Nje na soka kuna wachezaji wana elimu kubwa zitakazowawezesha kufanya kazi nyingine pindi watakapoamua kutundika daruga.
Mwanaspoti inakuchambulia baadhi yao ambao wakiamua kuachana na soka wana uwezo wa kurejea kuzifanya kazi kwa taaluma zao.
Yannick Bangala-Azam
Kiungo mkabaji wa Azam FC, Yannick Bangala nje na ufundi wake uwanjani jamaa alisomea udaktari nchini kwao DR Congo.
Aliwahi kufunguka hilo wakati anafanya mahojiano na Mwanaspoti, ingawa hilo hakulifafanua sana akisema: "Nje na soka nimesomea udaktari naweza nikasaidia mtu akipata dharula."
Victor Akpan -Ihefu
Kiungo wa kati wa Ihefu, Victor Akpan nje na soka ana shahada ya uhandisi. Mwenyewe anasema: "Nimetokea familia ya kisomi na haikuwa rahisi kucheza soka. Wazazi wangu walipenda niendelee na elimu zaidi, hivyo nikistaafu soka nitaifanyia kazi taaluma yangu."
Mussa Mbise-Prisons
Kipa wa Tanzania Prisons, Mussa Mbise nje ya uwanja ana taaluma ya utabibu ngazi ya diploma aliyosoma kwenye Chuo cha COTC kilichopo Sengerema (2013-2015).
"Kilichonifanya nihamie kwenye soka mzazi wangu aligharamikia kunisomesha halafu nikawa najitolea, nikaipa nguvu plani B ambayo ni soka," anasema.
Pia aliwahi kuwa padri na alikuwa na lengo la kutumikia kanisa, lakini baadaye alighairi na anatoa sababu ya maamuzi hayo.
"Nilijiunga na masomo ya upadri mwaka 2012, ila sikumaliza mwaka kutokana na mambo ya familia," anasema.
Anapoulizwa wapo mahusiano siyo moja ya sababu ya kufanya aghairi upadri? Anajibu: "Hapana sikuwa na mawazo hayo kabisa. Moyoni mwangu kulijaa mambo ya Mungu pekee."
Ayoub Semtawa-Mashujaa
Jamaa ni msomi wa shahada ya utabibu aliyopata kwenye Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Reliants Lusajo-Mashujaa
Straika huyu wa Mashujaa FC ana shahada ya ugavi na manunuzi aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi mwaka 2010.
Lusaji aliwahi kusema: "Elimu yangu ni msaada mkubwa kwenye soka inanifanya nijue kuyatafsiri mambo kwenye maisha ya kila siku."
Kuna taarifa pia kwamba Lusajo ana shahada ya uzamili, lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea ili kujua ni ya nini.