Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adam Adam ajiweka Top 5 ya wafungaji Ligi Kuu

Adama Adam Mashujaa Adam Adam ajiweka Top 5 ya wafungaji Ligi Kuu

Tue, 2 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mshambuliaji wa Mashujaa Adam Adam, anajipigia hesabu ya kumaliza katika nafasi tano za juu kwenye chati ya wafungaji wenye mabao mengi kwa msimu huu, jambo linalomfurahisha zaidi ni ushindani wa wazawa kwenye kucheka na nyavu.

Hadi sasa Adam amefunga mabao saba, jambo linalompa ari ya kuamini ndoto zake lazima zitatimia na anajiongeza kwa mazoezi yake binafsi nje na ya timu, ili kuhakikisha anakuwa fiti.

Mahojiano yake na Spoti Mikiki, Adam anasema mabao saba anayomiliki kafunga dhidi ya Kagera Sugar, Ihefu, Singida Fountain Gate, Mtibwa Sugar, KMC, Geita na Namungo FC na mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) .

“Ni imani yangu msimu huu utakuwa wa mafanikio makubwa, nahitaji niwe kwenye ‘Top 5’ ya wafungaji wenye mabao mengi, hilo linawezekana na nitapambana hadi niishi kwenye ndoto zangu,”anasema na kuongeza;

“Kitu kingine ninachokifurahia ni kuona wazawa wengi wana mabao mengi na kuna ushindani wa kutosha, Feisal Salum ‘Fei Toto’, (mabao 13), Wazir Junior (mabao 11), Samson Mbangula (mabao manane), Mudathir Yahya (mabao manane) na mimi nina saba, naamini wataongezeka na wengine.”

Anasema ile zana ya washambuliaji wazawa ni kama wasindikizaji wa wageni kuwania kiatu cha ufungaji inapotea

“Alianza kukichukua John Bocco msimu wa 2020/21 akimaliza na mabao 16, akaja George Mpole akiwa Geita Gold 2021/22, alimaliza na mabao 17, msimu uliopita wakachukua wageni ambao ni Fiston Mayele na Said Ntibanzokiza ‘Saido’, awamu hii ni zamu yetu, Wazir na Fei Toto wanatakiwa kukaza zaidi.

“Pamoja na malengo yake ya kufunga mabao mengi, anaitanguliza Mashujaa kwanza kuhakikisha haishuki daraja. ”Hatupo kwenye nafasi nzuri, tunahitaji kupambana kwa pamoja, kisha malengo ya mtu binafsi yatakuja baadaye,” alisema Adam.

Mbali na hilo, anaitaja rekodi Bocco ya mabao aliyofunga Ligi Kuu Bara, jinsi inavyompa ari ya kujituma, ili na yeye angalau afanye kitu ambacho atakuja kuwasimulia watoto wake.

DATA ZA BOCCO AKIWA AZAM FC

2008/09 - bao 1

2009/10 - mabao 14

2010/11 - mabao 12

2011/12 - mabao 19

2012/13 - mabao 7

2013/14 - mabao 7

2014/15 - mabao 2

2015/16 - mabao 12

2016/17- mabao 10

Jumla: Mabao 84

BOCCO AKIWA NA SIMBA SC

2017/18 (mabao 14), 2018/19 (mabao 16), 2019/20 (mabao 9), 2020/21 (mabao 16), 2021/22 (mabao 3), 2022/23 (mabao 10), 2023/2024 (mabao 2), hivyo hadi sasa ana jumla ya mabao 70, ukijumuisha na ya Azam ni 154.

“Kajiwekea rekodi ya heshima, kama mshambuliaji natamani kufanya kitu kama chake, natamani niandike iwe nitafikia mabao yake ama siyafikii ila niwe na kitu cha kuwaambia wanangu nilicheza soka la mafanikio,”anasema Adam ambaye nje na soka analima na kufuga.

ALAMA YA MAUMIVU

Msimu wa 2018/19, Mei 28 Adam alivunjika mkono baada ya kuisaidia Tanzania Prisons kusalia Ligi Kuu Bara, alifunga mabao mawili, timu ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Lipuli, ilikuaje anasimulia.

“Wakati nakwenda kufunga niligongana na kipa wa Lipuli dakika ya 85, nilidondoka chini na mkono wangu wa kulia ulipinda palepale, nakumbuka sikunyanyuka tena, nilibebwa hadi hospitali ya Keizi ipo maeneo ya Mafyati Mkoani Mbeya, nikafanyiwa upasuaji ndipo nikakaa sawa,” anasema na anaongeza;

“Tukio hilo linanifanya nisisahau dakika, tarehe, siku na mwaka, kiukweli kabla sijafanyiwa upasuaji nilikuwa naangalia mkono wangu hadi naogopa, nakumbuka msimu huu nilimaliza na mabao 11, ambapo 10 nilifunga nikiwa na Prisons na moja nilitoka nalo African Lyon ambako nilicheza miezi sita.”

Msimu uliofuata (2019/20) Adam alijiunga na JKT Tanzania na alimaliza na mabao 9, japokuwa anasema hakucheza mechi zaidi ya 10 kutokana na kusumbuliwa na majeraha na msimu uliofuata alimaliza na saba, kisha akaenda nje baada ya kurejea akajiunga na Polisi Tanzania akafunga mabao mawili, Mtibwa Sugar na Ihefu msimu mmoja nikafunga mabao matano.”.

“Ndani ya misimu mitatu mfululizo kiwango changu kilikuwa kizuri, nadhani ndicho kilichangia niitwe Stars, japokuwa wengi wanadhani ni kwasababu ya hat-trick niliyofunga dhidi ya Mwadui, timu yangu ikishinda mabao 6-1, lakini pia nilifunga mabao mawili na Namungo,” anasema.

KUCHEZA NJE

“Niliwahi kusaini Al Etihad Tripoli ya Libya, lakini wakanitoa kwa mkopo Al Wahda FC, pamoja na hayo yote nilijifunza vitu vya kiufundi na namna wenzetu ambavyo wapo mbali kwa miundo mbinu,” anasema.

STARS IMEMPA HESHIMA

Anasimulia baada ya kuitwa Taifa Stars chini ya aliyekuwa kocha Etienne Ndayiragije, kwamba ilimjengea heshima mtaani, ambako awali alionekana si chochote na aliwahi kukatishwa tamaa na watu kwamba hatafika popote na kazi ya soka.

“Baada ya kuitwa Stars niliona heshima inarejea na sasa wananisapoti, timu yangu ikicheza wanasema tunakuangalia, umecheza vizuri na kama nimecheza vibaya wananiambia,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti