Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afrika Kaskazini ilivyojenga utawala wake AFCON

Tanzania Morocco.jpeg Afrika Kaskazini ilivyojenga utawala wake AFCON

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), 2023 zinaendelea huko Ivory Coast na sasa zinakaribia kumaliza raundi ya pili ya hatua ya makundi kabla ya kuanza kwa raundi ya tatu na ya mwisho.

Haya hapana shaka ndiyo mashindano makubwa na yenye mvuto na thamani zaidi kulinganisha na mengine yote ya soka barani Afrika na ndio maana yamekuwa yakifuatiliwa kwa ukaribu na pande zote za dunia.

Matokeo ya mechi za mwanzoni za mashindano hayo mwaka huu yameonyesha ishara kwamba safari hii yatakuwa na ushindani na mvuto wa hali ya juu pengine kulinganisha na awamu zilizopita.

Mashindano hayo yalianzishwa mwaka 1957 na hii ni awamu ya 34 tangu yalipoanza kufanyika na huchezwa kila baada ya kipindi cha miaka miwili.

Katika kipindi cha miaka 67 ambayo fainali hizo zimefanyika, ukanda wa Kaskazini mwa Afrika umekuwa mtemi wa Afcon kutokana na mafanikio ilizopata timu zake kila zinaposhiriki.

Wakati fainali za Afcon zikiendelea huko Ivory Coast, Spoti Mikiki inakuletea tathmini ya ubabe wa kanda ya umoja wa vyama vya mpira wa miguu Kaskazini mwa Afrika (Unaf) pindi timu zake zinaposhiriki Afcon.

Uandaaji

Sio jambo rahisi kwa nchi kupata uenyeji wa fainali za Afcon na ili ifanikiwe kupata fursa hiyo inapaswa kutimiza vigezo vingi ambavyo ndio vimewekwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) kwa ajili ya uandaaji wake.

Miongoni mwa vigezo hivyo ni nchi kuwa na angalau viwanja sita vinavyokidhi vigezo vya kutumika kwa mechi za kimataifa, pia usalama, huduma nzuri za malazi na kadhalika.

Lakini pamoja na ugumu wa kupata uenyeji wa fainali hizo, Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika umekuwa na urahisi kwa kuongoza kuandaa mara nyingi Afcon kulinganisha na kanda nyingine.

Historia inaonyesha katika awamu 34 za kufanyika kwa mashindano hayo, Kanda ya Kaskazini imepata fursa ya kuandaa mara 11, ikifuatiwa na kanda ya Magharibi (Wafu) iliyoandaa fainali hizo mara 10 huku kanda inayoshika nafasi ya tatu ni ile ya kati (Uniffac) na ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambazo kila moja imeandaa mara tano.

Kanda ambayo imeandaa mara chache zaidi fainali hizo ni ile ya Kusini (Cosafa) ambayo imeshuhudia ikiwa mwenyeji mara tatu tu.

Misri ndio nchi ambayo imeibeba zaidi kanda ya Kaskazini kwani ndio imeandaa mara nyingi zaidi fainali hizo ikifanya hivyo mara tano, Tunisia ikiandaa mara tatu huku Libya, Algeria na Morocco kila ikiandaa mara mojamoja.

Kutwaa mataji

Kanda ya Kaskazini mwa Afrika haijaishia kuonyesha umwamba wake katika kuandaa fainali za Afcon bali pia hata katika mafanikio ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Idadi ya mataji 11 ya Afcon yametwaliwa na timu kutoka Kaskazini mwa Afrika na ukanda unaofuatia ni ule wa Wafu ambao timu zake kiujumla zimetwaa taji mara tisa huku kanda ya Uniffac ikichukua kiujumla ubingwa mara nane.

Cosafa na Cecafa ndio kanda zenye unyonge zaidi katika vita ya kuwania taji la Afcon kwani kila moja, imebeba ubingwa wa mashindano hayo mara mbili tu katika nyakati tofauti.

Kama ilivyo kwenye uandaaji wa Afcon ndicho kilichotokea katika kutwaa mataji kwani Misri ndio timu iliyoutoa kimasomaso ukanda huo kwa kutwaa idadi kubwa ya mataji sio tu kwa Unaf bali pia Afrika nzima.

Mafarao hao wa Misri imetwaa ubingwa wa Afcon mara saba tofauti wakifanya hivyo mwaka 1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010 huku ikifuatiwa na Algeria ambayo imetwaa ubingwa mara mbili huku Morocco na Tunisia kila moja ikiwa imetwaa ubingwa mara moja moja.

Kwa upande wa kanda ya Wafu ambayo inashika nafasi ya pili kwa kutwaa mara nyingi taji la Afcon ikifanya hivyo mara 10, timu kinara ni Ghana iliyotwaa mara nne, ikifuatiwa na Nigeria iliyobeba taji hilo mara tatu, Ivory Coast ikichukua mara mbili na Senegal imechukua mara moja.

Kanda ya Uniffac ambayo imetwaa taji hilo mara nane, imebebwa zaidi na Cameroon ambayo imechukua ubingwa mara tano, DR Congo ikitwaa mara mbili na Congo ikiambulia taji mara moja.

Cecafa na Cosafa kila moja imetwaa ubingwa mara mbili, ambapo Afrika Kusini na Zambia zimefanya hivyo mara moja moja kwa Cosafa kama ilivyo kwa Sudan na Ethiopia upande wa Cecafa.

Tuzo mchezaji bora

Tangu fainali za Afcon zifanyike kwa mara ya kwanza mwaka 1957 hadi sasa, tuzo ya mchezaji bora wa mashindano imeenda mara nyingi Afrika Kaskazini sawa na idadi ambayo imebebwa na wachezaji wa Afrika Magharibi.

Kanda ya Kaskazini na Magharibi kila moja imefanikiwa kunyakua tuzo ya mchezaji bora wa mashindano mara 10, zikifuatiwa na kanda ya Uniffac ambayo imebeba mara tisa, kanda ya kusini ikifanya hivyo mara tatu na kanda ya Afrika Mashariki na Kati ikiondoka nayo mara moja.

Chanzo: Mwanaspoti