataifa, hivyo kuwa na tafsiri tofauti anapoizungumzia timu anayoishabikia na timu yoyote ya taifa.

Kwa sasa tunaangalia kiashiria kingine muhimu ambacho ndicho kinatakiwa kutumika katika kupima maendeleo ya mchezo wa soka kwa taifa ambacho ni yale ya klabu kutoka katika ligi za mataifa mbalimbali kwenye mashindano ya kimataifa kama vile Ligi ya Mabingwa barani Afrika na Kombe la shirikisho ambalo kwa hapa kwetu katika msimu huu wa 2020/2021 tulipata nafasi ya kuwakilishwa na klabu za Simba, Yanga, Azam FC na Biashara United.

Klabu hizo ukiondoa Biashara ambayo hatima yake haijafahamika kutokana na mchezo wa pili wa marudiano na Al Ahly Tripoli kutochezwa hadi sasa, lakini zingine zilitolewa kizembe.

Ukiangalia kwa mtazamo huo utaona kuwa mataifa yaliyo katika ukanda wa Afrika Kaskazani bado yanaendelea kutawala soka la Afrika katika ngazi ya klabu na kuweka historia ya mafanikio kwa klabu, makocha na wachezaji wa timu za ukanda huo ambayo hutumika katika kuhamasisha vizazi vijavyo, hivyo kurahisisha maendeleo ya soka kwa mataifa hayo.

Tunaona, kwa mfano katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika klabu 16 zilizofanikiwa kuingia hatua ya makundi kwenye mashindano hayo, asilimia 50 ya zilizoingia zinatoka Afrika Kaskazini.

Ikumbukwe kuwa Shirikisho la Soka barani Afrika liliwagawa wanachama ambao ni mataifa kwa ukanda na kanda hizo kuwa na mashirikisho kama tunavyoona huu ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), wakati nchi za Afrika Mashariki shirikisho lao linajulikana kwa jina la Wafu-Ufoa ambao imegawanywa na kuwa na kanda mbili za Wafu ukanda A na Wafu ukanda B.

Mataifa yaliyo Kusini mwa Bara la Afrika shirikisho lao linajulikana kwa jina la Cosafa ilhali yale yaliyopo Afrika ya Kati yana shirikisho lao linalojulikana kifupi kama Uniffac, huku mataifa matano tu yaliyopo kwenye ukanda wa Afrika Kaskazini ambayo ni Algeria, Misri, Tunisia, Morocco na Libya shirikisho lao linatambuliwa kama Unaf.

Hivyo naweza kusema kuwa katika mashirikisho yote haya yanayogawanya kanda hizi za soka kwa Afrika, shirikisho la Unaf la nchi za Afrika Kaskazini ndilo limeonekana kuendelea kutawala mafanikio ya soka kwa Bara la Afrika kama tunavyoona leo hii asilimia 50 ya timu zilizoingia katika makundi zinatoka katika ukanda huo.

Kumbuka kuwa huo ni ukanda wenye mataifa matano tu hivyo kuwa na asilimia 50 ya uwezekano wa timu kutoka ukanda huo kuingia hatua ya robo fainali, nusu fainali na hata fainali kutokana na wingi wa klabu katika hatua hiyo.

Timu zilizoingia katika hatua ya 16 bora ni ES Setif na CR Belouzdad za Algeria, Al Ahly na Zamalek kutoka Misri, Esperance na Etoile Du Sahel za Tunisia, Raja Casablanca na Waydad Casablanca za Morocco na kuendelea kuthibitisha ubora wa soka kwa nchi za ukanda huo.

Ukanda mwingine ambao umefuatiwa kwa kuwa na wawakilishi wengi katika hatua ya timu 16 bora ni ule wa Cosafa ambao umetoa timu tano ambazo ni Mamelodi Sundowns na Amazulu za Afrika Kusini, Petro Atletico na Sagrada Esperanca za Angola na Jwaneng Galaxy kutoka Botswana na kuufanya kuwa na uwakilishi wa asilimia 31.25.

Wakati ukanda wetu wa Cecafa tumefanikiwa kuwa na timu mbili tu katika hatua hiyo ambazo ni Al Merrikh na Al Hilal zote kutoka nchini Sudan, hivyo kuwa na uwakilishi wa asilimia 12.5 na mwisho kabisa ni ukanda wa Wafu ambao una timu moja tu - Horoya FC kutoka nchini Guinea, hivyo kuwa na asilimia 6.25 ya uwakilishi licha ya wingi wa mataifa yaliyopo katika ukanda huo ambapo kuna mataifa 16 kutoka eneo la Magharibi A na B.

Hivyo kwa kuwa ubora wa ligi hupimwa kwa klabu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa kufanya vizuri katika mshindano hayo, bado ligi za mataifa yaliyo Afrika Kaskazini zinaendelea kuthibitisha ubora wake, huku kanda nyingine zikiendelea kugawana nafasi za chini lakini bila kusahau nchi ya Afrika Kusini pia ambayo kwa miaka ya hivi karibuni zimeonekana kuendelea kuubeba ukanda mzima wa Cosafa unaojumuisha mataifa 14 kwa klabu kutoka nchi hiyo kufanya vizuri, huku ukanda Cecafa tukibebwa na timu mbili.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz