Kama atatokea mtu akakwambia winga wa kimataifa wa Ghana, Benard Morrison sio mchezaji mzuri atatakiwa akapimwe uwezo wake wa kufikiri.
Hakuna anayebisha kwenye suala la uwezo wake wa uwanjani. Jamaa anajua soka hadi anapilitiliza. Ni fundi aliyezaliwa na kipaji cha kutosha. Kila timu inatamani kummiliki mchezaji kama Morrison kutokana na uwezo wake huo.
Staa huyu ni habari nyingine kwa kusakata soka. Ana uwezo binafsi wa kukokota mpira na kuingia nao ndani ya 18 na kusababisha madhara kwa timu pinzani.
Kwa nini Simba imemuacha?
Chanzo cha kuondoka kwake kilianzia Februari 4, 2022 Simba ilipotoa taarifa ya kusimamishwa kwa staa huyo kutokana na utovu wa nidhamu.
Winga huyo anatuhumiwa kuondoka na kulala nje ya kambi na kurudi asubuhi. Meneja wa Simba, Patrick Rweymamu ndiye aliyegundua kutokuwepo kwa Morrison kambini.
Inadaiwa Rweymamu alifika kambini usiku na Morisson hakuwepo. Meneja huyo alifuatia hadi asubuhi na kugundua muda ambao mchezaji huyo alirudi kambini.
Hapo tena zikaja stori nyingi zikisema Morrison alikuwa na tabia ya kutoka kambini usiku na kwenda kwenye nyendo zake huku akimuaga mlinzi kuwa anakwenda kufanya mazoezi.
Inasemekana aliporudi alikuwa akiilowesha kwa maji jezi yake, ili ionekane ametokwa na jasho kutokana na mazoezi aliyoyafanya.
Morisson alisimamishwa na viongozi wa Simba, ambao tayari walishashachoshwa na vituko vya kila siku vya staa huyo.
Aandika barua kuomba radhi
Kabla ya kuandika barua ya kuomba radhi, winga huyo alitoa kauli ambayo iliwashtua watu wengi katika mitandao ya kijamii akisema kuna jambo zito litatokea muda si mrefu.
Kipindi hicho kulikuwa na tetesi mwekezaji wa Simba Mohammed Dewji ‘MO’ alijiweka pembeni kuitumikia timu hiyo.
Tetesi zilisema bosi huyo hakuwa ametoa mishahara miezi miwili. Ikidaiwa alikuwa amesusa kutokana na timu kutolewa katika Kombe la Shirikisho na Orlando Pirates, Aprili 24, 2022.
Morisson na Chama hawakwenda Afrika Kusini kuitumikia Simba dhidi ya Oralndo Pirates kwa sababu tofauti.
Morisson alikuwa na matatizo ya kuingia Afrika Kusini tangu alipoitumikia Orland Pirates na Chama ni kwa sababu alishaitumikia Berkane FC katika mashindano hayo, hivyo wote walibaki Dar es Salaam.
Baada ya kutolewa, Simba ilikuwa na siku sita kurudi nchini na kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga.
Mechi ya Yanga ilichangia
Kama alivyoondoka Yanga na kujiunga na Simba baada ya mchezo wa Julai 12, 2020 wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), ndivyo inavyotokea sasa anapoondoka Simba na kurudi Yanga.
Kulikuwa na tuhuma za kuisaliti Yanga katika mchezo ule wa ASFC wa mwaka 2020 na sasa zimemtafuna tena katika mchezo wa Ligi Kuu wa Aprili 30, 2022.
Mashabiki wa Simba walikuwa na matumaini na wachezaji wao Morrison, Chama na Pape Sakho dhidi ya Yanga Aprili 30.
Lakini kilichotokea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kilikuwa ni tofauti kabisa.
Tuhuma zinaelekezwa kwa Morisson na Chama kucheza chini ya kiwango. Inadaiwa Morisson alikuwa akiitafuta kadi nyekundu ili Simba icheze pungufu katika mchezo huo.
Katika dakika ya sita tu ya mchezo, Morrison aliudunda mpira chini ili akitaka apewe kona kitendo ambacho kingemfanya aonyeshwe kadi ya njano, Mwamuzi Ramadhani Kayoko akamchunia.
Kama haitoshi katika dakika 26 ya mchezo, Morisson alitaka kumvaa kipa wa Yanga, Djigui Diara lakini Kayoko tena hakumruhusu akamzuia kufanya kitendo hicho ambacho kingeharibu mchezo.
Kipindi cha pili Chama alitolewa na kiungo huyo wa Zambia aliingia katika bifu na Kocha Pablo Franco Martin. Morrison alitolewa dakika ya 54.
Siku 13 baada ya mchezo huo wa watani, Simba ilimwandikia barua ya kumtakia kila la heri Morrison huku kukiwa kumebakiwa na michezo kadhaa za Ligi Kuu.
Pia, Simba ilikuwa na mchezo wa nusu fainali wa ASFC dhidi ya Yanga Mei 28, 2022 katika Uwanja wa CCM Kirumba lakini haikutaka kabisa staa huyo ahusike katika mchezo huo.
Hayo yametokea baada ya viongozi wa klabu hiyo kuvumilia vituko mbalimbali vya staa huyo.
Atawezana na Nabi
Ukizungumza na baadhi ya watu wa Simba, watakwambia jamaa anajua sana mpira ila tabia zake sio za kawaida. Watasema ni vigumu kuishi na mchezaji kama Morisson.
Kocha wa Yanga, Nasrudeen Nabi ni mmoja kati ya makocha wenye kutaka nidhamu ndani ya kikosi chake.
Hivi karibuni, Yanga iliachana na mchezaji wake muhimu, Saido Ntibanzonkiza kwa madai ya utovu wa nidhamu. Ni jukumu la Morrison kubadili mwenendo wake ili aweze kuishi maisha marefu ndani ya kikosi hicho la sivyo, atapotea.
Kama atashindwa kuitumikia Yanga, tusitarajie kumwona staa huyo katika timu yoyote ya Ligi Kuu katika Jiji la Dar es Salaam.