Adhabu ya Kadi Nyekundu iliyomuangukia Beki wa Kulia wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain Achraf Hakimi wakati wa mchezo wa Ligi Kuu mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Lorient, imemkera Meneja wa Miamba hiyo ya jijini Paris Christophe Galtier.
Mabingwa hao wa Ligue 1 waliteleza kwa kichapo cha mabao 3-1 baada ya kumpoteza Hakimi ndani ya dakika 20 za kwanza kwa kosa la pili la kadi ya njano.
Kupoteza huko kunaiacha PSG ikiwa bado inaongoza kwa alama tano kwenye msimamo wa ligi baada ya wapinzani wao Marseille kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Auxerre siku ya Jumapili (Aprili 30).
Akitafakari nyekundu ya Hakimi, ambayo ilikuja baada ya kuwafanyia madhambi Romain Faivre na Darlin Yongwa, Galtier amekiri kukerwa na tukio la mchezaji huyo
“Hakukuwa na sababu kwa Achraf kufanya kosa kama lile, yaani ilikua kadi ya kijinga sana,” amesema Meneja huyo
“Kadi ya pili ni ya kijinga sana. Hakukuwa na dalili wiki hii kwamba tutakuwa na wasiwasi.
“Inasikitisha sana, na inabidi tuchukue hatua haraka kwa sababu hatujui ni alama ngapi tutakuwa nazo. Nusu yetu ya pili ya msimu imekuwa mbaya sana.”
“Kuna haja ya kuwa na umoja lakini pia mwamko wa mtu binafsi. Wachezaji wengi sana wanaangalia ndani. Lazima tuangalie mbele.”
“Mchezo dhidi ya Troyes unakuja. Tumekuwa wa kwanza tangu kuanza kwa michuano, lakini tunapaswa kumaliza na ushindi. Tuna nia ya kufanya zaidi.”