Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Acheni masihara! Derby haizoeleki

Yanga Vs Simba FT Derby haizoeleki

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Makocha na wachezaji waliowahi kuzitumikia Simba na Yanga, wanaitazama dabi ya Aprili 16 kwamba itaamuliwa na mbinu, nidhamu na utalivu kutokana na ubora wa vikosi hivyo kwa sasa.

Kipa wa Namungo FC, Deogratius Munishi 'Dida' ambaye alizichezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti alisema;

"Ni mechi inayoweza ikampa thamani mchezaji ama ikamshusha, ila mimi ninayoikumbuka ni ile ya msimu wa 2015/16 nikiwa Yanga tuliifunga Simba nje, ndani kuhusu dabi ya Aprili 16 itaamuliwa na mbinu zaidi vikosi vyote vipo sawa."

Beki wa zamani wa Yanga, Adeyum Saleh ambaye kwa sasa anakipiga Dodoma Jiji, alisema; "Tutaona ufundi zaidi na ushindani, maana timu hizo zina wachezaji wazuri ingawa naipa nafasi Yanga ya kushinda mechi hiyo."

Kocha wa zamani wa Simba SC, Dylan Kerr anaamini kuwa; "Kiukweli hii ni kati ya dabi ambazo navutiwa nazo, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinabahati ya kuwa na mashabiki ambao wanapenda sana mpira, msisimko wa dabi huwa mkubwa sana naongelea kitu ambacho nakijua, nimefuatilia mwenendo wa timu zote mbili lakini natoa nafasi kwa Simba."

George Lwandamina ambaye alifanya makubwa akiwa na Yanga, alisema itakuwa mechi ngumu sana kwa sababu timu zote mbili zipo kwenye viwango bora ndio maana wametinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa hilo sio jambo dogo.

"Ni ngumu kusema nani anaweza kushinda lakini atakayekuwa amejiandaa vizuri zaidi na kuwa bora kimbinu anaweza kufanya vizuri, natamani ningeishuhudia hiyo mechi lakini nakabiliwa na majukumu mengi ya kufanya," alisema Lwandamina.

Upande wake, kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael ambaye kwa sasa yupo kwao Ubelgiji, amewatakia kila la kheri mashabiki wa soka la Tanzania kuufurahia mchezo huo, hakutaka kuuelezea kiundani kutokana na kile ambacho kinaendelea na waajiri wake hao wa zamani.

"Siku zote dabi huwa mchezo spesho sana, huwa na msisimko wa aina yake, kwangu huu mchezo nilikuwa nikiuchukulia kama sherehe nyingine kubwa," alisema kocha huyo.

Ukiachana na makocha hao, mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali alisema Dabi hiyo inakosa ufundi na kutawalia na rafu, kadi, kupaniana kutokana na presha wanayoipata nje ya uwanja.

"Ni mara chache kuona utulivu, ushindani wa burudani, kwasababu wachezaji akili zao zinakuwa zimepata presha ya nje ya uwanja, pamoja na hayo yote ni mechi ijayo ni ngumu, naamini kikosi cha Simba kitawapa raha mashabiki wake," alisema.

Chanzo: Mwanaspoti