Taarifa za Mbwana Samatta kustaafu timu ya taifa ‘Taifa Stars’ zilianza kama utani na baadaye ikaja kubainika kuwa ni kweli nahodha huyo amestaafu.
Haijabainika wazi sababu ambazo Samatta anayechezea PAOK ya Ugiriki amezitaja za kuchangia uamuzi huo wa kuiacha Taifa Stars lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limethibitisha kuwa ni kweli wana barua ya Samatta mezani.
Hata hivyo, jambo la kufurahisha ni kuona TFF imeamua kutokubali uamuzi huo wa Samatta kwa sasa na umepanga kukutana naye ili kuona ni kwa namna gani litazungumza naye ili atengue uamuzi huo
TFF imefanya jambo sahihi kwani Samatta ni mchezaji mwenye heshima kubwa katika hii nchi na hapaswi kuiacha Taifa Stars kirahisi kama ambavyo anataka kufanya hivi sasa.
Yeye ndie mchezaji mwenye jina kubwa kikosini na uwepo wake kwenye timu una maana kubwa sana kwenye kikosi hasa katika vyumba vya kubadilishia nguo katika kuwajenga kiukomavu na kuwahamasisha wachezaji wenzake.
Ni mchezaji ambaye amecheza katika mashindano yote makubwa Ulaya na ametwaa mataji katika Ligi Kuu mbili tofauti barani humo na akiwa hasotei benchi huku akishiriki hata kwa kufunga mabao.
Haikutakiwa kumruhusu astaafu katika kipindi hiki ambacho mshambuliaji mwingine mwandamizi kikosini, John Bocco ametundika daruga na sasa amejikita katika ukocha wa vijana.
Kwa bahati ni kipindi ambacho taifa halijawa na straika mzawa ambaye ameweza kufikia daraja la ubora la ama Bocco au Samatta ambaye pengine angefanya watu tuwe na uhakika kuwa viatu vya nahodha vitavaliwa vyema.
Mchezaji anapoichezea timu ya taifa anakuwa ni mali ya nchi hivyo TFF imefanya jambo la mbolea kutomkubalia Samatta kile anachotaka kukifanya kwa sasa.