Mabingwa wa zamani wa Tanzania, African Sports 'Wanakimanumanu' ya Tanga wametinga 16 Bora ya Kombe la Shirikisho (ASFC), huku wakisema Simba ijipange kwani mechi kubwa ndio zao na wanataka kurudisha heshima yao ya miaka ya nyuma pamoja na kujiweka vizuri kwa Championship.
Timu hiyo imetinga hatua hiyo baada ya juzi kuifunga New Dundee United ya Dodoma kwa penalti 4-2 mara baada ya dakika 90 timu hizo kutoka suluhu katika mtanange uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Jijini hapa.
Katika mchezo huo New Dundee itabidi wajilaumu kutokana na kupoteza nafasi nyingi ndani ya dakika 90 zilizokoswa na washambuliaji Jammy Simba, Ibrahim Nyoka na Hamis Rajab.
Sports itakutana na Simba kati ya Machi 3-5 mwaka huu baada ya juzi Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Tangu michuano hiyo imeanza kuchezwa mwaka 1967, ikifahamika FAT na sasa ASFC, Yanga ndio timu iliyobeba taji mara nyingi zaidi mara sita.
Sports iliyowahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Muungano mwaka 1988, huku watani wao Coastal wakibeba taji la Ligi Kuu Bara, kwa sasa inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Championship ikiwa na pointi 18 baada ya mechi 16, ikishinda tano, ikipoteza nane na kupata sare mitatu.
Kocha wa timu hiyo, Mussa Rashid alisema wanafurahi kupata ushindi huo na sasa wanajipanga kwa ajili ya kukutana na Mnyama.
"Tunataka kurudisha heshima yetu sisi mechi kubwa ndio zetu kutokana na historia yetu, tumeyumba kidogo baada ya wachezaji wetu kadhaa kuondoka lakini sasa hivi kidogo kidogo tunarudi," alisema kocha huyo.
Akiuzungumzia mchezo dhidi ya New Dundee United alisema ulikuwa mgumu na wapinzani wao walikuwa bora katika kila idara.
"Hawa Dundee wana timu lakini walikosa maarifa nilijua nakuja kucheza na timu ya mtaani lakini nilichokutana nacho ni tofauti kabisa wamecheza vizuriĀ lakini ndio hivyo uzoefu imetubeba na wao wameshindwa kumaliza kazi mapema,"alisema kocha huyo.
Kocha wa Dundee United, Athuman Hussein alisema wamecheza katika kiwango bora lakini bahati haikuwa kwao.
"One against one tulipata tatu mtu akiwa na kipa lakini tumekosa, tumemia kupoteza mchezo huu hii ilikuwa fursa kwa vijana wangu kuonesha uwezo wao lakini tumetolewa kikatili sana kila mtu ameumia, tunajipanga na tunasonga mbele ila kwa maumivu makubwa," alisema kocha huyo.