Wahenga walisema panapofukia moshi, pana moto chini. Methali hii unaweza kuitumia kuelezea kinachojiri ndani ya Simba katika siku za hivi karibuni.
Ndani ya Simba kwa sasa mambo hayajakaa sawa na ni lazima juhudi kubwa zifanywe na uongozi pamoja na wanachama wa timu hiyo kutuliza hali ya hewa ili kuinusuru timu na kuirudisha katika makali yake yaliyozoeleka ambayo kwa siku za hivi karibuni hayapo kutokana na mwenendo wa timu hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini uwepo wa matatizo na changamoto nyingi ambazo kwa kiasi kikubwa yamechangia kuiweka timu hiyo katika uwezekano mgumu wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu lakini pia kutimiza lengo lake la kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo kwa sasa wapo katika hatua ya makundi.
Nidhamu mbovu, makundi kwa wachezaji
Uongozi wa Simba pamoja na benchi la ufundi la timu hiyo kwa sasa umekuwa ukifanya kazi kubwa ya kutibu tatizo sugu la utovu wa nidhamu ambalo linaonekana kushika kasi kikosini siku hadi siku lakini pia kuvunja makundi ambayo yamewekwa na wachezaji wa timu hiyo jambo ambalo baadhi ya nyakati limekuwa likiathiri mwenendo wa timu kwenye mashindano inayoshiriki.
Idadi kubwa ya wachezaji ambao wamekuwa vinara wa utovu wa nidhamu ni wale ambao wanajiona ni vipenzi vya mashabiki na viongozi wa timu hiyo wanaoamini hawawezi kuchukuliwa hatua yoyote na timu au pindi wakichukuliwa hatua wanaamini watapata utetezi mkubwa kutoka kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.
Mfano wa kesi ambayo ni ishara tosha ya kuonyesha namna tatizo la utovu wa nidhamu limekithiri kwenye kikosi cha Simba ni mchezaji mmoja wa kigeni wa timu hiyo ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa akigomea kutumia usafiri wa ndege akidai huwa hajisikii vizuri pindi anaposafiri kwa kutumia usafiri huo pasipo uthibitisho maalum wa daktari wa Simba.
Hilo limepelekea nyota huyo kutoitumikia Simba katika michezo mingi ambayo imekuwa ikicheza nje ya Dar es Salaam ambako huwa inalazimika kusafiri kwa ndege au baadhi ya safai za nje ya nchi huku mara nyingi taarifa ambazo hutolewa kuhusu yeye zimekuwa zikisema kuwa ni mgonjwa ingawa kiuhalisia huwa haumwi.
“Wakati mwingine mnaweza kuona viongozi na watu wa benchi la ufundi tuna chuki na wachezaji lakini katika mazingira kama hayo unafanyaje ndugu yangu? Huyu ni mchezaji wa kigeni ambaye klabu inatumia gharama kubwa kumhudumia lakini hataki kwenda mechi za nje akidai hawezi kusafiri kwa ndege, je aliwezaje kufika hapa nchini kutoka huko kwao,” alihoji mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakupendwa kutajwa jina lake.
Lakini taarifa kutoka ndani ya kambi ya Simba zinafichua kuwa mchezaji huyo amekuwa kinara wa ulevi jambo ambalo limeathiri hata mahudhurio yake mazoezini.
Ukiondoa huyo, yupo mchezaji mwingine mzawa ambaye mara kwa mara amekuwa akishindwa kutokea mazoezini pasipo sababu ya kueleweka jambo ambalo limepelekea benchi la ufundi kutompatia nafasi ya kucheza kikosini.
Hata hivyo, kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda alisema kuwa wachezaji ambao hawapati nafasi za kucheza ni kwa sababu za majeraha, ugonjwa au sababu za kiufundi.
“Suala la utovu wa nidhamu halipo na kama kungekuwa na mchezaji mtovu wa nidhamu angekuwa ameshachukuliwa hatua. Suala la kutocheza kwa baadhi ya wachezaji mara nyingi ni kwa sababu ya majeruhi na wengine ni kwa sababu ya aina ya mechi lakini timu iko shwari na hakuna tatizo lolote,” alisisitiza Mgunda.
Mpasuko wa viongozi, wanachama
Uchaguzi uliofanywa na Simba, Januari 29 mwaka huu unaonekana kuacha mpasuko mkubwa kwa baadhi ya vigogo wa timu hiyo, wanachama na mashabiki jambo ambalo limesababisha umoja ambao umekuwa silaha kwa timu hiyo kufanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni kutetereka.
Katika uchaguzi huo, Murtaza Mangungu aliibuka mshindi katika nafasi ya uenyekiti akimpiku, Moses Kaluwa huku wanachama Issah Masoud, Selemani Haroub, Asha Baraka, Seif Ramadhan Muba na Rodney Chiduo wakishinda nafasi za ujumbe wa bodi ya wakurugenzi.
Kumekuwa na upande ambao unauunga mkono uongozi uliopo madarakani na upo upande ambao unaonekana kutokuwa tayari kuunga mkono ule ambao unaiongoza klabu hiyo kwa sasa.
Hilo limesababisha kutuhumiana kwa pande hizo - kila mmoja ukidai mwingine unaihujumu timu katika mechi mbalimbali.
Hivi karibuni, wanachama takribani 100 wa klabu hiyo waliitisha mkutano wa waandishi wa habari ambapo waliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuchunguza uchaguzi mkuu huo wa Simba wa Januari 29 wakidai uligubikwa na matendo ya rushwa.
“Ndio maana tumeamua kulifanya hili mwezi huu. Kikatiba tuko ndani ya wakati kwa sababu haitukatazi kudai haki yetu wakati wowote. Wako watu zaidi ya 2000 ambao wanaliunga mkono hili kwa sababu tunataka klabu yetu iendeshwe katika utaratibu na mwekezaji aone faida ya kuwekeza kwake,” alisema mwenyekiti wa matawi ya Simba, Dar es Salaam, Hamis Suleiman.
Mwanachama mwingine wa klabu hiyo, DK. Mohamed Wandwi alisema kuwa timu hiyo inafanya vibaya kwa sababu ya uongozi.
“Matokeo ya kufanya vibaya Simba, ni matokeo ya kuwa na uongozi usiokubalika na watu wengi, ndio maana Simba haifanyi vizuri. Malalamiko yote yanaenda kwa uongozi. Usajili umekuwa ni wa ovyo. Wachezaji wanaosajiliwa kutoka nje, ukiangalia viwango vyao wanazidiwa hadi na wale wa Dodoma Jiji. Tumeshuka kiwango,” alisema Dk. Wandwi.
Ofisa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally hata hivyo alikanusha taarifa za kuwepo kwa migogoro na mpasuko ndani ya klabu na kuwataka wanachama na mashabiki wa Simba kuwa watulivu.
“Simba kauli mbiu yetu ni ‘Nguvu Moja’. Wanasimba tutemmbee na kauli hii. Kama kuna kasoro au tatizo lolote, uongozi upo na zipo taratibu za kufikisha na kufanyiwa kazi. Bado tupo kwenye mstari sahihi na tukiwa pamoja tutaweza kutimiza malengo yetu. Simba ni moja na hakuna mgogoro wowote, wanaotoa hizo taarifa kuwa kuna mgogoro nia yao ni kutuvuruga tu na hawaitakii mema timu yetu,” alisema Ahmed Ally.
Ufanisi duni wa wachezaji
Kundi kubwa la wachezaji wa timun hiyo limekuwa halitoi mchango chanya kutokana na sababu mbalimbali ambazo nyingine zinaepukika na nyingine zikiwa ni zile zisizoepukika.
Wapo baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa wakishindwa kuitumikia kikamilifu timu hiyo kutokana na majeraha, wengine viwango duni na wapo ambao wanashindwa kuisaidia timu kutokana na utovu wa nidhamu.
Wadau watoa neno
Nyota wa zamani wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ alisema kuwa wanachama na mashabiki wa Simba wanapaswa kuwa watulivu kwani ndio silaha ya kufanya vizuri.
“Mimi ninachokiona ni kwamba mashabiki na wanachama wanaipa presha kubwa timu jambo linalofanya wachezaji wakose utulivu nan kushindwa kutoa mchango wao uwanjani. Ninachoshauri ni wawe nyuma ya timu na waiunge mkono mambo yatakaa sawa tu,” alisema Mgosi.
Beki za zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa alishauri kuwepo na umoja ndani ya klabu.
“Kuna usemi unasema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Kama kuna tofauti zozote zilizojitokeza wanapaswa kukaa pamoja na kuzimaliza ili timu iendelee kufanya vyema,” alisema Pawasa.